Revised Common Lectionary (Complementary)
Barua ya Yesu kwa kanisa la Filadelfia
7 Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia:
Huu ni ujumbe kutoka kwake aliye mtakatifu na wa kweli, anayeshikilia ufunguo wa Daudi. Anapofungua kitu, hakiwezi kufungwa. Na anapofunga kitu hakiwezi kufunguliwa.
8 Ninayajua matendo yako. Nimeweka mbele yako mlango ulio wazi ambao hakuna anayeweza kuufunga. Ninajua wewe ni dhaifu, lakini umeyafuata mafundisho yangu. Hukuogopa kulisema jina langu. 9 Sikiliza! Kuna kundi[a] la Shetani. Wanasema kuwa wao ni Wayahudi, lakini ni waongo. Si Wayahudi halisi. Nitawafanya waje mbele yako na kusujudu kwenye miguu yako. Watajua ya kuwa ninakupenda. 10 Umeifuata amri yangu kwa uvumilivu. Hivyo nitakulinda wakati wa shida itakayokuja ulimwenguni, wakati ambapo kila aishiye duniani atajaribiwa.
11 Naja upesi. Ishikilie imani uliyonayo, ili mtu yeyote asiichukue taji yako. 12 Wale watakaoshinda watakuwa nguzo katika hekalu la Mungu wangu. Hawataliacha hekalu la Mungu tena. Nitaandika juu yao jina la Mungu wangu na jina la mji wa Mungu wangu. Mji huo ni Yerusalemu mpya.[b] Unateremka kutoka mbinguni kwa Mungu wangu. Pia nitaandika jina langu jipya juu yao. 13 Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa.
© 2017 Bible League International