Read the New Testament in 24 Weeks
Viongozi katika Kanisa
3 Usemi huu ni wa kweli kwamba yeyote mwenye nia ya kuhudumu kama mzee,[a] anatamani kazi njema. 2 Mzee[b] lazima awe mtu mwema asiyelaumiwa na mtu yeyote. Anapaswa kuwa mwaminifu kwa mke wake.[c] Anapaswa kuwa na kiasi, mwenye busara na mwenye mwenendo mzuri katika maisha, anayeheshimiwa na watu wengine, aliye tayari kuwasaidia watu kwa kuwakaribisha katika nyumba yake. Ni lazima awe mwalimu mzuri. 3 Askofu asizoee kunywa mvinyo wala kuwa mgomvi. Bali awe mpole na mtu wa amani, na asiyependa fedha. 4 Ni lazima awe kiongozi mzuri kwa familia yake mwenyewe. Hii ina maana kwamba watoto wake wanamtii kwa heshima zote. 5 Ikiwa mtu hawezi kuiongoza familia yake mwenyewe, hawezi kulitunza Kanisa la Mungu.
6 Ni lazima askofu asiwe yule aliyeamini hivi karibuni. Hii inaweza kumfanya awe na kiburi. Kisha anaweza akahukumiwa kwa kiburi chake kama vile Shetani alivyopanga. 7 Pia, ni lazima askofu aheshimiwe na watu walio nje ya Kanisa. Kwa namna hiyo hataweza kukosolewa na kuabishwa na wengine na kunasa kwenye mtego wa Shetani.
Mashemasi
8 Kwa njia hiyo hiyo, watu wanaoteuliwa kuwa mashemasi inawapasa kuwa wale wanaostahili kuheshimiwa. Wasiwe watu wanaosema mambo wasiokuwa nayo moyoni au wanaotumia muda wao mwingi katika ulevi. Wasiwe watu wanaowaibia fedha watu wengine kwa udanganyifu. 9 Ni lazima waifuate imani ya kweli ambayo Mungu ameiweka wazi kwetu na sikuzote wawe watu wanaotenda mambo yaliyo sahihi. 10 Hao unapaswa kuwapima kwanza. Kisha, ukigundua kuwa hawawezi kushitakiwa jambo lolote baya walilotenda, basi wanaweza kuwa mashemasi.
11 Kwa njia hiyo hiyo wanawake wanaoteuliwa kuwa mashemasi wanapaswa kuwa wale wanaoastahili kuheshimiwa. Wasiwe wanawake wanaosema mambo mabaya juu ya watu wengine. Ni lazima wawe na kiasi. Ni lazima wawe wanawake wanaoweza kuaminiwa kwa kila jambo.
12 Wanaume walio mashemasi lazima wawe waaminifu katika ndoa. Ni lazima wawe viongozi wema wa watoto na familia zao binafsi. 13 Mashemasi wanaofanya kazi yao vyema wanajitengenezea nafasi nzuri ya kuheshimiwa. Nao kwa kiasi kikubwa sana wanajihakikishia imani yao katika Kristo Yesu.
Siri ya Maisha Yetu
14 Ninatarajia kuja kwenu hivi karibuni. Lakini ninakuandikia maneno haya sasa, 15 ili kwamba, hata kama sitakuja mapema, utafahamu jinsi ambavyo watu wanapaswa kuishi katika familia[d] ya Mungu. Familia hiyo ni kanisa la Mungu aliye hai. Na Kanisa la Mungu ni msaada na msingi wa ukweli. 16 Ndiyo, Mungu ametuonesha siri ya maisha yanayompa heshima na kumpendeza Yeye. Siri hii ya ajabu ni ukweli ambao wote tunakubaliana nao:
Kristo[e] alijulikana kwetu katika umbile la kibinadamu;
alioneshwa na Roho[f] kuwa kama alivyojitambulisha;
alionwa na malaika.
Ujumbe kuhusu Yeye ulitangazwa kwa mataifa;
watu ulimwenguni walimwamini;
alichukuliwa juu mbinguni katika utukufu.
Maonyo juu ya Walimu wa uongo
4 Roho anasema wazi wazi kwamba katika siku za mwisho wengine watajitenga na imani. Watazitii roho zinazodanganya, na kufuata mafundisho ya mashetani. 2 Mafundisho hayo yanafundishwa na watu wanaodanganya na kuwafanyia hila wengine. Watu hawa waovu hawapambanui kati ya mema na maovu. Ni kana kwamba dhamiri zao zimeharibiwa kwa chuma cha moto. 3 Wanasema ni vibaya kuoa. Na wanasema kwamba kuna baadhi ya vyakula ambavyo watu lazima wasile. Lakini Mungu aliumba vyakula hivi, na wale wanaoamini na kuelewa ukweli wanaweza kuvila kwa shukrani. 4 Kila kitu alichokiumba Mungu ni chema, hakuna chakula kitakachokataliwa kama kikikubaliwa kwa shukrani. 5 Kila kitu alichokiumba kiliumbwa kitakatifu kwa namna alivyosema na kwa maombi.
Uwe Mtumishi Mwema wa Kristo Yesu
6 Waambie haya kaka na dada huko. Hii itakuonesha wewe kuwa ni mtumishi mwema wa Kristo Yesu. Utaonyesha kwamba umefundishwa maneno ya imani na mafundisho mazuri uliyoyafuata. 7 Usitumie muda wowote katika masimulizi ya kipuuzi ambayo hayakubaliani na ukweli wa Mungu. Badala yake jizoeshe mwenyewe kuishi maisha ya kumheshimu na kumpendeza Mungu. 8 Kufanya mazoezi ya mwili wako kuna manufaa kidogo kwako. Lakini kujaribu kumpendeza Mungu kwa njia zote kunakufaa zaidi. Kunakuletea baraka katika maisha haya na maisha ya baadaye pia. 9 Huu ni usemi wa kweli ambao unaweza kukukubaliwa bila kuuliza swali: 10 Tunayo matumaini kwa Mungu aliye hai, Mwokozi wa watu wote. Ambaye hasa, ni Mwokozi wa wale wote wanaomuamini. Na hii ndiyo sababu tunafanya kazi na kupambana.
11 Amuru na kufundisha mambo haya. 12 Wewe ni kijana, lakini usiruhusu yeyote kukufanya wewe kama si mtu muhimu. Uwe mfano kuonesha waamini namna wanavyoweza kuishi. Waoneshe kwa namna unavyosema, unavyoishi, unavyopenda, unavyo amini, na namna ya maisha yako safi.
13 Endelea kusoma Maandiko kwa watu, watie moyo, na uwafundishe. Fanya hivyo mpaka nitakapo kuja. 14 Kumbuka kutumia kipawa ulichonacho, ambacho ulipewa kupitia unabii wakati kundi la wazee lilipo kuweka mikono juu yako. 15 Endelea kufanya haya, na jitoe maisha yako kutenda hayo. Kisha kila mtu anaweza kuona namna ilivyo vema unavyotenda. 16 Uwe mwangalifu katika maisha na mafundisho yako. Endelea kuishi na kufundisha kwa usahihi. Kisha, utajiokoa mwenyewe na wale wanaosikiliza mafundisho yako.
© 2017 Bible League International