Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Read the New Testament in 24 Weeks

A reading plan that walks through the entire New Testament in 24 weeks of daily readings.
Duration: 168 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Ufunuo 19-20

Watu Wamsifu Mungu Mbinguni

19 Baada ya hili nikasikia kitu kilichosikika kama kundi kubwa la watu mbinguni. Walikuwa wakisema:

“Haleluya![a]
Ushindi, utukufu na nguvu ni vyake Mungu wetu.
    Hukumu zake ni za kweli na za haki.
Mungu wetu amemwadhibu kahaba.
    Ndiye aliyeiharibu dunia kwa uzinzi wake.
Mungu amemwadhibu kahaba kulipa kisasi cha vifo vya watumishi wake.”

Pia, watu hawa walisema:

“Haleluya!
    Anaungua na moshi wake utasimama milele na milele.”

Ndipo wazee ishirini na nne na viumbe wenye uhai wanne wakaanguka chini kusujudu wakamwabudu Mungu, akaaye kwenye kiti cha enzi. Wakasema:

“Amina! Haleluya!”

Sauti ikatoka kwenye kiti cha enzi na kusema:

“Msifuni Mungu wetu,
    ninyi nyote mnaomtumikia!
Msifuni Mungu wetu,
    ninyi nyote mlio wadogo na wakubwa mnaomheshimu!”

Kisha nikasikia kitu kilichosikika kama kundi kubwa la watu. Kilikuwa na kelele kama mawimbi ya bahari au radi. Watu walikuwa wakisema:

“Haleluya!
    Bwana Mungu wetu anatawala.
    Ndiye Mwenye Nguvu, Mungu Mwenyezi.
Tushangilie na kufurahi na
    kumpa Mungu utukufu!
Mpeni Mungu utukufu, kwa sababu arusi ya Mwanakondoo imewadia.
    Na bibi arusi wa Mwanakondoo amekwisha jiandaa.
Nguo ya kitani safi ilitolewa kwa bibi arusi ili avae.
    Kitani ilikuwa safi na angavu.”

(Kitani safi inamaanisha mambo mazuri ambayo watakatifu wa Mungu waliyatenda.)

Kisha malaika akaniambia, “Andika hili: Heri ni kwa wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwanakondoo!” Kisha malaika akasema, “Haya ni maneno ya Mungu mwenyewe.”

10 Kisha nikaanguka chini mbele miguuni pa malaika ili nimwabudu. Lakini malaika akaniambia, “Usiniabudu! Mimi ni mtumishi kama wewe na ndugu zako na dada zako walio na ushuhuda kuhusu Yesu Kristo. Hivyo mwabudu Mungu! Kwa sababu ushuhuda kuhusu Yesu ndiyo roho ya unabii.”

Mpanda Farasi Juu ya Farasi Mweupe

11 Kisha nikaona mbingu zimefunguka, na nikamwona farasi mweupe. Mpanda farasi aliitwa Mwaminifu na Kweli, kwa sababu ni wa haki katika maamuzi yake na kufanya vita. 12 Macho yake yalikuwa kama mwali wa moto. Alikuwa na taji nyingi kichwani mwake. Jina lilikuwa limeandikwa juu yake, lakini yeye peke yake ndiye aliyejua maana ya jina hilo. 13 Alivaa vazi lililochovywa katika damu, na aliitwa Neno la Mungu. 14 Majeshi ya mbinguni yalikuwa yanamfuata mpanda farasi mweupe. Walikuwa wanaendesha farasi weupe pia. Walikuwa wamevaa kitani nzuri, nyeupe na safi. 15 Upanga mkali ulikuwa unatoka kwenye kinywa chake, upanga ambao angeutumia kuyashinda mataifa. Na atayatawala mataifa kwa fimbo ya chuma. Atazikanyaga zabibu katika shinikizo la ghadhabu ya Mungu Mwenye Nguvu. 16 Kwenye vazi lake na kwenye mguu wake alikuwa ameandikwa jina lake:

mfalme wa wafalme na bwana wa mabwana.

17 Kisha nikaona malaika amesimama katika jua. Kwa sauti kuu malaika akawaambia ndege wote wanaoruka angani, “Kusanyikeni kwa ajili ya karamu kuu ya Mungu. 18 Kusanyikeni mle miili ya watawala, majemadari na watu maarufu. Njooni mle miili ya farasi na wanaowapanda na miili ya watu wote, walio huru na watumwa, wadogo na wakubwa.”

19 Kisha nikamwona mnyama na watawala wa dunia. Majeshi yao yalikusanyika pamoja ili kufanya vita kupigana na mpanda farasi mweupe na jeshi lake. 20 Lakini mnyama na nabii wa uongo walikamatwa. Nabii wa uongo ndiye aliyefanya miujiza[b] kwa ajili ya mnyama. Alitumia miujiza hii kuwahadaa wale waliokuwa na alama ya mnyama na walioabudu sanamu yake. Nabii wa uongo na mnyama walitupwa kwenye ziwa la moto linalowaka kwa baruti. 21 Majeshi yao yaliuawa kwa upanga uliotoka kwenye kinywa cha mpanda farasi. Ndege wote walikula miili hii mpaka wakashiba.

Miaka Elfu Moja

20 Nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni. Malaika alikuwa na ufunguo wa kuzimu na mnyororo mkubwa mkononi mwake. Malaika alimkamata joka, nyoka wa zamani ambaye pia anajulikana kama Ibilisi au Shetani. Malaika akamfunga joka kwa minyororo kwa muda wa miaka elfu moja. Kisha akamtupia kuzimu na akaifunga. Malaika akamfungia joka kuzimu ili asiweze kuwadanganya watu wa dunia mpaka miaka elfu moja iishe. Baada ya miaka elfu moja joka lazima aachiwe huru kwa muda mfupi.

Kisha nikaona viti vya enzi na watu wamevikalia. Hawa ni wale waliopewa mamlaka ya kuhukumu. Na nikaona roho za wale waliouawa kwa sababu walikuwa waaminifu kwa kweli ya Yesu na ujumbe kutoka kwa Mungu. Hawakumwabudu mnyama wala sanamu yake. Hawakuipokea alama ya mnyama kwenye vipaji vya nyuso zao au mkononi mwao. Walifufuka na kutawala na Kristo kwa miaka elfu moja. (Wengine waliokufa hawakufufuka mpaka miaka elfu moja ilipokwisha.)

Huu ni ufufuo wa kwanza. Heri walifufuliwa mara ya kwanza. Ni watakatifu wa Mungu. Mauti ya pili haina nguvu juu yao. Watakuwa makuhani wa Mungu na Kristo. Watatawala pamoja naye kwa miaka elfu moja.

Kushindwa kwa Shetani

Miaka elfu moja itakapokwisha, Shetani ataachiwa huru kutoka kwenye gereza lake. Atatoka na kwenda kuwadanganya mataifa katika dunia yote, mataifa yajulikanayo kama Gogu na Magogu. Shetani atawakusanya watu kwa ajili ya vita. Kutakuwa watu wengi wasiohesabika kama mchanga katika ufukwe wa bahari.

Nililiona jeshi la Shetani likitembea na kujikusanya ili kuizingira kambi ya watu wa Mungu na mji anaoupenda Mungu. Lakini moto ukashuka kutoka mbinguni na kuliteketeza jeshi la Shetani. 10 Na Shetani, yule aliyewadanganya watu hawa, alitupwa kwenye ziwa la moto pamoja na mnyama na nabii wa uongo. Watateseka kwa maumivu usiku na mchana milele na milele.

Watu wa Dunia Wahukumiwa

11 Kisha nikaona kiti cha enzi kikubwa cheupe. Nikamwona aliyekuwa amekaa kwenye kiti cha enzi. Dunia na anga vikamkimbia na kutoweka. 12 Na nikaona wale waliokufa, wakubwa na wadogo, wamesimama mbele ya kiti cha enzi na vitabu vilifunguliwa. Na kitabu cha uzima kilifunguliwa pia. Watu walihukumiwa kwa yale waliyotenda, kama yalivyoandikwa katika vitabu.

13 Bahari ikawaachia wafu waliokuwa ndani yake. Mauti na kuzimu zikawaachia wafu waliokuwa ndani yake. Watu wote hawa walihukumiwa kutokana na matendo yao. 14 Mauti na kuzimu vilitupwa kwenye ziwa la moto. Ziwa hili la moto ni mauti ya pili. 15 Na yeyote ambaye jina lake halikuonekana limeandikwa kwenye kitabu cha uzima alitupwa kwenye ziwa la moto.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International