Read the New Testament in 24 Weeks
Wapende Watu Wote
2 Kaka zangu na dada zangu, ninyi ni wenye imani katika Bwana wetu mtukufu Yesu Kristo. Kwa hiyo msiwachukulie baadhi ya watu kuwa wa maana zaidi kuliko wengine. 2 Tuchukulie mtu mmoja anakuja katika mkutano wenu akiwa amevaa pete ya dhahabu ama akiwa amevaa mavazi ya thamani, na mtu maskini aliyevaa mavazi yaliyochakaa na machafu naye akaja ndani. 3 Na tuchukulie kuwa mnaonyesha kumjali zaidi yule mtu aliyevaa mavazi mazuri na kusema, “Wewe keti hapa katika kiti hiki kizuri.” Lakini unamwambia yule mtu maskini, “Wewe simama pale,” au, “Keti chini karibu na miguu yetu.” 4 Je, hiyo haioneshi kwamba mnafikiri miongoni mwenu kuwa baadhi ya watu ni bora kuliko wengine? Mmesimama kama mahakimu wenye maamuzi mabaya?
5 Sikilizeni kaka na dada zangu wapendwa! Mungu aliwachagua wale walio maskini machoni pa watu kuwa matajiri katika imani. Aliwachagua kuwa warithi wa Ufalme, ambao Mungu aliwaahidi wale wanaompenda? 6 Lakini ninyi mmewadhalilisha walio maskini! Na kwa nini mnawapa heshima kubwa watu walio matajiri? Hawa ndiyo wale ambao daima wanajaribu kuyadhibiti maisha yenu. Si ndiyo hao wanaowapeleka ninyi mahakamani? 7 Je, si ndiyo hao hao wanaolitukana Jina zuri la Bwana wenu?[a]
8 Kama kweli mnaitunza sheria ya ufalme inayopatikana katika Maandiko, “Mpende jirani yako[b] kama unavyojipenda mwenyewe,”(A) mtakuwa mnafanya vizuri. 9 Lakini kama mtakuwa mnaonyesha upendeleo, mtakuwa mnafanya dhambi na mtahukumiwa kuwa na hatia kama wavunja sheria.
10 Ninasema hivi kwa sababu yeyote anayeitunza Sheria yote, lakini akaikosea hata mmoja tu atakuwa na hatia ya kuihalifu Sheria yote. 11 Kwa sababu yeye aliyesema, “Usizini,”(B) pia ndiye aliyesema, “Usiue.”(C) Hivyo, kama hutazini lakini ukaua utakuwa umevunja Sheria yote ya Mungu.
12 Mseme na kutenda kama watu watakaokuja kuhukumiwa kwa sheria inayoleta uhuru. 13 Kwa kuwa hukumu ya Mungu haitakuwa na huruma kwake yeye ambaye hakuwa na rehema. Lakini rehema huishinda hukumu!
Imani na Kazi Njema
14 Ndugu zangu, ikiwa mtu atasema kuwa anayo imani lakini hafanyi kitu, imani hiyo haina manufaa yoyote. Imani ya jinsi hiyo haiwezi kumwokoa mtu yeyote. 15 Kama ndugu au dada anahitaji mavazi na anapungukiwa chakula cha kila siku, 16 na ukawaambia, “Mungu awe nanyi! Mkahifadhiwe mahala pa joto na mle vizuri!” Hiyo ina manufaa gani kwao? Usipowapa vitu wanavyovihitaji, maneno yako yanakosa maana! 17 Kwa jinsi hiyo hiyo, imani isipokuwa na matendo itakuwa imekufa.
18 Lakini mtu anaweza kuleta hoja kusema, “Watu wengine wanayo imani, na wengine wanayo matendo mema.” Jibu langu litakuwa, huwezi kunionyesha imani yako pasipo kufanya tendo lolote. Lakini mimi nitakuonesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu. 19 Je, mnaamini kwamba kuna Mungu mmoja tu? Vema! Hata mapepo yanaamini na kutetemeka kwa hofu.
20 Wewe mjinga! Je, unahitaji uthibitisho kwamba imani bila matendo haina manufaa? 21 Je, si baba yetu Ibrahimu alihesabiwa haki na Mungu kwa matendo yake alipomtoa sadaka mwanae Isaka juu ya madhabahu? 22 Kwa hakika unaweza kuiona imani hiyo ilifanya kazi pamoja na matendo yake. Kwa hiyo imani yake ilikamilishwa na matendo yake. 23 Ndipo yakatimizwa yale yaliyo kwenye Maandiko kuwa, “Ibrahimu alimwamini Mungu, na kwa imani hiyo akafanywa kuwa mwenye haki[c] kwa Mungu,”(D) na kwa sababu hiyo akaitwa “Rafiki wa Mungu”.(E) 24 Mnamwona mtu huyo amefanywa kuwa mwenye haki kwa Mungu kwa matendo yake wala siyo kwa imani peke yake.
25 Je, Rahabu[d] yule kahaba si alifanywa kuwa mwenye haki na Mungu kwa matendo aliyofanya, alipowasaidia wale waliokuwa wakipeleleza nchi kwa niaba ya watu wa Mungu. Aliwakaribisha nyumbani mwake na kuwawezesha kutoroka kwa njia nyingine.
26 Hivyo, kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo, imani imekufa ikiwa haina matendo.
Kuyamudu Mambo Tunayosema
3 Kaka na dada zangu, msiwe walimu wengi miongoni mwenu. Mnajua kuwa sisi tulio walimu tutahukumiwa zaidi tena kwa umakini kweli.
2 Ninawatahadharisha kwa sababu sote tunakosa mara kwa mara. Na kama kuna mtu asiyekosa kwa maneno yake, huyo ni mkamilifu, huyo anaweza kuumudu mwili wake wote. 3 Tunawaweka lijamu katika midomo ya farasi, ili waweze kututii sisi. Kwa lijamu hizo tunaweza kuidhibiti miili yao. 4 Au tuchukue meli kama mfano: Hata kama ni kubwa mno na husukumwa na upepo mkali, zinaongozwa kwa usukani mdogo sana na kwenda po pote alikokusudia nahodha kuipeleka. 5 Kwa jinsi hiyo hiyo, ulimi ni kiungo kidogo sana katika mwili, lakini unaweza kujivuna kuwa umetenda mambo makubwa sana.
Fikiri jinsi ambavyo msitu mkubwa unaweza kuwashwa moto kwa mwali mdogo tu! 6 Ndiyo, ulimi ni mwali wa moto. Ulimi unawakilisha ulimwengu wa uovu miongoni mwa viungo vya mwili wetu. Ulimi huo huo huuchafua mwili wote, na unaweza kuwasha moto maisha yote ya mtu. Nao unapata moto wake kutoka Jehanamu.
7 Aina zote za wanyama na ndege, mijusi na viumbe vya baharini wanaweza kufugwa na wanadamu wamekuwa wanawafuga. 8 Lakini hakuna mtu aliyefaulu kuufuga ulimi. Ni uovu usiotulia na umejaa sumu ya kuua. 9 Kwa ulimi huo tunambariki Bwana na Baba, na kwa huo huo tunawalaani watu walioumbwa kwa mfano wa Mungu! 10 Kutoka katika kinywa hicho hicho hutoka baraka na laana. Kaka na dada zangu, haipaswi kuwa hivyo. 11 Chemichemi ya maji haiwezi kutoa maji matamu na maji machungu kutoka katika tundu moja, je inawezekana? 12 Ndugu zangu, je mtini unaweza kuzaa zeituni? Au mzabibu waweza kuzaa tini? Kwa hakika haiwezekani! Wala chemichemi ya maji chumvi haiwezi kutoa maji matamu.
Hekima ya Kweli
13 Nani miongoni mwenu aliye na hekima na ufahamu? Na aoneshe hekima yake kwa mwenendo mzuri, kwa matendo yake yanayofanywa kwa unyenyekevu unaoletwa na hekima. 14 Lakini kama mtakuwa na wivu wenye uchungu na ubinafsi ndani ya mioyo yenu, hamwezi kujivunia hekima yenu; kwamba kujivuna kwenu kungekuwa ni uongo unaoficha ukweli. 15 Hii sio aina ya hekima inayotoka juu mbinguni, bali ni ya kidunia, isiyotoka kwa Roho wa Mungu bali ni ya kishetani. 16 Kwa sababu pale penye wivu na ubinafsi, basi panakuwepo vurugu na kila aina ya matendo maovu. 17 Lakini hekima inayotoka mbinguni juu kwanza juu ya yote ni safi, kisha ni ya amani ina upole na ina busara. Imejaa rehema na huzaa mavuno ya matendo mema. Haina upendeleo wala unafiki. 18 Wale wenye bidii ya kuleta amani na wanaopanda mbegu zao kwa matendo ya amani, watavuna haki kama mavuno yao.
© 2017 Bible League International