Revised Common Lectionary (Complementary)
Kutatua Migogoro Miongoni Mwa Waamini
6 Kwa nini mnakwenda kwenye mahakama za kisheria mmoja wenu anapokuwa na shauri dhidi ya mwingine aliye miongoni mwenu? Mnajua ya kwamba mahakimu wa aina hiyo hawawezi kutegemewa kuamua kwa haki iliyo ya kweli. Sasa kwa nini mnawaruhusu wawaamulie aliye na haki? Kwa nini msiwaruhusu watakatifu wa Mungu waamue ni nani aliye na haki? 2 Hamjui kuwa watakatifu wa Mungu watauhukumu ulimwengu? Hivyo, ikiwa mtauhukumu ulimwengu, hakika mnaweza kutatua mashauri kama hayo miongoni mwenu. 3 Hakika mnajua kuwa tutawahukumu malaika. Kwa kuwa hiyo ni kweli basi hakika tunaweza kuhukumu masuala ya kawaida ya maisha. 4 Sasa, ikiwa mna masuala kama haya ya kawaida ya maisha yanayotakiwa kuamuliwa, kwa nini mnayapeleka kwa wasio waamini? Hao ambao hawana umuhimu wo wote kwenu? 5 Ninasema hivi ili kuwatahayarisha. Nina uhakika yupo mwenye hekima miongoni mwa waamini katika kanisa lenu anayeweza kutatua mgogoro kati ya waamini wawili. 6 Lakini sasa mwamini mmoja anamshtaki mwamini mwenzake na mnaruhusu watu wasio waamini wawaamulie!
7 Ule ukweli kuwa mnayo mashitaka baina yenu ninyi kwa ninyi tayari ni uthibitisho wa kushindwa kwenu kabisa. Ingekuwa bora kwenu kustahimili yasiyo haki ama kulaghaiwa. 8 Lakini ninyi ndiyo mnaotenda mabaya kwa kudanganya. Na mnawafanyia hivi ndugu zenu katika Kristo!
9 Msijidanganye. Hamjui ya kuwa wanaowatendea mabaya hawana nafasi katika ufalme wa Mungu. Ninasema kuhusu wazinzi, wanaoamini miungu wa uongo, wasio waaminifu katika ndoa, nao wanaolawitiana.[a] 10 Pia wezi, walafi, walevi, watukanaji, au waongo wanaowadanganya wengine ili wawaibie hawatakuwa na sehemu katika ufalme wa Mungu. 11 Baadhi yenu mlikuwa hivyo huko nyuma. Lakini mlisafishwa mkawa safi, mkafanywa kuwa watakatifu na mkahesabiwa haki na Mungu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo na kwa Roho wa Mungu wetu.
© 2017 Bible League International