Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Read the New Testament in 24 Weeks

A reading plan that walks through the entire New Testament in 24 weeks of daily readings.
Duration: 168 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
1 Wakorintho 11-12

11 Fuateni mfano wangu, kama ninavyoufuata mfano wa Kristo.

Kanuni kwa Ajili ya Mikutano Yenu

Nawasifu kwa sababu daima mnanikumbuka mimi na kuyafuata mafundisho niliyowapa. Lakini ninataka mwelewe kuwa kichwa cha kila mwanaume ni Kristo. Na Kichwa cha mwanamke ni mwanaume.[a] Na Kichwa cha Kristo ni Mungu.

Kila mwanaume anayeomba au kutabiri akiwa amefunika kichwa chake, anakiaibisha kichwa chake. Lakini kila mwanamke anayeomba au kutabiri pasipo kufunika kichwa chake anakiaibisha kichwa chake. Kwa jinsi hiyo anakuwa sawa na mwanamke yule aliyenyoa nywele zake. Ikiwa mwanamke hatafunika kichwa chake, basi na azinyoe nywele zake. Lakini ni aibu kwa mwanamke kukata nywele zake au kuzinyoa kichwani mwake. Hivyo anapaswa kufunika kichwa chake.

Lakini mwanaume hapaswi kufunika kichwa chake, kwa sababu ni mfano na utukufu wa Mungu. Lakini mwanamke ni utukufu wa mwanaume. Mwanaume hakutoka kwa mwanamke bali mwanamke ndiye aliyetoka kwa mwanaume. Na mwanaume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke lakini mwanamke ndiye aliumbwa kwa ajili ya mwanaume. 10 Hivyo, kutokana na nilivyosema, mwanamke anapaswa kukitawala kichwa chake kwa kukifunika anapoomba au anapotabiri. Pia, anapaswa kufanya hivi kwa sababu ya malaika.[b]

11 Lakini katika Bwana mwanamke anamhitaji mwanaume, na mwanaume anamhitaji mwanamke. 12 Hii ni kweli kwa sababu mwanamke alitoka kwa mwanaume, lakini pia mwanaume anazaliwa na mwanamke. Hakika, kila kitu kinatoka kwa Mungu.

13 Amueni hili ninyi wenyewe: Je, ni sahihi mwanamke kumwomba Mungu akiwa hajafunika kichwa chake? 14 Je, si hata hali ya asili inatufundisha kuwa ni aibu kwa mwanaume kuwa na nywele ndefu? 15 Lakini kuwa na nywele ndefu ni heshima kwa mwanamke. Mwanamke amepewa nywele ndefu ili kufunika kichwa chake. 16 Baadhi ya watu wanaweza kuanzisha mabishano kuhusiana na yale niliyosema. Lakini desturi ambayo sisi na makanisa ya Mungu yanafuata ni hii: ya kwamba wanawake wanaweza kuomba na kutabiri ujumbe kutoka kwa Mungu, vichwa vyao vikiwa vimefunikwa.

Chakula cha Bwana

17 Siwasifu kwa mambo ninayowaambia sasa. Mikutano yenu inawaumiza kuliko inavyowasaidia. 18 Kwanza, nimesikia kuwa mnapokutana kama kanisa mmegawanyika. Hili si gumu kuliamini 19 kwa sababu ya fikra zenu kwamba imewapasa kuwa na makundi tofauti ili kuonesha ni akina nani walio waamini wa kweli!

20 Mnapokusanyika, hakika hamli chakula cha Bwana.[c] 21 Ninasema hivi kwa sababu mnapokula, kila mmoja anakula na kumaliza chakula chake pasipo kula na wengine. Baadhi ya watu hawapati chakula cha kutosha, ama kinywaji cha kutosha na hivyo kubaki na njaa na kiu, ambapo wengine wanakula na kunywa zaidi hata kulewa.[d] 22 Mnaweza kula na kunywa katika nyumba zenu. Inaonekana kuwa mnadhani kanisa la Mungu si muhimu. Mnawatahayarisha wasio na kitu. Niseme nini? Je, niwasifu? Hapana, siwezi kuwasifu katika hili.

23 Mafundisho niliyowafundisha ni yale yale niliyopokea kutoka kwa Bwana, ya kwamba usiku ule ambao Bwana Yesu alikamatwa, aliuchukua mkate 24 na akashukuru. Kisha akaumega na kusema, “Huu ni mwili wangu; ni kwa ajili yenu. Uleni mkate huu kwa ajili ya kunikumbuka mimi.” 25 Kwa namna hiyo hiyo, baada ya wote kula, Yesu alichukua kikombe cha divai na akasema, “Divai hii inawakilisha agano jipya ambalo Mungu anafanya na watu wake, linaloanza kwa sadaka ya damu yangu. Kila mnywapo divai hii, fanyeni hivi kwa ajili ya kunikumbuka mimi.” 26 Hii inamaanisha kuwa kila mnapokula mkate huu na kunywa kikombe hiki, mnawaambia wengine kuhusu kifo cha Bwana mpaka atakaporudi.

27 Hivyo, ukiula mkate na kukinywea kikombe cha Bwana isivyostahili, unautendea dhambi mwili na damu ya Bwana. 28 Unapaswa kujichunguza mwenendo wako kabla ya kula mkate na kunywa kikombe. 29 Ukila na kunywa bila kuwajali wale ambao ndiyo mwili wa Bwana, kula na kunywa kwako kutasababisha uhukumiwe kuwa mwenye hatia. 30 Ndiyo sababu watu wengi katika kanisa lenu ni wagonjwa na dhaifu, na wengi wameshakufa. 31 Lakini ikiwa tungejichunguza kwa usahihi, Mungu asingetuhukumu. 32 Lakini Bwana anapotuhukumu, anatuadhibu ili kutuonesha njia sahihi. Hufanya hivi ili tusishutumiwe kuwa wakosa na tukahukumiwa pamoja na ulimwengu.

33 Hivyo ndugu zangu, mnapokusanyika pamoja ili mle, subirianeni na mkaribishane kwa moyo wa upendo. 34 Ikiwa mtu yeyote anawaza kuhusu njaa yake mwenyewe, basi akae nyumbani kwake na ale huko! Fanyeni hivi ili kukutanika kwenu kusilete hukumu ya Mungu juu yenu. Nitakapokuja nitawaambia nini cha kufanya kuhusu masuala mengine.

Karama Kutoka kwa Roho Mtakatifu

12 Na sasa ninataka mwelewe kuhusu karama za Roho Mtakatifu. Mnayakumbuka maisha mliyoishi kabla hamjawa waamini. Mlipotoshwa na kuongozwa kuziabudu sanamu, ambazo hata kuzungumza haziwezi. Hivyo ninawaambia ya kwamba hakuna mtu anayezungumza kwa Roho wa Mungu anayeweza kusema, “Yesu alaaniwe.” Na hakuna anayeweza kusema “Yesu ni Bwana,” bila msaada wa Roho Mtakatifu.

Kuna karama mbalimbali za Roho, lakini zote zinatoka kwa Roho yule yule. Kuna namna mbalimbali za kutumika, lakini sote tunatumika kwa niaba ya Bwana yule yule. Na kuna namna ambazo Mungu hufanya kazi ndani yetu sote, lakini ni Mungu yule yule anayetenda kazi ndani yetu ili tutende kila kitu.

Kitu fulani kutoka kwa Roho kinaweza kuonekana ndani ya kila mtu. Roho humpa kila mtu hili ili awasaidie wengine. Roho humpa mtu fulani uwezo wa kuzungumza kwa hekima. Na Roho huyo huyo humpa mwingine uwezo wa kuzungumza kwa maarifa. Roho huyo huyo humpa mtu karama ya imani na humpa mwingine karama ya kuponya. 10 Roho humpa mtu nguvu ya kutenda miujiza, na humpa mwingine uwezo wa kutabiri, na mwingine uwezo wa kupambanua kujua kilichotoka kwa Roho na ambacho hakikutoka kwa Roho. Roho humpa mtu fulani uwezo wa kusema kwa lugha zingine tofauti, na humpa mwingine uwezo wa kufasiri lugha hizo. 11 Roho mmoja, Roho yule yule hufanya mambo yote haya. Roho ndiye huamua ampe nini kila mtu.

Mwili wa Kristo

12 Mtu ana mwili mmoja, lakini una viungo vingi. Kuna viungo vingi, lakini viungo vyote hivyo ni mwili mmoja. Kristo yuko vivyo hivyo pia. 13 Baadhi yetu ni Wayahudi na baadhi yetu si Wayahudi; baadhi yetu ni watumwa na baadhi yetu ni watu tulio huru. Lakini sisi sote tulibatizwa ili tuwe sehemu ya mwili mmoja kwa njia ya Roho mmoja. Nasi tulipewa[e] Roho mmoja.

14 Na mwili wa mtu una viungo zaidi ya kimoja. Una viungo vingi. 15 Mguu unaweza kusema, “Mimi si mkono, na hivyo mimi si wa mwili.” Lakini kusema hivi hakutafanya mguu usiwe kiungo cha mwili. 16 Sikio linaweza kusema, “Mimi si jicho, hivyo mimi si wa mwili.” Lakini kwa kusema hivi hakutafanya sikio lisiwe kiungo cha mwili. 17 Ikiwa mwili wote ungekuwa jicho, usingeweza kusikia. Ikiwa mwili wote ungekuwa sikio, usingeweza kunusa kitu chochote. 18-19 Ikiwa viungo vyote vya mwili vingekuwa kiungo kimoja, mwili usingekuwepo. Kama jinsi ilivyo, Mungu aliweka viungo katika mwili kama alivyotaka. Alikipa kila kiungo sehemu yake. 20 Hivyo kuna viungo vingi, lakini kuna mwili mmoja tu.

21 Jicho haliwezi kuuambia mkono, “Sikuhitaji!” Na kichwa hakiwezi kuuambia mguu, “sikuhitaji!” 22 Hapana, viungo vya mwili vinavyoonekana kuwa dhaifu zaidi, ndivyo vilivyo na umuhimu zaidi. 23 Na viungo ambavyo tunadhani kuwa vina umuhimu mdogo ndivyo tunavitunza kwa heshima kubwa. Na tunavitunza kwa kuvifunika kwa uangalifu maalum viungo vya mwili tusivyotaka kuvionesha. 24 Viungo vinavyopendeza zaidi visipofunikwa havihitaji matunzo haya maalum. Lakini Mungu aliuunganisha mwili pamoja na akavipa heshima zaidi viungo vilivyohitaji hadhi hiyo. 25 Mungu alifanya hivi ili mwili wetu usigawanyike. Mungu alitaka viungo vyote tofauti vitunzane kwa usawa. 26 Ikiwa kiungo kimoja cha mwili kinaugua, basi viungo vyote vinaugua pamoja nacho. Au ikiwa kiungo kimoja kinaheshimiwa, basi viungo vingine vyote vinashiriki heshima ya kiungo hicho.

27 Ninyi nyote kwa pamoja ni mwili wa Kristo. Kila mmoja wenu ni kiungo cha mwili huo. 28 Na Mungu ameweka katika kanisa, kwanza, baadhi kuwa mitume, pili manabii, na tatu walimu. Kisha Mungu ametoa nafasi kwa wale wanaofanya miujiza, wenye karama ya uponyaji, wanaoweza kuwasaidia wengine, wanaoweza kuwaongoza wengine na wale wanaoweza kuzungumza kwa lugha zingine. 29 Je, wote ni mitume? Je, wote ni manabii? Je, wote ni walimu? Je, wote hufanya miujiza? 30 Si wote wenye karama ya uponyaji. Si wote wanaozungumza kwa lugha zingine. Si wote wanaofasiri lugha. 31 Endeleeni kuwa na ari ya kuwa na karama za Roho mnazoona kuwa ni kuu zaidi. Lakini sasa ninataka kuwaonesha njia iliyo kuu zaidi.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International