Revised Common Lectionary (Complementary)
1 Kutoka kwa Paulo mfungwa kwa kusudi la Kristo Yesu,[a] na kutoka kwa Timotheo ndugu yetu. Kwa Filemoni rafiki yetu mpendwa na mtenda kazi pamoja nasi; 2 kwa Afia dada yetu, Arkipo askari mwenzetu na kwa kanisa linalokutania nyumbani mwako.
3 Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo ziwe pamoja nawe.
Upendo na Imani ya Filemoni
4 Namshukuru Mungu wangu siku zote kila ninapokukumbuka katika maombi yangu, 5 kwa sababu nasikia juu ya upendo na uaminifu ulionao katika Bwana Yesu na unaouonesha kwa watu wa Mungu. 6 Ninaomba kwamba ile imani unayoishiriki pamoja nasi ikusaidie wewe kuelewa kila fursa tulio nayo ya kutenda mema kama wale tunaomwamini Kristo. 7 Nimepokea furaha kubwa na faraja kutokana na upendo wako, kwa sababu mioyo ya watu wa Mungu imepata nguvu mpya kwa juhudi zako ndugu yangu.
Mpokee Onesimo Kama Kaka
8 Hivyo hiyo ndiyo sababu nakuagiza wewe kufanya jambo unalopaswa kulifanya. Kwa mamlaka niliyo nayo katika Kristo naweza kukuamuru kufanya hilo. 9 Lakini sikuamuru; bali kwa sababu ya upendo nakusihi ufanye hivyo. Mimi Paulo, niliye mzee wa umri sasa, na sasa mfungwa kwa ajili ya Kristo Yesu. 10 Ninakusihi kuhusu mwanangu Onesimo niliyemleta[b] katika maisha mapya tulio nayo katika Bwana nilipokuwa gerezani. 11 Huyo ambaye siku za nyuma hakuwa wa manufaa kwako, lakini sasa anafaa[c] sio kwako tu bali hata kwangu mimi.
12 Ninamrudisha kwako, kitu ambacho kimekuwa kigumu sawa na kuupoteza moyo wangu.[d] 13 Ningetamani kuendelea kuwa naye hapa, ili aendelee kunihudumia kwa niaba yako nitakapokuwa bado gerezani kwa ajili ya Habari Njema. 14 Lakini sikuwa tayari kufanya jambo lo lote bila ruhusa yako, ili kila jambo lako zuri litendeke bila lazima bali kwa hiari yako mwenyewe.
15 Labda sababu ya Onesimo kutenganishwa nawe kwa kipindi kifupi ni kuwezesha muwe pamoja siku zote, 16 si mtumwa tena, bali ni zaidi ya mtumwa; kama ndugu mpendwa. Nampenda sana lakini wewe utampenda zaidi, sio tu kama kaka katika familia yenu, bali pia kama mmoja wa walio katika familia ya Bwana.
17 Ikiwa unanitambua mimi kama niliye mwenye imani moja nawe, basi mpokee Onesimo na umkubali kama vile ambavyo ungenikubali. 18 Endapo amekukosea jambo lo lote au unamdai kitu cho chote, unidai mimi badala yake. 19 Mimi Paulo naandika kwa mkono wangu mwenyewe ya kwamba nitakulipa. Tena sina sababu ya kukumbusha kuwa una deni kwangu juu ya maisha yako. 20 Kwa hiyo kaka yangu, kama mfuasi wa Bwana, tafadhali nipe upendeleo[e] katika hili. Ndipo itakuwa faraja kuu kwangu kama kaka yako katika Kristo. 21 Ninapokuandikia barua hii nina ujasiri mkubwa kwamba utakubaliana nami na najua kwamba utafanya zaidi ya haya ninayokuomba.
Amua Ikiwa Unaweza Kunifuata
(Mt 10:37-38)
25 Watu wengi walikuwa wanasafiri pamoja na Yesu. Akawaambia, 26 “Ikiwa unakuja kwangu na hauko tayari kuiacha familia yako, huwezi kuwa mfuasi wangu. Ukimpenda zaidi baba yako, mama yako, mke wako, watoto wako, kaka na dada zako na hata maisha yako zaidi yangu huwezi kuwa mwanafunzi wangu. 27 Yeyote ambaye hatauchukua msalaba atakaopewa na akanifuata, hawezi kuwa mfuasi wangu.
28 Ikiwa unataka kujenga nyumba, kwanza utakaa na kuamua ili kujua itakugharimu kiasi gani. Ni lazima uone ikiwa una pesa za kutosha kumaliza kazi ya ujenzi. 29 Usipofanya hivyo, unaweza ukaanza kazi, lakini ukashindwa kumaliza kujenga nyumba. Na usipoweza kuimaliza, kila mtu atakucheka, 30 Watasema, ‘Mtu huyu alianza kujenga, lakini alishindwa kumalizia.’
31 Ikiwa mfalme anakwenda kupigana vita na mfalme mwingine, atakaa chini kwanza na kupanga. Ikiwa ana askari elfu kumi, ataamua ikiwa ana uwezo wa kumshinda mfalme mwenye askari elfu ishirini. 32 Akiona hawezi kumshinda mfalme mwingine, atatuma baadhi ya watu kwa mfalme mwingine ili wapatane akiwa bado yuko mbali.
33 Ndivyo ilivyo kwa kila mmoja wenu. Lazima uache kila kitu ulichonacho. La sivyo, huwezi kuwa mfuasi wangu.
© 2017 Bible League International