Revised Common Lectionary (Complementary)
Barua ya Yesu kwa Kanisa la Pergamo
12 Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Pergamo:
Huu ni ujumbe kutoka kwake aliye na upanga wenye makali kuwili unaotoka katika kinywa chake.
13 Ninapafahamu mahali unapoishi. Unaishi mahali kilipo kiti cha enzi cha Shetani, lakini wewe ni mwaminifu kwangu. Hukukataa kueleza kuhusu imani yako kwangu hata wakati wa Antipa. Antipa alikuwa shahidi wangu mwaminifu[a] aliyeuawa katika mji wako, mji ambao shetani anaishi.
14 Lakini nina vitu vichache kinyume nawe. Una watu huko wanaofuata mafundisho ya Balaamu. Balaamu alimfundisha Balaki namna ya kuwafanya watu wa Israeli kutenda dhambi. Walitenda dhambi kwa kula vyakula vilivyotolewa kwa ajili ya sanamu na kwa kufanya uzinzi. 15 Ndivyo ilivyo hata kwa kundi lako. Una watu wanaofuata mafundisho ya Wanikolai. 16 Hivyo igeuzeni mioyo yenu! Msipobadilika, nitakuja kwenu haraka na kupigana kinyume na watu hawa kwa kutumia upanga unaotoka katika kinywa changu.
17 Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa!
Kila atakayeshinda nitampa mana iliyofichwa. Pia nitampa kila mshindi jiwe jeupe lililoandikwa jina jipya juu yake. Na hakuna atakayejua jina hili isipokuwa yule atakayepata jiwe hili.
Barua ya Yesu kwa Kanisa la Thiatira
18 Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira:
Huu ni ujumbe kutoka kwa Mwana wa Mungu, aliye na macho yanayong'aa kama moto na miguu kama shaba inayong'aa.
19 Ninayajua matendo yako. Ninajua kuhusu upendo wako, imani yako, huduma yako na uvumilivu wako. Ninajua kwamba unafanya zaidi sasa kuliko ulivyofanya kwanza. 20 Lakini ninalo hili kinyume nawe: Umemruhusu yule mwanamke Yezebeli afanye anachotaka. Anasema kwamba yeye ni nabii,[b] lakini anawapotosha watu wangu kwa mafundisho yake. Yezebeli huwaongoza watu wangu kutenda dhambi ya uzinzi na kula vyakula vilivyotolewa kwa sanamu. 21 Nimempa muda ili aubadili moyo wake na kuiacha dhambi yake, lakini hataki kubadilika.
22 Hivyo nitamtupa kwenye kitanda cha mateso. Na wale wote wanaozini naye watateseka sana. Nitafanya hivi sasa ikiwa hawataacha mambo anayofanya. 23 Pia, nitawaua wafuasi wake. Ndipo makanisa yote wataona kuwa mimi ndiye ninayefahamu kile ambacho watu wanadhani na kufikiri. Na nitamlipa kila mmoja wenu kutokana na kile alichotenda.
24 Lakini ninyi wengine mlioko Thiatira ambao hamjafuata mafundisho yake. Hamjajifunza mambo yanayoitwa ‘Siri za ndani za Shetani.’ Hivi ndivyo ninawaambia: Sitawatwika mzigo wowote. 25 Shikeni katika kweli mliyo nayo tu mpaka nitakapo kuja.
26 Nitawapa nguvu juu ya mataifa wale wote watakaoshinda na wakaendelea kutenda yale ninayotaka mpaka mwisho. 27 Watayatawala mataifa kwa fimbo ya chuma. Watayavunja vipande vipande kama vyombo vya udongo wa mfinyanzi.[c] 28 Watakuwa na nguvu ile ile niliyoipokea kutoka kwa Baba yangu, na nitawapa nyota ya asubuhi. 29 Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa.
© 2017 Bible League International