Revised Common Lectionary (Complementary)
13 Maandiko yanasema, “Niliamini, hivyo nikasema.”(A) Tuna Roho huyo huyo anayetupa imani kama hiyo. Tunaamini, na hivyo tunasema pia. 14 Mungu alimfufua Bwana Yesu kutoka kwa wafu, nasi tunajua kuwa atatufufua pamoja na Yesu. Mungu atatukusanya pamoja nanyi, na tutasimama mbele zake. 15 Mambo yote haya ni kwa ajili yenu. Na hivyo neema ya Mungu inatolewa kwa watu wengi zaidi na zaidi. Hili litaleta shukrani nyingi zaidi na utukufu kwa Mungu.
Kuishi kwa Imani
16 Hii ndiyo sababu hatukati tamaa. Miili yetu inazidi kuzeeka na kuchoka, lakini roho zetu ndani zinafanywa upya kila siku. 17 Tuna masumbufu, lakini ni madogo na ni ya muda mfupi. Na masumbufu haya yanatusaidia kuupata utukufu wa milele ulio mkuu kuliko masumbufu yetu. 18 Hivyo twafikiri juu ya mambo tusiyoweza kuyaona, si tunayoona. Tunayoyaona ni ya kitambo tu, na yale tusiyoyaona yanadumu milele.
5 Tunafahamu kuwa miili yetu, ambayo ni hema tunaloishi ndani yake hapa duniani itaharibiwa. Hilo litakapotokea, Mungu atakuwa na nyumba tayari kwa ajili yetu kuishi ndani yake. Haitakuwa nyumba kama ambayo watu hujenga hapa duniani. Itakuwa nyumba ya mbinguni itakayodumu milele.
Nguvu ya Yesu Inatoka kwa Mungu
(Mt 12:22-32; Lk 11:14-23; 12:10)
20 Kisha Yesu akaenda nyumbani. Kwa mara nyingine tena umati wa watu ukakusanyika, kiasi kwamba Yesu na wanafunzi wake hawakupata nafasi ya kula. 21 Familia ya Yesu ilipoyasikia haya, walikwenda kumchukua kwa sababu watu walisema amerukwa na akili.
22 Walimu wa Sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu walikuwa wanasema, “Yeye ana Beelzebuli[a] ndani yake! Kwani anafukuza mashetani kwa nguvu ya mkuu wa mashetani!”
23 Yesu akawaita na kuanza kuzungumza nao kwa kulinganisha: “Inawezekanaje Shetani ambaye ni roho mchafu kufukuza mashetani? 24 Ikiwa basi ufalme utagawanyika katika sehemu mbili zinazopingana zenyewe kwa zenyewe, ufalme huo hautaendelea. 25 Vivyo hivyo ufalme wa Shetani ukigawanyika naye akapigana dhidi ya pepo wake wabaya, basi huo utakuwa ndio mwisho wa ufalme wake. Pia ikiwa nyumba itapingana yenyewe kwa yenyewe, nyumba hiyo haitaweza kusalimika. 26 Kwa hiyo ikiwa Shetani atajipinga mwenyewe na kugawanyika basi hataweza kuendelea na huo utakuwa mwisho wake.
27 Hakika, hakuna anayeweza kuingia kwenye nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuzichukua mali zake bila kwanza kumfunga mtu huyo mwenye nguvu; hapo ndipo atakapoweza kuiba katika nyumba hiyo.
28 Ninawaambia ukweli: Watu wanaweza kusamehewa dhambi zao zote na maneno yao yenye matusi kwa Mungu. 29 Lakini yeyote atakayemtukana Roho Mtakatifu hatasamehewa kabisa. Kwa sababu mtu anayefanya hivyo atakuwa na hatia ya dhambi isiyosamehewa milele.”
30 Yesu alisema haya kwa sababu walimu wa sheria walikuwa wanasema, “Yeye ana pepo mchafu ndani yake.”
Wafuasi wa Yesu ni Familia Yake Halisi
(Mt 12:46-50; Lk 8:19-21)
31 Kisha mama yake Yesu na nduguze wakaja. Wao walisimama nje na wakamtuma mtu aende kumwita ndani. 32 Humo lilikuwepo kundi lililoketi kumzunguka, lakini wao wakamwambia, “Tazama! Mama yako, kaka zako na dada zako wako[b] nje wanakusubiri.”
33 Yesu akauliza, “Mama yangu ni nani na kaka zangu ni akina nani?” 34 Yesu akawatazama wale walioketi kumzunguka na akasema “Hapa yupo mama yangu na wapo kaka zangu na dada zangu! 35 Yeyote anayeyafanya mapenzi ya Mungu ndiye kaka yangu, dada yangu, na mama yangu.”
© 2017 Bible League International