Revised Common Lectionary (Complementary)
8 Endelea kumkumbuka Yesu Kristo, aliyefufuka kutoka kwa wafu, na ni kutoka ukoo wa Daudi. Na huu ndiyo Habari Njema ninayoihubiri. 9 Kwa sababu ya Habari Njema ninateseka, hadi hatua ya kufungwa kwa minyororo kama mhalifu. Lakini ujumbe wa Mungu haujafungwa. 10 Kwa hiyo nayavumilia yote kwa ajili ya wateule wa Mungu, ili na wao waweze kuufikia wokovu unaopatikana katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele.
11 Na hapa kuna usemi wa kuaminiwa:
Kama tumekufa pamoja naye,
tutaweza kuishi naye pia.
12 Kama tutastahimili, tutaweza pia kumiliki pamoja naye.
Kama tutamkana yeye, naye atatukana sisi.
13 Kama hatutakuwa waaminifu,
yeye anabaki kuwa mwaminifu,
kwa sababu hawezi kujikana mwenyewe.
Mtendakazi Ampendezaye Mungu
14 Endelea kuwakumbusha watu juu ya mambo haya. Waonye kwa mamlaka mbele za Mungu wasipigane juu ya maneno. Mapigano hayo hayana mambo mazuri, bali huwaharibu wanaoyasikiliza. 15 Jitahidi kujionesha mwenyewe kuwa umekubaliwa na Mungu, kama mtumishi asiye na kitu cho chote cha kumfadhaisha na anayeufanyia kazi ujumbe wa kweli ya Mungu katika njia sahihi.
Yesu Awaponya Baadhi ya Wayahudi na Msamaria
11 Yesu alikuwa anasafiri kwenda Yerusalemu. Alipotoka Galilaya alisafiri akipita kando ya mpaka wa Samaria. 12 Aliingia katika mji mdogo, na wanaume kumi walimwendea. Hawakumkaribia, kwa sababu wote walikuwa na ugonjwa mbaya sana wa ngozi. 13 Lakini watu wale wakaita kwa kupaza sauti wakisema, “Yesu! Mkuu! Tafadhali utusaidie!”
14 Yesu alipowaona, akasema, “Nendeni mkajioneshe kwa makuhani.”[a]
Wale watu kumi walipokuwa wanakwenda kujionesha kwa makuhani, waliponywa. 15 Mmoja wao alipoona kuwa amepona, alirudi kwa Yesu huku akimsifu Mungu kwa kupaza sauti. 16 Akaanguka kifudifudi miguuni pa Yesu, akamshukuru. (Alikuwa Msamaria.) 17 Yesu akasema, “Watu kumi wameponywa, wengine tisa wako wapi? 18 Mtu huyu wala si mmoja wa watu wetu. Ni yeye peke yake aliyerudi kumsifu Mungu?” 19 Ndipo Yesu akamwambia, “Inuka! Unaweza kwenda. Umeponywa kwa sababu uliamini.”
© 2017 Bible League International