Revised Common Lectionary (Complementary)
Imani
11 Imani inaleta uthabiti wa mambo tunayoyatarajia. Ni uthibitisho wa yale tusiyoweza kuyaona. 2 Mungu alifurahishwa na watu walioishi muda mrefu uliopita kwa sababu walikuwa na imani ya namna hii.
3 Imani hutusaidia sisi kufahamu kwamba Mungu aliumba ulimwengu wote kwa amri yake. Hii inamaanisha kwamba vitu tunavyoviona viliumbwa kwa kitu kisichoonekana.
4 Kaini na Habili wote walitoa sadaka kwa Mungu. Lakini Habili alitoa sadaka bora zaidi kwa Mungu kwa sababu alikuwa na imani. Mungu akasema alifurahishwa na kile alichotoa Habili. Na hivyo Mungu akamwita kuwa mtu mwema kwa sababu alikuwa na imani. Habili akafariki, lakini kupitia imani yake bado anazungumza.
5 Henoko alitwaliwa kutoka duniani, hivyo kamwe yeye hajafariki. Maandiko yanatueleza kwamba kabla ya kuchukuliwa, alikuwa mtu aliyempendeza Mungu. Baadaye, hayupo yeyote aliyejua kule alikokuwa, kwa sababu Mungu alimchukua Henoko ili awe pamoja naye. Haya yote yakatokea kwa vile alikuwa na imani. 6 Bila kuwa na imani hakuna anayeweza kumfurahisha Mungu. Yeyote anayemjia Mungu anatakiwa kuamini kwamba yeye ni hakika na kwamba anawalipa wale ambao kwa uaminifu wanajitahidi kumtafuta.
7 Nuhu alionywa na Mungu juu ya mambo ambayo hakuwa ameyaona bado. Lakini alikuwa na imani na heshima kwa Mungu, hivyo akaijenga meli kubwa ili kuiokoa familia yake. Kwa imani yake, Nuhu alionesha kwamba ulimwengu ulikuwa umekosea. Na akawa ni mmoja wa wale waliohesabiwa haki na Mungu kwa njia ya imani.
© 2017 Bible League International