Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Read the New Testament in 24 Weeks

A reading plan that walks through the entire New Testament in 24 weeks of daily readings.
Duration: 168 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Wafilipi 3-4

Yesu Kristo ni wa Muhimu Zaidi

Kwa hiyo sasa, kaka na dada zangu, furahini kwa kuwa ninyi ni wa Bwana. Sisiti kuwaandikia mambo haya haya, kwa sababu yatawasaidia ninyi kuwa imara na salama.

Mjihadhari na mbwa, mjihadhari na wafanyakazi waovu, mjihadhari na watu wanaotaka kumkata kila mtu ambaye hajatahiriwa.[a] Lakini sisi ndiyo wenye tohara[b] ya kweli, tunaomwabudu Mungu kupitia Roho wake. Hatutumaini katika namna tulivyo kwa kuzaliwa au kwa yale tuliyoyakamilisha. Tunajivuna kuwa sisi ni milki ya Kristo Yesu. Hata kama ninaweza kujitumainisha mimi mwenyewe, bado sifanyi hivyo. Ikiwa kuna watu wanadhani wana sababu za kutumaini sifa za kibinadamu, wanapaswa kujua kuwa nina sababu zaidi za kufanya hivyo. Nilitahiriwa siku ya nane baada ya kuzaliwa. Mimi ni Myahudi wa kabila la Benjamini. Mimi ni Mwebrania halisi, hata wazazi wangu pia. Nikawa Farisayo na nilitii torati kwa uangalifu sana. Nilikuwa na hamu sana ya kumridhisha Mungu[c] hata nikalitesa kanisa. Kwa usahihi niliitii sheria ya Musa.

Wakati fulani mambo haya yote yalikuwa muhimu kwangu. Lakini kwa sababu ya Kristo, sasa ninayachukulia mambo haya yote kuwa yasiyo na thamani. Na si haya tu, lakini sasa ninaelewa kuwa kila kitu ni hasara tu ukilinganisha na thamani kuu zaidi ya kumjua Kristo Yesu, ambaye sasa ni Bwana wangu. Kwa ajili yake nilipoteza kila kitu. Na ninayachukulia yote kama kinyesi, ili nimpate Kristo. Ninataka niwe wake. Katika Kristo ninayo haki mbele za Mungu, lakini kuwa na haki mbele za Mungu hakuji kwa kuitii sheria, Bali inakuja toka kwa Mungu kupitia imani kwa[d] Kristo. Mungu anatumia imani yangu kwa Kristo kunihesabia haki. 10 Ninachotaka ni kumjua Kristo na nguvu iliyomfufua kutoka kwa wafu. Ninataka kushiriki katika mateso yake na kuwa kama yeye hata katika kifo chake. 11 Kisha mimi mwenyewe naweza kuwa na matumaini kwamba nitafufuliwa kutoka kwa wafu.

Kuyafikia Malengo

12 Sisemi kuwa nimekwisha kupata ujuzi huo au kuifikia shabaha ya mwisho. Lakini bado ninajitahidi kuifikia shabaha kwa kuwa ndivyo ambavyo Kristo Yesu anataka nifanye. Ndiyo sababu alinifanya kuwa wake. 13 Kaka na dada zangu, ninajua ya kuwa bado nina safari ndefu. Lakini kuna kitu kimoja ninachofanya, nacho ni kusahau yaliyopita na kujitahidi kwa kadri ninavyoweza kuyafikia malengo yaliyo mbele yangu. 14 Ninaendelea kupiga mbio kuelekea mwisho wa mashindano ili niweze kushinda tuzo ambayo Mungu ameniitia kutoka mbinguni kwa njia ya Kristo Yesu.

15 Sisi sote tuliokua kiroho tunapaswa kufikiri namna hii. Na ikiwa kuna jambo lolote ambalo hamkubaliani nalo, Mungu atalifunua kwenu. 16 Lakini tunapaswa kuendelea kuifuata kweli tuliyonayo tayari.

17 Kaka na dada zangu, unganeni pamoja na mfuate mfano wangu. Mtazame na mjifunze pia kutoka kwa wale wanaoishi katika namna tuliyoionesha kwenu. 18 Wapo wengi ambao mwenendo wao unaonesha kuwa ni adui za msalaba wa Kristo. Nimekwishawaambia kuhusu hao mara nyingi. Na inanifanya nitokwe machozi ninapowaambia kuhusu watu hao sasa. 19 Wanauendea uharibifu kwa namna wanavyoishi. Wanaabudu tamaa za mili yao kana kwamba hizo ndizo Mungu. Wanatenda mambo ya aibu na wanajivuna kwa kutenda mambo hayo. Wanayawazia mambo ya kidunia tu. 20 Lakini sisi tunatawaliwa na serikali iliyoko mbinguni. Tunamsubiri Mwokozi wetu, Bwana wetu Yesu Kristo atakayekuja kutoka mbinguni. 21 Ataibadilisha miili yetu minyenyekevu na kuifanya iwe kama mwili wake yeye mwenyewe, mwili wenye utukufu. Kristo atafanya hivi kwa nguvu yake inayomwezesha kutawala juu ya vyote.

Maagizo ya Mwisho

Kaka na dada zangu wapenzi, ninawapenda na ninataka kuwaona. Mnanifurahisha na ninajivuna kwa sababu yenu. Endeleeni kuwa imara kumfuata Bwana kama nilivyowaambia.

Ninawasihi Euodia na Sintike, ninyi nyote wawili ni wa Bwana, hivyo muwe na mtazamo mmoja. Kwa ajili ya hili ninamwomba rafiki yangu aliyetumika pamoja nami kwa uaminifu: Wasaidieni wanawake hawa. Waliwahubiri watu Habari Njema kwa bidii kama watendaji wenzangu tukiwa pamoja na Klementi na wengine waliofanya kazi pamoja nami. Majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima.[e]

Furahini katika Bwana daima. Ninasema tena, furahini.

Kila mtu auone wema na uvumilivu wenu. Bwana yu karibu kuja. Msisumbuke kitu chochote, lakini salini na kumwomba Mungu kwa mahitaji yenu. Mshukuruni Mungu wakati mnapomwomba yale mnayohitaji. Na kwa kuwa ninyi ni milki ya Kristo Yesu, amani ya Mungu itailinda mioyo na mawazo yenu isipate wasiwasi. Amani yake inaweza kutenda haya zaidi ya akili za kibinadamu.[f]

Na sasa, mwisho kabisa, kaka na dada zangu, fikirini kuhusu yale yaliyo ya kweli, ya kuheshimiwa, ya haki, yaliyo safi, yenye kupendeza, na yanayosemwa vema. Yatendeni yale mliyojifunza na kupokea kutoka kwangu, niliyowaambia na yale mliyoyaona nikitenda. Na Mungu atoaye amani atakuwa pamoja nanyi.

Paulo Apokea Zawadi Kwa Furaha

10 Nimefurahi sana katika Bwana kwa sababu mmeonesha tena kuwa mnanijali. Mmeendelea kujali juu yangu, lakini haikuwepo njia ya kuonesha hili. 11 Ninawaambia hili, si kwa sababu ninahitaji msaada kutoka kwa yeyote. Nimejifunza kuridhika na kile nilichonacho na chochote kinachotokea. 12 Ninajua namna ya kuishi ninapokuwa na vichache na ninapokuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuishi katika hali zote, ninapokuwa na vyakula vingi au ninapokuwa na njaa, ninapokuwa na vingi zaidi ya ninavyohitaji au ninapokuwa sina kitu. 13 Kristo ndiye anayenitia nguvu kuyakabili mazingira yote katika maisha.

14 Lakini mlifanya vyema mliposhiriki nami katika kipindi changu kigumu. 15 Enyi watu wa Filipi kumbukeni nilipokuja mara ya kwanza kuwahubiri Habari Njema watu wa Makedonia. Nilipoondoka huko, ninyi ndiyo kanisa pekee ambalo lilishirikiana nami katika uhusiano ulioendelea wa kutoa na kupokea. 16 Ukweli ni kuwa hata nilipokuwa Thesalonike, zaidi ya mara moja mlinitumia kila kitu nilichohitaji. 17 Si kwamba natafuta msaada wa kifedha kutoka kwenu. Bali ninataka ninyi mpokee manufaa yanayozidi kukua yanayotokana na kutoa. 18 Nina kila kitu ninachohitaji. Nina zaidi ya hata ninavyohitaji kwa sababu Epafrodito ameniletea kila kitu mlichompa aniletee. Zawadi zenu ni kama sadaka yenye harufu nzuri inayotolewa kwa Mungu. Ni sadaka anayoikubali, na inampendeza. 19 Mungu wangu atatumia utajiri wake wenye utukufu kuwapa ninyi kila kitu mnachohitaji kupitia Kristo Yesu. 20 Utukufu kwa Mungu na Baba yetu milele na milele. Amina.

21 Wasalimuni watakatifu wote wa Mungu walio wake Kristo Yesu. Wale walio katika familia ya Mungu walio pamoja nami wanawasalimu. 22 Na watu wote wa Mungu walio hapa wanawasalimu, hasa wale walio katika utumishi wa Kaisari.

23 Neema ya Bwana Yesu Kristo iwe pamoja na utu wenu wa ndani.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International