Revised Common Lectionary (Complementary)
Wayahudi na Sheria
17 Wewe unajiita Myahudi, na unajiona upo salama kwa kuwa tu una sheria. Kwa majivuno unadai kuwa wewe ni mmoja wa wateule wa Mungu. 18 Unajua yale ambayo Mungu anataka ufanye. Na unajua yaliyo muhimu, kwa sababu umejifunza sheria. 19 Unadhani kuwa wewe ni kiongozi wa watu wasioweza kuiona njia sahihi, na nuru kwa wale walio gizani. 20 Unafikiri unaweza kuwaonesha wajinga kilicho sahihi. Na unadhani kuwa wewe ni mwalimu wa wanaoanza kujifunza. Unayo sheria, na hivyo unadhani unajua kila kitu na una kweli yote. 21 Unawafundisha wengine, sasa kwa nini usijifundishe wewe wenyewe? Unawaambia usiibe, lakini wewe mwenyewe unaiba. 22 Unasema wasizini, lakini wewe mwenyewe una hatia ya dhambi hiyo. Unachukia sanamu, lakini unaziiba sanamu katika mahekalu yao. 23 Unajivuna sana kwamba una sheria ya Mungu, lakini unamletea Mungu aibu kwa kuivunja sheria yake. 24 Kama Maandiko yanavyosema, “Watu wa mataifa mengine wanamtukana Mungu kwa sababu yako.”[a]
25 Ikiwa mnaifuata sheria, basi kutahiriwa kwenu kuna maana. Lakini mkiivunja sheria, mnakuwa kama watu ambao hawakutahiriwa. 26 Wale wasiokuwa Wayahudi hawatahiriwi. Lakini wakiifuata sheria inavyosema, wanakuwa kama watu waliotahiriwa. 27 Mnayo sheria na tohara, lakini mnaivunja sheria. Hivyo wale wasiotahiriwa katika miili yao, lakini bado wanaitii sheria, wataonesha kuwa mna hatia.
28 Wewe si Myahudi halisi ikiwa utakuwa Myahudi tu kwa nje. Tohara halisi si ile ya nje ya mwili tu. 29 Myahudi halisi ni yule aliye Myahudi kwa ndani. Tohara halisi inafanywa moyoni. Ni kitu kinachofanywa na Roho, na hakifanyiki ili kufuata sheria iliyoandikwa. Na yeyote aliyetahiriwa moyoni kwa Roho hupata sifa kutoka kwa Mungu, siyo kutoka kwa watu.
© 2017 Bible League International