Readings for Lent and Easter
Yesu Aomba Akiwa Peke Yake
(Mt 26:36-46; Mk 14:32-42)
39-40 Yesu akaondoka mjini akaenda Mlima wa Mizeituni. Wafuasi wake wakaenda pamoja naye. (Alikuwa akienda huko mara kwa mara.) Akawaambia wafuasi wake, “Ombeni ili mtiwe nguvu msije mkajaribiwa.”
41 Kisha Yesu akaenda kama hatua hamsini mbali nao. Akapiga magoti na akaomba akisema, 42 “Baba, ukiwa radhi, tafadhali usinifanye ninywe katika kikombe[a] hiki. Lakini fanya unalotaka wewe, siyo ninalotaka mimi.” 43 Kisha malaika kutoka mbinguni akaja akamtia nguvu. 44 Yesu aliomba kwa nguvu zaidi na kustahimili zaidi kama mpiganaji wa mieleka akiwa katika mapambano makali. Jasho kama matone ya damu likadondoka kutoka kwenye uso wake.[b] 45 Alipomaliza kuomba, alikwenda kwa wafuasi wake. Akawakuta wamelala, wamechoka kwa sababu ya huzuni. 46 Yesu akawaambia, “Kwa nini mnalala? Amkeni, ombeni mtiwe nguvu msije mkajaribiwa.”
Yesu Akamatwa
(Mt 26:47-56; Mk 14:43-50; Yh 18:3-11)
47 Yesu alipokuwa anaongea, kundi likaja. Lilikuwa linaongozwa na Yuda, mmoja wa mitume kumi na wawili. Akamwendea Yesu ili ambusu.
48 Lakini Yesu akamwambia, “Yuda unatumia busu la urafiki kumsaliti Mwana wa Adamu kwa adui zake?” 49 Wafuasi wa Yesu walikuwa wamesimama pale pia. Walipoona kilichokuwa kinatokea, wakamwambia Yesu, “Bwana, tutumie panga zetu?” 50 Na mmoja wao akautumia upanga wake. Akakata sikio la kulia la mtumishi wa kuhani mkuu.
51 Yesu akasema, “Acha!” Kisha akaligusa sikio la mtumishi na akamponya.
52 Yesu akaliambia lile kundi lililokuja kumkamata. Walikuwa viongozi wa makuhani, viongozi wa wazee wa Kiyahudi na askari walinzi wa Hekalu. Akawaambia, “Kwa nini mmekuja hapa mkiwa na mapanga na marungu? Mnadhani mimi ni mhalifu? 53 Nilikuwa pamoja nanyi kila siku katika eneo la Hekalu. Kwa nini hamkujaribu kunikamata pale? Lakini sasa ni wakati wenu, wakati ambao giza linatawala.”
Petro Amkana Yesu
(Mt 26:57-58,69-75; Mk 14:53-54,66-72; Yh 18:12-18,25-27)
54 Walimkamata Yesu na kumpeleka nyumbani kwa kuhani mkuu. Petro alimfuata Yesu lakini alikaa nyuma kwa mbali. 55 Baadhi ya watu walikoka moto katikati ya ua kisha wakaketi pamoja. Petro naye aliketi pamoja nao. 56 Kutokana na mwanga wa moto, mtumishi wa kike alimwona Petro amekaa pale. Akamtazama Petro usoni kwa makini. Kisha akasema, “Huyu pia alikuwa na yule mtu.”
57 Lakini Petro akasema si kweli. Akasema, “Mwanamke, simfahamu mtu huyo!” 58 Muda mfupi baadaye, mtu mwingine akamwona Petro na akasema, “Wewe pia ni mmoja wa lile kundi!”
Lakini Petro akasema, “Wewe, mimi si mmoja wao!”
59 Baada ya kama saa moja baadaye, mtu mwingine akasema, “Ni kweli, nina uhakika mtu huyu alikuwa pamoja naye, kwa sababu yeye pia anatoka Galilaya.”
60 Lakini Petro akasema, “Wewe, wala sijui unazungumza kuhusu nini!”
Alipokuwa bado anazungumza, jogoo aliwika. 61 Bwana aligeuka akamtazama Petro kwenye macho yake. Kisha Petro akakumbuka Bwana alivyokuwa amesema ya kwamba, “Kabla ya jogoo kuwika asubuhi, utakuwa umenikana mara tatu.” 62 Kisha Petro akatoka nje na kulia kwa uchungu.
© 2017 Bible League International