Read the New Testament in 24 Weeks
1 Salamu kutoka kwa Paulo, mtume wa Kristo Yesu.[a] Ni mtume kwa sababu ndivyo Mungu alivyotaka. Yeye alinituma kwa sababu Mungu alipenda niwaeleze watu juu ya ahadi ya uzima ulio katika Kristo Yesu.
2 Kwa Timotheo, mwanangu mpendwa:
Neema, rehema na amani iwe kwako kutoka kwa Mungu Baba na Kristo Yesu Bwana wetu.
Shukrani na Kutia Moyo
3 Daima namshukuru Mungu katika maombi yangu ninapokukumbuka usiku na mchana kwa ajili yako. Ni Mungu wa mababu zangu na daima nimemtumikia kwa dhamiri safi. 4 Nikiyakumbuka machozi yako kwa ajili yangu, ninatamani kukuona, ili niweze kujazwa na furaha. 5 Nimekumbuka imani yako ya kweli ambayo mwanzoni ilikuwa kwa bibi yako Loisi na kwa mama yako Eunike. Nami nashawishika hiyo iko kwako. 6 Kwa sababu hii ninakukumbusha karama ya Mungu ambayo uliipokea wakati nilipokuwekea mikono. Sasa nataka uitumie karama hiyo na ikue zaidi na zaidi kama mwali wa moto mdogo uwakavyo ndani ya moto. 7 Kwani Roho ambaye Mungu alitupa sisi ni chanzo cha ujasiri wetu, ni nguvu, upendo na fikra safi.
8 Hivyo usione aibu kushuhudia juu ya Bwana wetu Yesu au kunionea aibu mimi, niliye mfungwa kwa ajili yake. Bali aliteseka pamoja nami kwa ajili ya Habari Njema na Mungu hutupa nguvu.
9 Alituokoa na kutuita katika maisha ya utakatifu, sio kwa sababu ya kitu cho chote tulichokifanya wenyewe, bali kwa kusudi lake mwenyewe na neema, ambayo ametupa sisi kwa Kristo Yesu kabla ya mwanzo wa wakati, 10 na ambayo sasa imeonyeshwa kwetu kwa kuja kwake Kristo Yesu, Mwokozi wetu. Yeye Kristo aliiharibu mauti na kuleta uzima na kutokufa kwenye nuru kwa njia ya Habari Njema.
11 Niliteuliwa na Mungu kutangaza Habari Njema kama mtume na mwalimu. 12 Na ni kwa kazi hii ninateseka lakini sioni haya kwa sababu namjua yeye niliyemwekea imani yangu, na nina uhakika kuwa anaweza kukilinda kile nilichokikabidhi kwake hadi Siku ile.
13 Yale uliyoyasikia nikiyafundisha yawe mfano kwako wa mafundisho utakayofundisha wewe. Uyafuate na yawe kielelezo cha mafundisho ya kweli na uzima kwa uaminifu na upendo ule ule ambao Kristo Yesu ametuonesha. 14 Kwa msaada wa Roho Mtakatifu anayeishi ndani yako, uyalinde mafundisho haya ya mazuri na yenye thamani mliyopewa dhamana kwayo.
15 Unajua kwamba kila mtu aliyeko Asia ameniacha. Hata Figelo na Hermogene nao wameniacha. 16 Ninaomba kwamba Bwana ataonesha rehema wa familia ya Onesiforo, amekuwa faraja yangu mara nyingi, na hakuona haya kwa ajili yangu kuwa gerezani. 17 Kinyume chake, alipofika Rumi, alinitafuta kwa bidii hadi aliponiona. 18 Bwana Yesu na amjalie kupata rehema kutoka kwa Bwana Mungu katika siku ile ya hukumu ya mwisho! Unafahamu vema ni kwa njia ngapi alinihudumia wakati nilipokuwa Efeso.
Askari Mwaminifu wa Kristo Yesu
2 Kwako wewe mwanangu, uwe hodari kwa njia ya neema inayopatikana kwa Kristo Yesu. 2 Yachukue mambo uliyoyasikia kwangu mbele za mashahidi wengi, na yakabidhi kwa watu waaminifu ambao watakuwa na uwezo wa kuwafundisha wengine pia. 3 Kama askari mwaminifu wa Kristo Yesu, jiunge nami katika mateso. 4 Hakuna hata mmoja anayefanya kazi kama askari kisha akajishughulisha pia na mambo ya kiraia. Hii ni wa sababu anataka kumfurahisha kamanda wake. 5 Na kama kuna mtu anayeshiriki katika mashindano ya riadha, hawezi kushinda taji endapo hatashindana kwa kufuata sheria. 6 Mkulima mwenye juhudi anastahili kuwa wa kwanza kufurahia sehemu ya mavuno yake. 7 Nakutaka wewe kuyafikiri ninayokuambia na Bwana atakupa uwezo wa kuyaelewa mambo haya yote.
8 Endelea kumkumbuka Yesu Kristo, aliyefufuka kutoka kwa wafu, na ni kutoka ukoo wa Daudi. Na huu ndiyo Habari Njema ninayoihubiri. 9 Kwa sababu ya Habari Njema ninateseka, hadi hatua ya kufungwa kwa minyororo kama mhalifu. Lakini ujumbe wa Mungu haujafungwa. 10 Kwa hiyo nayavumilia yote kwa ajili ya wateule wa Mungu, ili na wao waweze kuufikia wokovu unaopatikana katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele.
11 Na hapa kuna usemi wa kuaminiwa:
Kama tumekufa pamoja naye,
tutaweza kuishi naye pia.
12 Kama tutastahimili, tutaweza pia kumiliki pamoja naye.
Kama tutamkana yeye, naye atatukana sisi.
13 Kama hatutakuwa waaminifu,
yeye anabaki kuwa mwaminifu,
kwa sababu hawezi kujikana mwenyewe.
Mtendakazi Ampendezaye Mungu
14 Endelea kuwakumbusha watu juu ya mambo haya. Waonye kwa mamlaka mbele za Mungu wasipigane juu ya maneno. Mapigano hayo hayana mambo mazuri, bali huwaharibu wanaoyasikiliza. 15 Jitahidi kujionesha mwenyewe kuwa umekubaliwa na Mungu, kama mtumishi asiye na kitu cho chote cha kumfadhaisha na anayeufanyia kazi ujumbe wa kweli ya Mungu katika njia sahihi.
16 Bali uyaepuke majadiliano ya kijinga ya kidunia, ambayo huwapeleka watu mbali na Mungu, 17 na mafundisho ya wale wanaoyachukua mafundisho hayo wanaenea kama saratani mwilini. Miongoni mwao wamo Himenayo na Fileto, 18 aliyeiasi na kuikosa kweli. Wanasema kuwa ufufuo kutoka kwa wafu kwa watu wote umekwisha kutokea, na wanageuza imani za watu wengine.
19 Hata hivyo, msingi ulio imara ambao Mungu aliuweka unasimama imara, na maneno haya yameandikwa juu yake: “Bwana anawajua wale walio wake,”(A) na “Kila anayesema kuwa ni wa Bwana aweze kuuacha ubaya.”
20 Ndani ya nyumba kubwa hakuna vyombo vya dhahabu na fedha pekee, bali hata vya udongo na mbao. Na vingine ni vya kutumika kwa matukio maalumu, na vingine ni kwa matumizi ya kawaida. 21 Hivyo mtu akitakaswa kutoka maovu yote, atakuwa mtakatifu na chombo maalumu cha kutumiwa na Bwana kilicho tayari kwa kila kazi njema.
22 Bali uzikimbie tamaa za ujana na kuyatafuta maisha ya haki, imani, upendo na amani, pamoja na wote wanaomwita Bwana kwa mioyo safi. 23 Nyakati zote ujiepushe na mabishano ya kijinga, kwa sababu unajua kuwa huleta mabishano makubwa. 24 Kwani mtumwa wa Bwana hapaswi kubishana, bali kuwa mkarimu kwa watu wote, mwenye ujuzi katika kufundisha na asiye mtukanaji. 25 Anapaswa kuwaelekeza wapinzani wake kwa upole katika tumaini kwamba Mungu anaweza kuwasaidia hao kutubu na kuujua ukweli, 26 na ili waweze kurudi katika fahamu zao na kuuepuka mtego wa adui, ambako wameshikiliwa kama mateka na Ibilisi na wamelazimishwa kuyafanya mapenzi yake.
© 2017 Bible League International