Revised Common Lectionary (Complementary)
29 Na watu wa Mungu wote wakatembea kuvuka Bahari ya Shamu kama vile ilikuwa ni ardhi kavu. Waliweza kufanya hivi kwa sababu walikuwa na imani. Lakini wakati Wamisri walipojaribu kuwafuata, wote wakazama majini.
30 Na kuta za Yeriko zilianguka kwa ajili ya imani ya watu wa Mungu. Walitembea kuuzunguka ukuta kwa siku saba, na kisha kuta zikaanguka.
31 Na Rahabu, yule kahaba, aliwakaribisha wapelelezi wa Kiisraeli kama marafiki. Na kwa sababu ya imani yake, hakuuawa pamoja na wale waliokataa kutii.
32 Je, nahitaji niwape mifano zaidi? Sina muda wa kutosha kuwaeleza kuhusu Gidioni, Baraki, Samsoni, Yefta, Daudi, Samweli na manabii. 33 Wote walikuwa na imani kuu. Na kwa njia ya imani hiyo wakaziangusha falme. Wakafanya kilichokuwa sahihi, na Mungu akawasaidia katika njia alizoahidi. Kwa imani zao watu wengine waliifunga midomo ya simba. 34 Na wengine waliweza kuizuia miali ya moto. Wengine wakaepuka katika kuuawa kwa upanga. Wengine waliokuwa dhaifu wakafanywa wenye nguvu. Wakawa na nguvu katika vita na kuyaangusha majeshi mengine. 35 Walikuwepo wanawake waliowapoteza wapendwa wao lakini wakawapata tena walipofufuliwa kutoka wafu. Wengine waliteswa lakini wakakataa kuukubali uhuru wao. Walifanya hivi ili waweze kufufuliwa kutoka kifoni kuingia katika maisha bora zaidi. 36 Wengine walichekwa na kupigwa. Wengine walifungwa na kutiwa magerezani. 37 Waliuawa kwa mawe. Walikatwa vipande viwili. Waliuawa kwa panga. Mavazi pekee wengine wao waliyokuwa nayo yalikuwa ni ngozi za kondoo au za mbuzi. Walikuwa maskini, waliteswa, na kutendewa mabaya na wengine. 38 Ulimwengu haukustahili kuwa na watu wakuu na waaminifu kama hawa. Hawa waliweza kuzunguka jangwani na milimani, wakiishi katika mapango na mashimo ardhini.
39 Mungu alifurahishwa nao wote kwa sababu ya imani zao. Lakini hakuna hata mmoja wao aliyepokea ahadi ya Mungu. 40 Mungu alikusudia kitu bora zaidi kwa ajili yetu. Alitaka kutukamilisha sisi. Hakika, pia alitaka watu hawa wakuu wakamilishwe, lakini siyo kabla ya sisi wote kuzifurahia baraka pamoja.
Sisi Pia Tuufuate Mfano wa Yesu
12 Tunao hawa watu mashuhuri wakituzunguka kama mifano kwetu. Maisha yao yanatueleza imani ni nini. Hivyo, nasi pia, tunapaswa kufanya mashindano yaliyo mbele yetu na kamwe tusikate tamaa. Tunapaswa kuondoa katika maisha yetu kitu chochote kitakachotupunguzia mwendo pamoja na dhambi zinazotufanya tutoke kwenye mstari mara kwa mara. 2 Hatupaswi kuacha kumwangalia Yesu. Yeye ndiye kiongozi wa imani yetu, na ndiye anayeikamilisha imani yetu. Aliteseka hadi kufa msalabani. Lakini aliikubali aibu ya msalaba kama kitu kisicho na maana kwa sababu ya furaha ambayo angeiona ikimngojea. Na sasa ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.
Kumfuata Yesu Kunaleta Matatizo
(Mt 10:34-36)
49 Yesu aliendelea kusema: “Nimekuja kuleta moto ulimwenguni. Ninatamani ungekuwa unawaka tayari! 50 Kuna aina ya ubatizo[a] ambao ni lazima niupitie na niteseke. Ninajisikia kusumbuka mpaka pale utakapotimizwa. 51 Mnadhani nilikuja kuleta amani ulimwenguni? Hapana, nilikuja kuugawa ulimwengu! 52 Kuanzia sasa, familia ya watu watano itagawanyika, watatu watakuwa kinyume cha wawili, na wawili kinyume cha watatu.
53 Kina baba watakuwa kinyume cha wana wao:
na wana nao watakuwa kinyume cha baba zao.
Kina mama watakuwa kinyume cha binti zao:
na binti nao watakuwa kinyume cha mama zao.
Mama wakwe watakuwa kinyume cha wake za wana wao,
na wake za wana wao watakuwa kinyume cha mama wakwe zao.”[b]
Kuzielewa Nyakati
(Mt 16:2-3)
54 Ndipo Yesu akawaambia watu, “Mnapoona wingu likikua upande wa magharibi, mnasema, ‘Mvua inakuja,’ na muda si mrefu huanza kunyesha. 55 Mnapoona upepo unaanza kuvuma kutoka kusini mnasema, ‘Kutakuwa joto,’ na huwa hivyo. 56 Enyi wanafiki! Mnaweza kuiona nchi na anga na mkajua hali ya hewa itakavyokuwa. Kwa nini hamwelewi kinachotokea sasa?
© 2017 Bible League International