Read the New Testament in 24 Weeks
Yohana Aonya juu ya Walimu wa Uongo
4 Rafiki zangu wapenzi, manabii wengi wa uongo wapo duniani sasa. Hivyo msiiamini kila roho, lakini zijaribuni hizo roho ili muone kama zinatoka kwa Mungu. 2 Hivi ndivyo mwezavyo kuitambua Roho ya Mungu. Roho inayosema, “Naamini kuwa Yesu ni Masihi aliye kuja duniani na akafanyika mwanadamu.” Roho hiyo inatoka kwa Mungu. 3 Roho inayokataa kutamka hayo juu ya Yesu, hii ni roho iliyo adui kwa Kristo. Mmesikia kuwa adui wa kristo anakuja, na sasa amekwishakuja naye yupo tayari ulimwenguni.
4 Wanangu wapenzi, ninyi ni wa Mungu, hivyo mmeshawashinda tayari hawa manabii wa uongo. Hii ni kwa sababu yule aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliyeko duniani. 5 Wao ni wa ulimwengu. Hivyo kile wanachokisema ni cha ulimwengu pia. Na ulimwengu husikia kile wanachokisema. 6 Lakini sisi tunatokana na Mungu. Kwa hiyo watu wanaomjua Mungu hutusikia sisi. Lakini watu wasiotokana na Mungu hawatusikii sisi. Hivi ndivyo tunavyiojua Roho iliyo ya kweli na ile iliyo ya uongo.
Upendo Hutoka kwa Mungu
7 Wapenzi rafiki, tunatakiwa tupendane sisi kwa sisi, kwa sababu upendo watoka kwa Mungu. Yeyote apendae amefanyika mwana wa Mungu. Na kila apendae anamfahamu Mungu. 8 Kila asiyependa hamfahamu Mungu, kwa sababu Mungu ni Pendo. 9 Hivi ndivyo Mungu alivyo tuonyesha pendo lake sisi: Alimtuma mwanawe wa pekee ulimwenguni kutupatia sisi uzima katika yeye. 10 Upendo wa kweli ni upendo wa Mungu kwa ajili yetu, si upendo wetu kwa Mungu. Alimtuma mwanawe kama njia ya kuziondoa dhambi zetu.
11 Hivyo ndivyo Mungu atupendavyo, rafiki wapenzi! Kwa hiyo tupendane sisi kwa sisi. 12 Hakuna aliyemwona Mungu. Ila tukipendana sisi kwa sisi, Mungu anaishi ndani yetu. Kama tukipendana sisi kwa sisi, Upendo wa Mungu unafikia shabaha yake na unafanywa kamili ndani yetu.
13 Twatambua kuwa tunaishi katika Mungu na mungu ndani yetu. Twalitambua hilo kwa sababu ametupa Roho wake. 14 Tumeona kuwa Baba alimtuma mwanaye aje kuwa Mwokozi wa ulimwengu, na hili ndilo tunalowaambia watu sasa. 15 Yeyote anayesema, “Naamini kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu,” huyo ni mtu anayeishi ndani ya Mungu, na Mungu anaishi ndani ya mtu huyo. 16 Hivyo twalifahamu pendo alilonalo Mungu kwetu, na tunalitumainia pendo hilo.
Mungu ni pendo. Kila anae ishi katika pendo anaishi ndani ya Mungu, na Mungu ndani yao. 17 Kama pendo la Mungu limekamilishwa ndani yetu, tunaweza kuwa bila hofu siku ambayo Mungu atahukumu ulimwengu. Hatutakuwa na hofu, kwa sababu katika ulimwengu huu tunaishi kama Yesu.[a] 18 Palipo na upendo wa Mungu, hakuna hofu, kwa sababu upendo wa Mungu ulio kamili unaondoa hofu. Ni hukumu yake ndiyo inayomfanya mtu kuwa na hofu. Hivyo pendo lake halikamilishwi kwa mtu ambaye ndani yake kuna hofu.
19 Tunapenda kwa sababu Mungu alitupenda sisi kwanza. 20 Kama tukisema kuwa tunampenda Mungu na tunamchukia mmojawapo wa kaka na dada zetu katika familia ya Mungu, basi sisi tu waongo. Kama hatuwezi kumpenda mtu tunayemwona, tutawezaje kumpenda Mungu, ambaye hata hatujamwona. 21 Mungu ametupa amri hii: Kama tunampenda Mungu, Ni lazima pia tupendane sisi kwa sisi kama kina kaka na kina dada.
Watoto wa Mungu Ushindeni Ulimwengu
5 Watu wanao amini kuwa Yesu ni Masihi ni wana wa Mungu. Na kila ampendae Baba pia anawapenda watoto wa Baba. 2 Twatambuaje kuwa tunawapenda watoto wa Mungu? Twatambua kwa sababu tunampenda Mungu na tunazitii amri zake. 3 Kumpenda Mungu ni kuzitii amri zake. Na amri za Mungu si ngumu kwetu, 4 kwa sababu kila ambae ni mwana wa Mungu ana uwezo wa kushinda dhidi ya ulimwengu. Ni imani yetu iliyoshinda vita dhidi ya ulimwengu. 5 Hivyo ni nani anayeushinda ulimwengu? Ni wale tu wanaoamini kuwa Yesu ni mwana wa Mungu.
Mungu alituambia kwa Habari ya Mwanae
6 Yesu Kristo ndiye aliyekuja. Alikuja kwa maji na damu.[b] Hakuja kwa maji peke yake. Lahasha, Yesu alikuja kwa vyote maji na damu. Na Roho atuambia kuwa hili ni kweli. Roho ndiye Kweli. 7 Kwa hiyo kuna mashahidi watatu wanao tuambia habari za Yesu: 8 Roho, Maji, na Damu. Mashuhuda hawa watatu wanakubaliana.
9 Tunawaamini watu wanaposema jambo llililo kweli. Lakini kile anachosema Mungu ni muhimu zaidi. Na Hivi ndivyo Mungu alivyotuambia: Alituambia ukweli kuhusu Mwanaye. 10 Kila amwaminiye Mwana wa Mungu anayo kweli ambayo Mungu alituambia. Lakini watu wasiomwamini Mungu wanamfanya Mungu kuwa mwongo, kwa sababu hawaamini kile ambacho Mungu ametueleza kuhusu mwanaye. 11 Hiki ndicho ambacho Mungu alitueleza: Mungu ametupatia uzima wa milele, na uzima huu umo katika wanawake. 12 Yeyote aliye na mwana anao uzima wa milele, lakini asiye na mwana wa mungu hana huo uzima wa milele.
Tunao uzima wa Milele Sasa
13 Ninawaandikia barua hii ninyi mnaomwamini Mwana wa Mungu ili mjue ya kwamba sasa mnao uzima wa milele. 14 Tunaweza kwenda kwa Mungu tukiwa na ujasiri huo. Hii ina maana kuwa tunapomwomba Mungu mambo (na mambo hayo yakakubaliana na matakwa yake kwetu), Mungu huyajali yale tunayosema. 15 Hutusikiliza kila wakati tunapomwomba. Hivyo tunatambua kuwa yeye hutupa kila tunachomwomba.
16 Utakapomwona muumini mwenzio akitenda dhambi (Dhambi isiyomwongoza kwenye mauti), unapaswa kumwombea. Kisha Mungu atampa uzima. Ipo aina ya dhambi inayomwongoza mtu hadi mauti ya milele. Sina maana ya kusema unapaswa kuombea aina hiyo ya dhambi. 17 Daima kutenda yasiyo haki ni dhambi. Lakini ipo dhambi isiyomwongoza mtu katika mauti ya milele.
18 Tunajua kwamba wale waliofanyika watoto wa Mungu hawaendelei kutenda dhambi. Mwana wa Mungu anawahifadhi salama.[c] Yule Mwovu hawezi kuwagusa. 19 Tunajua kwamba sisi ni wa Mungu, Lakini yule Mwovu anautawala ulimwengu wote. 20 Nasi tunajua kwamba Mwana wa Mungu amekuja na ametupa uelewa. Hivyo sasa tunaweza kumjua yeye aliye kweli, na tunaishi katika Mungu huyo wa kweli. Nasi tumo ndani ya mwanaye, Yesu Kristo. Yeye ndiye Mungu wa kweli, naye ndiye uzima wa milele. 21 Kwa hiyo, watoto wapendwa, mjiepushe na miungu wa uongo.
© 2017 Bible League International