Revised Common Lectionary (Complementary)
Mungu ni Mwaminifu Na Atauadhibu Uovu
18 Mungu huonesha hasira yake kutokea mbinguni dhidi ya mambo mabaya ambayo waovu hutenda. Hawamheshimu na wanatendeana mabaya. Maisha yao maovu yanasababisha ukweli kuhusu Mungu usijulikane. 19 Hili humkasirisha Mungu kwa sababu wamekwisha oneshwa Mungu alivyo. Ndiyo, Mungu ameliweka wazi kwao.
20 Yapo mambo yanayoonekana kuhusu Mungu, kama vile nguvu zake za milele na yale yote yanayomfanya awe Mungu. Lakini tangu kuumbwa kwa ulimwengu, mambo haya yamekuwa rahisi kwa watu kuyaona. Maana yake ni kuwa, watu wanaweza kumwelewa Mungu kwa kuangalia yale aliyoumba. Hivyo watu hawana udhuru kwa uovu wanaotenda.
21 Watu walimjua Mungu, lakini hawakumheshimu kama Mungu. Na hawakumpa shukrani. Badala yake waliyageukia mambo ya hovyo yasiyo na manufaa. Akili zao zilichochanganyikiwa zilijaa giza. 22 Walisema kuwa wana hekima, lakini wakawa wajinga. 23 Hawakuuheshimu ukuu wa Mungu, anayeishi milele. Wakaacha kumwabudu Mungu wakaanza kuabudu sanamu, vitu vilivyotengenezwa vikaonekana kama wanadamu, ambao wote mwisho hufa, au kwa mfano wa ndege na wanyama wanaotembea na wanaotambaa.
24 Hivyo Mungu akawaacha wazifuate tamaa zao chafu. Wakawa najisi na wakaivunjia heshima miili yao kwa njia za uovu walizotumia. 25 Waliibadili kweli kuhusu Mungu kwa uongo. Wakasujudu na kuabudu vitu alivyoviumba Mungu badala ya kumwabudu Mungu aliyeviumba vitu hivyo. Yeye ndiye anayepaswa kusifiwa milele yote. Amina.
© 2017 Bible League International