Old/New Testament
Yesu Awaosha Miguu Wanafunzi Wake
13 Ilikuwa siku moja kabla ya sikukuu ya Pasaka. Yesu alijua ya kuwa wakati wake wa kuondoka duniani na kurudi kwa Baba yake umekaribia. Alikuwa amewapenda sana wafuasi wake hapa duniani, akawapenda hadi mwisho. 2 Na wakati alipokuwa akila chakula cha jioni pamoja na wanafunzi wake, shetani alikuwa amekwisha kumpa Yuda Iskariote, mwana wa Simoni, wazo la kumsaliti Yesu. 3 Yesu akijua ya kwamba Baba yake alikwisha mpa mamlaka juu ya vitu vyote; na kwamba yeye alitoka kwa Mungu na alikuwa anarudi kwa Mungu, 4 alitoka mezani akaweka vazi lake kando, akajifunga taulo kiunoni. 5 Kisha akamimina maji katika chombo akaanza kuwaosha wanafunzi wake miguu na kuikausha kwa ile taulo aliyojifunga kiu noni. 6 Alipomfikia Simoni Petro, Petro akamwambia, “Bwana, wewe unaniosha miguu?” 7 Yesu akamjibu, “Hivi sasa huelewi ninalofa nya lakini baadaye utaelewa.” 8 Petro akamjibu, “La, hutaosha miguu yangu kamwe!” Yesu akamwambia, “Kama sitaosha miguu yako, huwezi kuwa mfuasi wangu.” 9 Ndipo Petro akasema, “Kama ni hivyo Bwana, nioshe miguu yangu pamoja na mikono yangu na kichwa changu pia!” 10 Yesu akamwambia, “Mtu aliyekwishaoga ni safi mwili mzima naye hahitaji tena kunawa ila kuosha miguu tu. Ninyi nyote ni safi, isipokuwa mmoja.” 11 Yesu alifahamu ni nani angemsaliti, ndio sababu akasema, “Ninyi nyote ni safi, isipo kuwa mmoja.”
12 Alipomaliza kuwaosha miguu alivaa tena vazi lake, akarudi alipokuwa amekaa, ndipo akawaambia, “Je, mnaelewa maana ya jambo nililowafanyia? 13 Ninyi mnaniita mimi, Mwalimu na Bwana, na hii ni sawa, kwani ni kweli. 14 Kwa hiyo ikiwa mimi niliye Bwana wenu na Mwalimu wenu nimewaosha miguu, ninyi pia hamna budi kuoshana miguu. 15 Mimi nimewaonyesha mfano, ili mtendeane kama nilivyowafanyia. 16 Ninawaambia hakika, mtumishi hawezi kuwa mkuu kuliko bwana wake; wala anayetumwa hawezi kuwa mkuu kuliko aliyemtuma. 17 Kwa kuwa sasa mnafahamu mambo haya, mtabarikiwa na Mungu ikiwa mtayafanya. 18 Siwazungumzii ninyi nyote. Ninawa fahamu wote niliowachagua. Maandiko yaliyotamka, ‘Yeye aliyekula chakula pamoja nami amekuwa msaliti wangu,’ hayana budi kutimia. 19 Ninawaambia mambo haya kabla hayajatokea ili yatakapotokea mpate kuamini ya kuwa mimi ndiye Kristo. 20 Nawahakikishia kuwa mtu anayemkubali na kumpokea ye yote ninayemtuma, ananipokea mimi. Na mtu anayenikubali na kunipokea, anampokea Baba yangu ambaye amenituma.”
Copyright © 1989 by Biblica