Revised Common Lectionary (Complementary)
Kuja Kwa Ufalme Wa Mungu
(Mt 24:23-28,37-41)
20 Baadhi ya Mafarisayo walimuuliza Yesu, “Ufalme wa Mungu utakuja lini?” Yesu akajibu, “Kuja kwa ufalme wa Mungu si kitu unachoweza kuona. 21 Watu hawatasema, ‘Tazama ufalme wa Mungu uko hapa’ au ‘Ule pale!’ Hapana, Ufalme wa Mungu upo hapa pamoja nanyi.”[a]
22 Kisha Yesu akawaambia wafuasi wake, “Wakati utakuja, ambapo mtatamani angalau kuwa na Mwana wa Adamu hata kwa siku moja, lakini hamtaweza. 23 Watu watawaambia, ‘Tazameni, yuko kule!’ au ‘Tazameni, yuko hapa!’ Kaeni pale mlipo; msitoke kwenda kumtafuta. 24 Iweni na subira kwa sababu Mwana wa Adamu atakaporudi, mtatambua. Siku hiyo atang'aa kama mwanga wa radi umulikavyo angani kutoka upande mmoja hadi mwingine. 25 Lakini kwanza, ni lazima Mwana wa Adamu ateseke kwa mambo mengi na watu wa leo watamkataa.
26 Mwana wa Adamu atakaporudi, itakuwa kama ilivyokuwa Nuhu alipoishi. 27 Watu walikuwa wakila, wakinywa, wakioa na kuolewa hata siku Nuhu alipoingia katika safina. Ndipo gharika ilikuja na kuwaangamiza wote.
28 Ilikuwa vivyo hivyo katika wakati wa Lutu, Mungu alipoteketeza Sodoma. Watu wa Sodoma walikuwa wakila, wakinywa, wakinunua, wakiuza, wakipanda na kujijengea nyumba. 29 Lakini siku ambayo Lutu alitoka Sodoma, moto na baruti vilinyesha kutoka mbinguni na kuwaua wote. 30 Hivi ndivyo itakavyokuwa siku ambayo Mwana wa Adamu atarudi.
31 Siku hiyo, ikiwa mtu atakuwa juu ya paa ya nyumba yake, hatakuwa na muda wa kushuka kwenda ndani ya nyumba kuchukua vitu vyake. Ikiwa atakuwa shambani, hataweza kurudi nyumbani. 32 Kumbukeni yaliyompata mke wa Lutu![b]
33 Kila atakayejaribu kutunza maisha aliyonayo atayaangamiza. Lakini yeyote atakayeyasalimisha maisha yake atayaokoa. 34 Usiku ule watu wawili wataweza kuwa wamelala katika chumba kimoja, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. 35 Wanawake wawili watakuwa wanasaga nafaka pamoja, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.” 36 [c]
37 Wafuasi wake wakamuuliza, “Hii itakuwa wapi Bwana?”
Yesu akajibu, “Ni kama kuutafuta mzoga, utaupata pale ambapo tai wamekusanyika.”
© 2017 Bible League International