Revised Common Lectionary (Complementary)
17-18 Mungu aliijaribu imani ya Ibrahimu. Mungu alimtaka amtoe Isaka kama sadaka. Ibrahimu akatii kwa sababu alikuwa na imani. Tayari alikuwa na ahadi kutoka kwa Mungu. Na Mungu tayari alikuwa amekwishamwambia, “Ni kupitia kwa Isaka kwamba vizazi vyako watakuja.”(A) Lakini Ibrahimu alikuwa tayari kumtoa mwana wake wa pekee. Alifanya hivi kwa sababu alikuwa na imani. 19 Aliamini kwamba Mungu angeweza kuwafufua watu kutoka kifoni. Na hakika, Mungu alipomzuia Ibrahimu katika kumuua Isaka, ilikuwa ni kama vile alimpata tena kutoka kifoni.
20 Isaka akayabariki maisha ya mbeleni ya Yakobo na Esau. Alifanya hivyo kwa sababu alikuwa na imani. 21 Na Yakobo, pia kwa vile alikuwa na imani, alimbariki kila mmoja wa wana wa Yusufu. Alifanya haya wakati alipokuwa akifa, akaiegemea fimbo yake akimwabudu Mungu.
22 Na Yusufu alipokuwa karibu amefariki, alizungumza kuhusu watu wa Israeli kuondoka Misri. Na aliwaambia yale waliyotakiwa kuufanyia mwili wake. Alifanya haya kwa sababu alikuwa na imani.
23 Na mama na baba wa Musa wakaona kwamba alikuwa ni mtoto mzuri hivyo wakamficha kwa miezi mitatu baada ya kuzaliwa kwake. Hili lilikuwa kinyume na agizo la mfalme. Lakini hawakuogopa kwa sababu walikuwa na imani.
24-25 Musa akakua na akawa mwanaume. Akakataa kuitwa mwana wa binti Farao. Akachagua kutokujifurahisha katika raha na dhambi zinazodumu kwa muda mfupi tu. Badala yake, akachagua kuteseka pamoja na watu wa Mungu. Alifanya hivi kwa sababu alikuwa na imani. 26 Alifikiri kuwa ni bora kuteseka kwa ajili ya Masihi kuliko kuwa na hazina zote za Misri. Alikuwa anaisubiri malipo ambayo Mungu angempa.
27 Musa akaondoka Misri kwa sababu alikuwa na imani. Hakuiogopa hasira ya mfalme. Aliendelea kuwa jasiri kama vile angemwona Mungu ambaye hakuna mtu mwingine angeweza kumwona. 28 Na kwa sababu alikuwa na imani, Musa akaandaa mlo wa Pasaka. Na akanyunyiza damu ya mwanakondoo katika miimo ya milango ya watu wake, ili kwamba malaika wa kifo[a] asiwaue wazaliwa wao wa kwanza wa kiume.
© 2017 Bible League International