Revised Common Lectionary (Complementary)
Malaika Amjulisha Zakaria Kuhusu Kuzaliwa kwa Yohana Mbatizaji
5 Herode alipokuwa mfalme wa Uyahudi, alikuwepo kuhani mmoja aliyeitwa Zakaria, aliyekuwa mmoja wa makuhani wa kikundi[a] cha Abiya. Mkewe alikuwa mzaliwa wa ukoo wa Haruni, na jina lake alikuwa Elizabeti. 6 Wote wawili Zakaria na Elizabeti walikuwa wema waliompendeza Mungu na daima walifanya yote yaliyoamriwa na Bwana na kila mara walifuata maagizo yake kwa ukamilifu. 7 Lakini hawakuwa na watoto kwa sababu Elizabeti alikuwa tasa, na wote wawili walikuwa wazee sana.
8 Ilipofika zamu ya kundi la Zakaria kuhudumu Hekaluni, yeye mwenyewe alikuwepo ili kuhudumu kama kuhani mbele za Mungu kwa ajili kundi. 9 Makuhani walikuwa wanapiga kura kumchagua mmoja wao atakayeingia katika Hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba. Na Zakaria alichaguliwa wakati huu. 10 Wakati wa kufukiza uvumba ulipofika watu wote walikusanyika nje ya Hekalu wakiomba.
11 Zakaria akiwa ndani ya Hekalu alitokewa na malaika wa Bwana akiwa amesimama mbele yake upande wa kulia wa madhabahu ya uvumba. 12 Zakaria alipomwona malaika aliogopa, na akaingiwa na hofu. 13 Lakini Malaika akamwambia, “Usiogope, Zakaria. Mungu amelisikia ombi lako. Mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita jina lake Yohana. 14 Utafurahi sana, na watu wengine wengi watamfurahia pamoja nawe. 15 Atakuwa mkuu kwa ajili ya Bwana. Kamwe asinywe mvinyo wala kitu chochote kile kitakachomlewesha. Atajazwa Roho Mtakatifu tangu akiwa tumboni mwa mama yake.
16 Naye atawafanya Waisraeli wengi wamrudie Bwana Mungu wao. 17 Atamtangulia Bwana ili kuwaandaa watu kuupokea ujio wake. Atakuwa na nguvu na roho kama Eliya. Atawapatanisha wazazi na watoto wao na kuwafanya wale wasiomtii Mungu kubadilika na kuanza kumtii Mungu.”
© 2017 Bible League International