Revised Common Lectionary (Complementary)
3 Je, Wayahudi wana upendeleo wowote kuliko wengine? Je, tohara yao inawasaidia lolote jema? 2 Ndiyo, Wayahudi wana upendeleo mwingi. Lililo muhimu zaidi ni kuwa: Mungu aliwaamini akawapa kazi ya kuzitangaza ahadi zake kwa watu wote. 3 Ni kweli kuwa baadhi ya Wayahudi hawakuwa waaminifu kufanya yale Mungu aliyotaka. Lakini je, hilo laweza kumzuia Mungu kutenda kwa uaminifu yale aliyoahidi? 4 Hapana! Hata ikiwa wengine wote watashindwa kutimiza ahadi zao, daima, Mungu atatekeleza aliyosema. Kama Maandiko yanavyosema kuhusu Mungu,
“Utathibitika kuwa mwenye haki kwa maneno yako,
na utashinda utakaposhitakiwa na watu.”(A)
5 Lakini hivi ndivyo wengine hufikiri: Tunapotenda mabaya, inaonesha wazi kuwa Mungu ni wa haki. Je, tunaweza kusema kwamba Mungu hatutendei haki anapotuadhibu? 6 Hapana. Ikiwa Mungu si wa haki atawezaje kuuhukumu ulimwengu?
7 Ninaposema uongo, inamletea Mungu utukufu, kwa sababu uongo wangu hurahisisha ionekane kuwa yeye ni wa kweli. Hivyo kwa nini nihukumiwe kama mtenda dhambi? 8 Na kwa nini tusiseme, “Tufanye maovu ili jambo jema litokee humo.” Baadhi ya watu wanadai kuwa hivyo ndivyo tunavyofundisha! Wahukumiwe kwa kusema hivyo.
© 2017 Bible League International