Revised Common Lectionary (Complementary)
1 Salamu kutoka kwa Paulo, Sila na Timotheo.
Kwa kanisa la Thesalonike lililo mali ya Mungu baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo.
2 Neema na amani viwe kwenu kutoka kwa Mungu Baba na Bwana wetu Yesu Kristo.
3 Kaka na dada zetu, tunamshukuru Mungu kwa ajili yenu. Na hivyo ndivyo tunavyopaswa kufanya, kwani mnatupa sababu ya kushukuru na imani yenu inakua zaidi na zaidi. Pamoja na hilo upendo ambao kila mmoja wenu anao kwa mwenzake nao unakua. 4 Hivyo tunayaeleza makanisa mengine ya Mungu namna tunavyojivuna kuhusu ninyi. Tunawaeleza jinsi mlivyoendelea kwa subira kuwa imara na waaminifu, ingawa mnateswa na kusumbuliwa na matatizo mengi.
11 Hii ndiyo sababu daima tunawaombea. Tunamwomba Mungu wetu awasaidie kuishi katika njia njema aliyoitaka alipowachagua. Wema mlionao unawafanya mtake kufanya mema. Na imani mliyonayo inafanya mfanye kazi. Tunaomba kwamba kupitia nguvu zake Mungu atayakamilisha yote mema mliyokusudia kufanya pamoja na kazi zote zinazotokana na imani yenu. 12 Kisha jina la Bwana wetu Yesu litaheshimiwa kwa sababu yenu, nanyi mtaheshimiwa kwa sababu yake, na mtaheshimiwa kwa sababu yake. Hii inaweza kutokea tu kwa neema ya Mungu wetu na Bwana Yesu Kristo.
Zakayo
19 Yesu alikuwa anasafiri kupitia katika mji wa Yeriko. 2 Katika mji wa Yeriko alikuwepo mtu aliyeitwa Zakayo. Alikuwa mtoza ushuru mkuu na alikuwa tajiri. 3 Alitaka kumwona Yesu na watu wengine wengi walitaka kumwona Yesu pia. Lakini alikuwa mfupi na hakuweza kuona juu ya watu. 4 Hivyo alikimbia akaenda mahali alipojua kuwa Yesu angepita. Kisha akapanda mkuyu ili aweze kumwona Yesu.
5 Yesu alipofika mahali alipokuwa Zakayo, alitazama juu na kumwona akiwa kwenye mti. Yesu akasema, “Zakayo, shuka upesi! Ni lazima nikae nyumbani mwako leo.”
6 Zakayo alishuka chini haraka. Alifurahi kuwa na Yesu nyumbani mwake. 7 Kila mtu aliliona hili na watu wakaanza kulalamika, wakisema, “Tazama aina ya mtu ambaye Yesu anakwenda kukaa kwake. Zakayo ni mwenye dhambi!”
8 Zakayo akamwambia Bwana, “Sikiliza Bwana nitawapa maskini nusu ya pesa zangu. Ikiwa nilimdhulumu mtu yeyote, nitamrudishia mara nne zaidi.”
9 Yesu akasema, “Leo ni siku kwa ajili ya familia hii kuokolewa kutoka katika dhambi. Ndiyo, hata mtoza ushuru huyu ni mmoja wa wateule wa Mungu.[a] 10 Mwana wa Adamu alikuja kuwatafuta na kuwaokoa watu waliopotea.”
© 2017 Bible League International