Revised Common Lectionary (Complementary)
Paulo Ajitetea Mbele ya Feliki
10 Gavana alifanya ishara ili Paulo aanze kuzungumza. Hivyo Paulo alijibu, “Gavana Feliki, ninafahamu kuwa umekuwa jaji wa nchi hii kwa muda mrefu. Hivyo ninafurahi kujitetea mimi mwenyewe mbele yako. 11 Nilikwenda kuabudu Yerusalemu siku kumi na mbili tu zilizopita. Unaweza kutambua wewe mwenyewe kuwa hii ni kweli. 12 Wayahudi hawa wanaonishitaki, hawakuniona nikibishana na mtu yeyote wala kukusanya kundi la watu Hekaluni. Na sikuwa nabishana au kufanya vurugu kwenye masinagogi au mahali popote katika mji. 13 Watu hawa hawawezi kuthibitisha mambo wanayoyasema dhidi yangu sasa.
14 Lakini nitakuambia hili: Ninamuabudu Mungu, Mungu yule yule aliyeabudiwa na baba zetu, na kama mfuasi wa Njia, ambayo wayahudi hawa wanasema si njia sahihi. Na ninaamini kila kitu kinachofundishwa katika Sheria ya Musa na yote yaliyoandikwa katika vitabu vya manabii. 15 Nina tumaini katika Mungu kama walilonalo Wayahudi hawa, kwamba watu wote, wema na wabaya, watafufuliwa kutoka kwa wafu. 16 Hii ndiyo sababu daima nimejaribu kufanya kile ninachoamini kuwa sahihi mbele za Mungu na kila mtu.
17-18 Nimekuwa mbali na Yerusalemu kwa miaka mingi. Nilikwenda kule nikiwa na fedha za kuwasaidia watu wangu. Pia nilikuwa na sadaka za kutoa Hekaluni. Nilipokuwa nafanya hivyo, baadhi ya Wayahudi waliponiona pale. Nilikuwa nimemaliza ibada ya utakaso.[a] Sikufanya vurugu yoyote, na hakuna watu waliokuwa wamekusanyika kunizunguka. 19 Lakini baadhi ya Wayahudi kutoka Asia walikuwa pale. Walipaswa kuwa hapa mbele yako wakinishtaki ikiwa wana ushahidi kuwa nilifanya kitu chochote kibaya. 20 Waulize watu hawa ikiwa waliona kosa lolote kwangu niliposimama mbele ya mkutano wa baraza kuu mjini Yerusalemu. 21 Jibu pekee watakaloweza kukujibu ni hili: Kwamba nilipokuwa mbele zao nilipaza sauti na kusema, ‘Mnanishitaki leo kwa sababu ninaamini watu watafufuka kutoka kwa wafu!’”
22 Feliki tayari alikuwa anaelewa mengi kuhusu Njia. Akasimamisha kesi na kusema, “Kamanda Lisiasi atakapokuja hapa, nitaamua nini cha kufanya.” 23 Feliki alimwambia ofisa wa jeshi kumlinda Paulo lakini wampe uhuru kiasi na wawaruhusu rafiki zake wamletee chochote atakachohitaji.
© 2017 Bible League International