Revised Common Lectionary (Complementary)
Habari Kuhusu Wale Walio Pamoja na Paulo
7 Tikiko ni ndugu yangu mpendwa katika Kristo. Yeye ni msaidizi mwaminifu na anamtumikia Bwana pamoja nami. Atawaambia kila kitu kuhusu mimi. 8 Hii ndiyo sababu ninamtuma, ninataka mfahamu hali yetu, na ninamtuma awatie moyo ninyi. 9 Ninamtuma yeye pamoja na Onesimo, ndugu mpendwa na mwaminifu kutoka kwenye kundi lenu. Watawaeleza kila kitu kilichotokea hapa.
10 Aristarko, aliyefungwa pamoja nami humu gerezani anawasalimu. Marko, binamu yake Barnaba anawasalimu pia. (Nimekwisha kuwaambia kuhusu Marko. Ikiwa atakuja, mpokeeni.) 11 Pia pokeeni salamu toka kwa Yesu, aitwaye pia Yusto. Hawa ni Wayahudi waamini pekee wanaofanya kazi pamoja nami kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Wamekuwa faraja kubwa sana kwangu.
12 Epafra, mtumishi mwingine wa Yesu Kristo, kutoka kwenu anawasalimu. Yeye anahangaika kwa ajili yenu kwa kuwaombea mara kwa mara, ili mkue kiroho na kupokea kila kitu ambacho Mungu anataka kwa ajili yangu. 13 Ninafahamu kwamba amefanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu ninyi na kwa ajili ya watu wa Laodikia na Hierapoli. 14 Pokeeni pia salamu kutoka kwa Dema na kutoka kwa rafiki yetu mpendwa Luka ambaye ni tabibu.
15 Wasalimuni kaka na dada zetu walioko Laodikia. Msalimuni pia Nimfa na kanisa lililo katika nyumba yake. 16 Baada ya kusoma barua hii, ipelekeni katika kanisa la Laodikia, ili isomwe huko pia. Ninyi nanyi msome barua niliyowaandikia wao. 17 Mwambieni Arkipo hivi, “Hakikisha unaifanya kazi aliyokupa Bwana.”
© 2017 Bible League International