Read the New Testament in 24 Weeks
1 Salamu kutoka kwa Paulo, mtume wa Kristo Yesu.[a] Mimi ni mtume kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Kristo Yesu atupaye tumaini.
2 Ninakuandikia wewe, Timotheo. Wewe ni kama mwanangu halisi kwa sababu ya imani yetu.
Neema, rehema na amani kutoka kwa Mungu Baba na Kristo Yesu Bwana wetu ziwe pamoja nawe.
Maonyo kuhusu Mafundisho ya Uongo
3 Nilipokwenda Makedonia, nilikuomba ubaki Efeso. Baadhi ya watu huko wanafundisha mambo yasiyo ya kweli, nami ninataka uwaonye waache. 4 Uwaambie wasitumie muda wao kusimulia simulizi zisizo na maana za mambo ya kale na kutengeneza orodha ndefu ya mababu. Mambo hayo husababisha mabishano tu na hayaisaidii katika kuikamilisha kazi ya Mungu tuliyopewa, ambayo ni lazima tuikamilishe kwa imani. 5 Kusudi langu la kukueleza ufanye jambo hili ni kutaka kukuza upendo; aina ya upendo unaooneshwa na wale ambao mawazo yao ni safi; watu ambao hufanya yale wanayojua kuwa ni sahihi na ambao imani yao kwa Mungu ni ya kweli. 6 Lakini wengine wamekosa jambo hili la msingi katika mafundisho yao na wamepoteza mwelekeo. Sasa wanazungumza juu ya mambo yasiyo na msaada kwa mtu yeyote. 7 Wanataka kuwa walimu wa sheria,[b] lakini hawafahamu mambo wanayosema, wanasema kwa ujasiri wote juu ya mambo wasiyoyaelewa wenyewe.
8 Tunajua kwamba sheria ni nzuri ikiwa mtu anaitumia kwa usahihi. 9 Pia tunajua kwamba sheria haikutengenezwa kwa ajili ya wale wanaotenda haki. Imetengenezwa kwa ajili ya wale wanayoipinga na kukataa kuifuata. Sheria ipo kwa ajili ya wenye dhambi wanaompinga Mungu na mambo yote yanayompendeza. Ipo kwa ajili ya wale wasio na hamu ya mambo ya kiroho na kwa ajili ya wale wanaowaua baba au mama zao au mtu yeyote yule. 10 Ipo kwa ajili ya watu wanaotenda dhambi ya uasherati, kwa wanaume wanaolala na wanaume wenzao au wavulana, kwa wote wanaoteka watu na kuwauza kama watumwa, kwa wote wanaodanganya au wale wasiosema ukweli wakiwa katika kiapo, na kwa ajili ya wale walio kinyume na mafundisho ya kweli ya Mungu. 11 Mafundisho hayo ni sehemu ya Habari Njema ambayo Mungu wetu wa utukufu alinipa kuhubiri na ndani yake tunauona utukufu wake.
Shukrani kwa Rehema za Mungu
12 Ninamshukuru Kristo Yesu Bwana wetu kwa sababu aliniamini na kunipa kazi hii ya kumtumikia. Yeye hunitia nguvu ya kufanya kazi hii. 13 Hapo zamani nilimtukana Kristo. Nikiwa mtu mwenye majivuno na mkorofi, niliwatesa watu wake. Lakini Mungu alinihurumia kwa sababu sikujua nilichokuwa nafanya. Nilifanya hayo kabla sijaamini. 14 Lakini Bwana wetu alinipa kiwango kikubwa cha neema yake. Na pamoja na neema hiyo imani na upendo ulio katika Kristo Yesu vilifuata.
15 Huu ndiyo usemi wa kweli unaopaswa kukubaliwa pasipo kuuliza maswali; kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuokoa wenye dhambi, nami ni mbaya zaidi ya wote. 16 Lakini nilipata rehema kwa sababu ili Kristo Yesu aweze kunitumia, mimi mtenda dhambi kuliko wote, ili kuonesha uvumilivu wake usio na kikomo. Alitaka niwe mfano kwa wale ambao wangemwamini na kupata uzima wa milele. 17 Heshima na utukufu kwa mfalme anayetawala milele. Hawezi kuharibiwa wala kuonekana. Heshima na utukufu apewe Mungu wa pekee milele na milele, Amina.
18 Timotheo wewe ni mwanangu mwenyewe kwa sababu ya ushirika wetu wa imani ya kweli. Ninayokuambia kuyatenda yanakubaliana na unabii[c] ambao ulisemwa juu yako hapo zamani. Nataka uukumbuke unabii huo na kupigana vita vizuri vya imani. 19 Endelea kumwamini Mungu na kutenda yale unayojua kuwa ni sahihi. Watu wengine hawajatenda haya, na imani yao sasa imeharibiwa. 20 Himenayo na Iskanda ni mfano wa watu hao. Nimewakabidhi kwa Shetani ili wafundishwe kutosema kinyume cha Mungu.
Mungu Anataka Tumwombee Kila Mtu
2 Kwanza kabisa, ninakuagiza uwaombee watu wote. Uwaombee kwa Mungu ili awabariki na kuwapa mahitaji yao. Kisha umshukuru Yeye. 2 Unapaswa kuwaombea watawala na wote wenye mamlaka. Uwaombee viongozi hawa ili tuweze kuishi maisha yenye utulivu na amani, maisha yaliyojaa utukufu kwa Mungu na yanayostahili heshima. 3 Hili ni jambo jema na linampendeza Mungu Mwokozi wetu.
4 Mungu anataka kila mtu aokolewe na aielewe kweli kikamilifu. 5 Kuna Mungu mmoja tu, na kuna mwanadamu mmoja tu anayeweza kuwaleta pamoja wanadamu wote na Mungu wao. Huyo mtu ni Kristo Yesu kama mwanadamu. 6 Alijitoa mwenyewe kulipa deni ili kila mtu awe huru. Huu ni ujumbe ambao Mungu alitupa wakati unofaa. 7 Nami nilichaguliwa kama mtume kuwaambia watu ujumbe huo. Ninasema kweli. Sidanganyi. Nilichaguliwa kuwafundisha wasio Wayahudi na nimefanya kazi hii kwa imani na ukweli.
Maagizo Maalumu kwa Wanawake na Wanaume
8 Nataka wanaume walio kila mahali waombe. Ni lazima wawe watu wanaoishi kwa kumpendeza Mungu na wanaonyoosha mikono yao wanapoomba na wawe watu wasio na hasira na wanaopenda mabishano.
9 Na ninawataka wanawake wajipambe kwa namna inayofaa. Mavazi yao yawe yanayofaa na yanayostahili. Hawapaswi kuvutia watu kwa kutengeneza nywele zao kwa mitindo ya ajabu ama kwa kuvaa dhahabu, vito au lulu au nguo za gharama. 10 Lakini wajipambe na kuvutia kwa matendo mema wanayofanya. Hayo ndiyo yanayofaa zaidi kwa wanawake wanaosema kuwa wamejitoa kwa ajili ya Mungu.
11 Mwanamke anapaswa kujifunza akisikiliza kwa utulivu huku akiwa radhi kutii kwa moyo wake wote. 12 Simruhusu mwanamke kumfundisha mwanaume au kumwelekeza jambo la kufanya. Bali lazima asikilize kwa utulivu, 13 kwa sababu Adamu aliumbwa kwanza na Hawa akaumbwa baadaye. 14 Na Adamu hakudanganywa.[d] Bali mwanamke ndiye aliyedanganywa naye akatenda dhambi. 15 Lakini wanawake wataokolewa kwa jukumu lao la kuzaa watoto.[e] Wakiendelea kuishi katika imani, upendo, utakatifu na tabia njema.
© 2017 Bible League International