Revised Common Lectionary (Complementary)
Kanuni kwa Ajili ya Mikutano Yenu
2 Nawasifu kwa sababu daima mnanikumbuka mimi na kuyafuata mafundisho niliyowapa. 3 Lakini ninataka mwelewe kuwa kichwa cha kila mwanaume ni Kristo. Na Kichwa cha mwanamke ni mwanaume.[a] Na Kichwa cha Kristo ni Mungu.
4 Kila mwanaume anayeomba au kutabiri akiwa amefunika kichwa chake, anakiaibisha kichwa chake. 5 Lakini kila mwanamke anayeomba au kutabiri pasipo kufunika kichwa chake anakiaibisha kichwa chake. Kwa jinsi hiyo anakuwa sawa na mwanamke yule aliyenyoa nywele zake. 6 Ikiwa mwanamke hatafunika kichwa chake, basi na azinyoe nywele zake. Lakini ni aibu kwa mwanamke kukata nywele zake au kuzinyoa kichwani mwake. Hivyo anapaswa kufunika kichwa chake.
7 Lakini mwanaume hapaswi kufunika kichwa chake, kwa sababu ni mfano na utukufu wa Mungu. Lakini mwanamke ni utukufu wa mwanaume. 8 Mwanaume hakutoka kwa mwanamke bali mwanamke ndiye aliyetoka kwa mwanaume. 9 Na mwanaume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke lakini mwanamke ndiye aliumbwa kwa ajili ya mwanaume. 10 Hivyo, kutokana na nilivyosema, mwanamke anapaswa kukitawala kichwa chake kwa kukifunika anapoomba au anapotabiri. Pia, anapaswa kufanya hivi kwa sababu ya malaika.[b]
11 Lakini katika Bwana mwanamke anamhitaji mwanaume, na mwanaume anamhitaji mwanamke. 12 Hii ni kweli kwa sababu mwanamke alitoka kwa mwanaume, lakini pia mwanaume anazaliwa na mwanamke. Hakika, kila kitu kinatoka kwa Mungu.
13 Amueni hili ninyi wenyewe: Je, ni sahihi mwanamke kumwomba Mungu akiwa hajafunika kichwa chake? 14 Je, si hata hali ya asili inatufundisha kuwa ni aibu kwa mwanaume kuwa na nywele ndefu? 15 Lakini kuwa na nywele ndefu ni heshima kwa mwanamke. Mwanamke amepewa nywele ndefu ili kufunika kichwa chake. 16 Baadhi ya watu wanaweza kuanzisha mabishano kuhusiana na yale niliyosema. Lakini desturi ambayo sisi na makanisa ya Mungu yanafuata ni hii: ya kwamba wanawake wanaweza kuomba na kutabiri ujumbe kutoka kwa Mungu, vichwa vyao vikiwa vimefunikwa.
© 2017 Bible League International