Old/New Testament
Yesu Afundisha Kuhusu Talaka
(Mt 19:1-12)
10 Naye aliondoka mahali pale, na kufika katika nchi ya Uyahudi ng'ambo ya Mto Yordani. Na makundi ya watu wakamjia tena na kama alivyofanya daima aliwafundisha.
2 Kisha baadhi ya Mafarisayo walimwendea na kumwuliza “Je, ni sahihi mtu kumtaliki mkewe?” Nao walimwuliza hivyo ili kumjaribu.
3 Yesu akawajibu, “Musa aliwapa amri mfanye nini?”
4 Wakasema, “Musa alimpa ruhusa mume kuandika hati ya kutangua ndoa[a] na kisha kumtaliki mke wake.”
5 Yesu akawaambia, “Musa aliwaandikia amri hii kwa sababu ninyi ni wakaidi na hamkutaka kuyapokea mafundisho ya Mungu. 6 Lakini tangu mwanzo wa uumbaji wake Mungu ‘aliwaumba mwanaume na mwanamke’.(A) 7 ‘Basi kwa sababu ya hiyo mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, na kujiunga na mkewe. 8 Na hao wawili wataungana pamoja na kuwa mwili mmoja.’(B) Nao si wawili tena bali ni mwili mmoja. 9 Kwa hiyo, mtu yeyote asitenganishe kile ambacho Mungu amekiunganisha pamoja.”
10 Walipokuwa ndani ya nyumba ile kwa mara nyingine, wanafunzi wake wakamwuliza Yesu juu ya jambo hili. 11 Naye akawaambia, “yeyote atakayemtaliki mke wake na kuoa mwanamke mwingine, anazini kinyume cha mkewe. 12 Na ikiwa mke atamtaliki[b] mumewe na kuolewa na mume mwingine, basi naye anafanya zinaa.”[c]
Yesu Awakaribisha Watoto
(Mt 19:13-15; Lk 18:15-17)
13 Nao watu wakawaleta watoto wadogo kwa Yesu, ili aweze kuwawekea mikono na kuwabariki. Hata hivyo wanafunzi wake waliwakemea. 14 Yesu alipoona hayo, alikasirika, na akawaambia, “Waruhusuni watoto hao waje kwangu. Msiwazuie, kwa kuwa ufalme wa Mungu ni wa watu kama hao. 15 Ninawaambia kweli, Yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo anavyoupokea hataweza kuingia ndani yake.” 16 Naye Yesu akawakumbatia watoto kifuani mwake na akaweka mikono yake juu yao na kuwabariki.
Mtu Tajiri Akataa Kumfuata Yesu
(Mt 19:16-30; Lk 18:18-30)
17 Na alipokuwa ameanza safari, mtu mmoja alimkimbilia, akafika na kupiga magoti mbele yake, akamwuliza, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?
18 Yesu akamwuliza, kwa nini unaniita mimi mwema? Hakuna aliye mwema isipokuwa Mungu peke yake. 19 Je, unazijua amri: Usiue, usizini, usiibe, usitoe ushahidi wa uongo, usidanganye wengine, uwaheshimu baba na mama yako.”(C)
20 Naye akamwambia Yesu, “Mwalimu, nimeyatii hayo tangu ujana wangu.”
21 Yesu akamwangalia. Naye akashikwa na upendo kwa mtu yule, na hivyo akamwambia, “umekosa kitu kimoja: Nenda ukaviuze vyote ulivyo navyo kisha ukawape walio maskini, nawe utakuwa umejitunzia hazina mbinguni. Kisha uje ukanifuate.”
22 Yule mtu alisikitishwa sana na usemi huo, na akaondoka kwa huzuni kwa kuwa alikuwa na mali nyingi.
23 Yesu aligeuka kuwatazama wanafunzi wake na kuwaambia wake, “Angalieni jinsi ilivyo vigumu sana kwa walio na mali nyingi kuingia katika ufalme wa Mungu.”
24 Wanafunzi wake walistaajabishwa na maneno yale. Lakini Yesu akawaambia tena, “Wanangu, ni vigumu[d] sana kuuingia ufalme wa Mungu. 25 Kwani ni rahisi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuuingia ufalme wa Mungu.”
26 Nao walistajaabu zaidi, na wakaambiana wao kwa wao, “Ni nani basi atakayeweza kuokolewa?”
27 Huku akiwatazama, Yesu alisema, “Hili haliwezekani kwa wanadamu, lakini kwa Mungu linawezekana, kwa sababu yote yanawezekana kwake Mungu.”
28 Petro akaanza kumwambia, “Tazama! Tumeacha kila kitu tukakufuata.”
29 Yesu akasema, “Nawaambieni kweli: Hakuna aliyeacha nyumba, kaka, dada, mama, baba, watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili 30 ambaye hatapata malipo mara mia zaidi katika nyakati hizi; nyumba, kaka, dada, mama, watoto, na mashamba, pamoja na mateso; na uzima wa milele katika kizazi kinachokuja. 31 Lakini wengi walio wa kwanza sasa watakuwa wa mwisho baadaye na wale walio wa mwisho sasa watakuwa wa kwanza baadaye.”
© 2017 Bible League International