Old/New Testament
Yesu Azungumzia Tena Kifo Chake
30 Wakaondoka mahali hapo, wakapitia Galilaya. Yesu haku taka mtu ye yote afahamu walipokuwa 31 kwa maana alikuwa anawa fundisha wanafunzi wake. Alikuwa akiwaambia, “Mimi Mwana wa Adamu nitasalitiwa mikononi mwa watu ambao wataniua, lakini siku ya tatu baada ya kuuawa, nitafufuka.” 32 Lakini wao hawakuelewa alichokuwa akisema na waliogopa kumwuliza.
Mabishano Kuhusu Aliye Mkuu
33 Basi wakafika Kapernaumu na baada ya kuingia nyumbani akawauliza, “Mlikuwa mnabishana nini njiani?” 34 Lakini hawa kumjibu, kwa sababu njiani walikuwa wakibishana kuhusu nani kati yao alikuwa mkuu zaidi.
35 Akaketi chini, akawaita wote kumi na wawili akawaambia: “Mtu anayetaka kuwa kiongozi hana budi kuwa wa chini kuliko wote na kuwa mtumishi wa wote.” 36 Kisha akamchukua mtoto mdogo akamweka mbele yao, akamkumbatia akawaambia, 37 “Mtu ye yote amkaribishaye mmoja wa hawa watoto wadogo, ananikaribisha mimi. Na ye yote anayenikaribisha mimi anamkaribisha Baba yangu ali yenituma.”
Kutumia Jina La Yesu
38 Yohana akamwambia, “Mwalimu, tumemwona mtu akitoa pepo kwa jina lako tukamzuia kwa sababu yeye si mmoja wetu.” 39 Yesu akasema, “Msimzuie, ye yote atendaye miujiza kwa jina langu kwani hawezi kunigeuka mara moja na kunisema vibaya. 40 Kwa maana ye yote ambaye si adui yetu yuko upande wetu. 41 Ninawahakikishia kwamba mtu atakayewapa japo maji ya kunywa kwa kuwa ninyi ni wafuasi wangu, atapewa tuzo.”
Kuhusu Kuwakwaza Wengine
42 “Na mtu atakayesababisha mmojawapo wa hawa wadogo waniaminio kupoteza imani yake, ingalikuwa nafuu kama mtu huyo angefungiwa jiwe kubwa shingoni akatupwa ziwani. 43 Kama mkono wako ukikusababisha utende dhambi, ukate. Ni afadhali kuingia katika uzima ukiwa na mkono mmoja kuliko kuwa na mikono miwili ukaingia katika moto usiozimika. [ 44 Huko funza hawafi wala moto hauzimiki.] 45 Na kama mguu wako ukikusababisha utende dhambi, ukate. Ni afadhali kuingia katika uzima ukiwa kiwete kuliko kuwa na miguu miwili ukaingia katika moto usiozimika. [ 46 Huko funza hawafi wala moto hauzimiki.] 47 Na kama jicho lako litakusababisha utende dhambi, ling’oe. Ni afadhali kuwa chongo ukaingia katika Ufalme wa Mungu kuliko kuwa na macho mawili ukatupwa Jehena. 48 Huko funza hawafi wala moto hauzimiki. 49 Wote watatiwa chumvi kwa moto. 50 “Chumvi ni nzuri, lakini ikipoteza ladha yake utafanya nini ili iweze kukolea tena? Muwe na chumvi ndani yenu. Muishi pamoja kwa amani.”
Copyright © 1989 by Biblica