Revised Common Lectionary (Complementary)
Chakula cha Bwana
17 Siwasifu kwa mambo ninayowaambia sasa. Mikutano yenu inawaumiza kuliko inavyowasaidia. 18 Kwanza, nimesikia kuwa mnapokutana kama kanisa mmegawanyika. Hili si gumu kuliamini 19 kwa sababu ya fikra zenu kwamba imewapasa kuwa na makundi tofauti ili kuonesha ni akina nani walio waamini wa kweli!
20 Mnapokusanyika, hakika hamli chakula cha Bwana.[a] 21 Ninasema hivi kwa sababu mnapokula, kila mmoja anakula na kumaliza chakula chake pasipo kula na wengine. Baadhi ya watu hawapati chakula cha kutosha, ama kinywaji cha kutosha na hivyo kubaki na njaa na kiu, ambapo wengine wanakula na kunywa zaidi hata kulewa.[b] 22 Mnaweza kula na kunywa katika nyumba zenu. Inaonekana kuwa mnadhani kanisa la Mungu si muhimu. Mnawatahayarisha wasio na kitu. Niseme nini? Je, niwasifu? Hapana, siwezi kuwasifu katika hili.
27 Hivyo, ukiula mkate na kukinywea kikombe cha Bwana isivyostahili, unautendea dhambi mwili na damu ya Bwana. 28 Unapaswa kujichunguza mwenendo wako kabla ya kula mkate na kunywa kikombe. 29 Ukila na kunywa bila kuwajali wale ambao ndiyo mwili wa Bwana, kula na kunywa kwako kutasababisha uhukumiwe kuwa mwenye hatia. 30 Ndiyo sababu watu wengi katika kanisa lenu ni wagonjwa na dhaifu, na wengi wameshakufa. 31 Lakini ikiwa tungejichunguza kwa usahihi, Mungu asingetuhukumu. 32 Lakini Bwana anapotuhukumu, anatuadhibu ili kutuonesha njia sahihi. Hufanya hivi ili tusishutumiwe kuwa wakosa na tukahukumiwa pamoja na ulimwengu.
33 Hivyo ndugu zangu, mnapokusanyika pamoja ili mle, subirianeni na mkaribishane kwa moyo wa upendo.
© 2017 Bible League International