Revised Common Lectionary (Complementary)
Shukrani kwa Rehema za Mungu
12 Ninamshukuru Kristo Yesu Bwana wetu kwa sababu aliniamini na kunipa kazi hii ya kumtumikia. Yeye hunitia nguvu ya kufanya kazi hii. 13 Hapo zamani nilimtukana Kristo. Nikiwa mtu mwenye majivuno na mkorofi, niliwatesa watu wake. Lakini Mungu alinihurumia kwa sababu sikujua nilichokuwa nafanya. Nilifanya hayo kabla sijaamini. 14 Lakini Bwana wetu alinipa kiwango kikubwa cha neema yake. Na pamoja na neema hiyo imani na upendo ulio katika Kristo Yesu vilifuata.
15 Huu ndiyo usemi wa kweli unaopaswa kukubaliwa pasipo kuuliza maswali; kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuokoa wenye dhambi, nami ni mbaya zaidi ya wote. 16 Lakini nilipata rehema kwa sababu ili Kristo Yesu aweze kunitumia, mimi mtenda dhambi kuliko wote, ili kuonesha uvumilivu wake usio na kikomo. Alitaka niwe mfano kwa wale ambao wangemwamini na kupata uzima wa milele. 17 Heshima na utukufu kwa mfalme anayetawala milele. Hawezi kuharibiwa wala kuonekana. Heshima na utukufu apewe Mungu wa pekee milele na milele, Amina.
Furaha Mbinguni
(Mt 18:12-14)
15 Watoza ushuru na wenye dhambi wengi waliendelea kuja kumsikiliza Yesu. 2 Hivyo Mafarisayo na walimu wa sheria wakaanza kulalamika wakisema, “Mtazameni mtu huyu[a] huwakaribisha wenye dhambi na hata kula pamoja nao!”
3 Hivyo Yesu akawaambia mfano huu, 4 “Chukulia mmoja wenu ana kondoo mia, lakini mmoja akapotea. Utafanya nini? Utawaacha wale tisini na tisa na kwenda kumtafuta yule mmoja aliyepotea mpaka umpate. 5 Na ukishampata, utafurahi sana. Utambeba mabegani mwako 6 mpaka nyumbani. Kisha utakwenda kwa majirani na rafiki zako na utawaambia, ‘Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimempata kondoo wangu aliyepotea!’ 7 Katika namna hiyo hiyo ninawaambia, kunakuwa na furaha zaidi mbinguni kwa sababu ya mtu anayeacha dhambi zake. Kuna furaha zaidi kwa ajili ya mtu mmoja anayeacha dhambi kuliko watu wema tisini na tisa ambao hudhani hawahitaji kubadilika.
8 Fikiria kuhusu mwanamke mwenye sarafu kumi za fedha,[b] lakini akapoteza sarafu moja kati ya hizo. Atawasha taa na kuifagia nyumba. Ataitafuta sarafu kwa bidii mpaka aione. 9 Na akiiona, atawaita rafiki na jirani zake na kuwaaambia, ‘Furahini pamoja nami, kwa sababu nimeipata sarafu niliyoipoteza!’ 10 Katika namna hiyo hiyo, ni furaha kwa malaika wa Mungu, mwenye dhambi mmoja anapotubu.”
© 2017 Bible League International