Revised Common Lectionary (Complementary)
6 Kwangu mimi, nimemiminwa kama kinywaji cha sadaka, na wakati wa kuondoka kwangu kutoka katika maisha haya umekwisha kufika. 7 Nimejihusisha katika mashindano ya thamani; nimemaliza mbio; nimeilinda imani. 8 Sasa tuzo ya mshindi inaningoja, hii ni taji inatolewa kwa wenye haki. Bwana, aliye hakimu wa haki atanipa taji hiyo katika Siku ile. Ndio atanipa mimi na yeyote mwingine anayengojea kwa dhati kuja kwake.
16 Mara ya kwanza nilipokuwa nafanya utetezi wangu, hakuna hata mmoja aliyekuja kunisaidia. Badala yake wote wakaniacha. Na wasihesabiwe hayo na Mungu. 17 Lakini Bwana akasimama upande wangu na kunitia nguvu, ili ujumbe uweze kunenwa nami kwa ukamilifu ili kwamba Mataifa wote waweze kusikia. Na nikaokolewa kutoka katika mdomo wa simba. 18 Bwana ataniokoa kutokana na kila mashambulizi maovu na atanileta salama katika Ufalme wake wa mbinguni. Utukufu uwe wake milele na milele. Amina.
Farisayo na Mtoza Ushuru
9 Walikuwepo baadhi ya watu waliojiona kuwa wenye haki na waliwadharau wengine. Yesu alitumia simulizi hii kuwafundisha: 10 “Siku moja Farisayo na mtoza ushuru walikwenda Hekaluni kuomba. 11 Farisayo alisimama peke yake mbali na mtoza ushuru. Farisayo aliomba akisema, ‘Ee Mungu, ninakushukuru kwa kuwa mimi si mwovu kama watu wengine. Mimi siyo kama wezi, waongo au wazinzi. Ninakushukuru kwa kuwa mimi ni bora kuliko huyu mtoza ushuru. 12 Ninafunga mara mbili kwa wiki na kutoa sehemu ya kumi ya vyote ninavyopata!’
13 Mtoza ushuru alisimama peke yake pia. Lakini alipoanza kuomba, hakuthubutu hata kutazama juu mbinguni. Alijipigapiga kifua chake akijinyenyekeza mbele za Mungu. Akasema, ‘Ee Mungu, unihurumie, mimi ni mwenye dhambi.’ 14 Ninawaambia, mtu huyu alipomaliza kuomba na kwenda nyumbani, alikuwa amepatana na Mungu. Lakini Farisayo, aliyejisikia kuwa bora kuliko wengine, hakuwa amepatana na Mungu. Watu wanaojikweza watashushwa. Lakini wale wanaojishusha watakwezwa.”
© 2017 Bible League International