Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Read the New Testament in 24 Weeks

A reading plan that walks through the entire New Testament in 24 weeks of daily readings.
Duration: 168 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Waebrania 12-13

Sisi Pia Tuufuate Mfano wa Yesu

12 Tunao hawa watu mashuhuri wakituzunguka kama mifano kwetu. Maisha yao yanatueleza imani ni nini. Hivyo, nasi pia, tunapaswa kufanya mashindano yaliyo mbele yetu na kamwe tusikate tamaa. Tunapaswa kuondoa katika maisha yetu kitu chochote kitakachotupunguzia mwendo pamoja na dhambi zinazotufanya tutoke kwenye mstari mara kwa mara. Hatupaswi kuacha kumwangalia Yesu. Yeye ndiye kiongozi wa imani yetu, na ndiye anayeikamilisha imani yetu. Aliteseka hadi kufa msalabani. Lakini aliikubali aibu ya msalaba kama kitu kisicho na maana kwa sababu ya furaha ambayo angeiona ikimngojea. Na sasa ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Mfikirie Yesu. Kwa uvumilivu alistahimili matusi ya hasira ya watenda dhambi waliokuwa wakiwapigia kelele. Mfikirie yeye ili usikate tamaa na kuacha kujaribu.

Mungu ni Kama Baba

Mnashindana na dhambi, lakini bado hamjamwaga damu hata kuutoa uhai wenu katika mashindano hayo. Ninyi ni watoto wa Mungu, naye huzungumza maneno ya faraja kwenu. Labda mmeyasahau maneno haya:

“Mwanangu, wakati Mungu anapokurekebisha,
    zingatia na usiache kujaribu.
Bwana humrekebisha kila anayempenda;
    humpa adhabu kila anayemkubali kama mwana wake.”(A)

Hivyo muyapokee mateso kama adhabu ya baba. Mungu hufanya mambo haya kwenu kama baba anavyowarekebisha watoto wake. Mnajua kuwa watoto wote hurekebishwa na baba zao. Hivyo, kama hukupata marekebisho ambayo kila mtoto anapaswa kuyapata, wewe siyo mtoto wa kweli na hakika wewe siyo wa Mungu. Sisi wote tulikuwa na baba wa hapa duniani walioturekebisha, na tuliwaheshimu. Ni muhimu zaidi basi kwamba tunapaswa kuyapokea marekebisho kutoka kwa Baba wa roho zetu. Tukifanya hivyo, tutakuwa na uzima. 10 Baba zetu wa duniani waliturekebisha kwa muda mfupi katika njia waliyofikiri ilikuwa bora zaidi. Lakini Mungu huturekebisha sisi ili atusaidie tuweze kuwa watakatifu kama yeye. 11 Hatufurahii marekebisho tunapokuwa tunayapata. Yanauma. Lakini baadaye, baada ya kujifunza somo kutokana na hayo, tutaifurahia amani itakayokuja kwa njia ya kufanya yaliyo sahihi.

Muwe Makini Jinsi Mnavyoishi

12 Mmekuwa dhaifu, hebu mjitie nguvu tena. 13 Muishi katika njia iliyo sahihi ili muweze kuokolewa na udhaifu wenu hautawasababisha ninyi kupotea.

14 Jitahidini kuishi kwa amani na kila mtu. Na mjitahidi kuyaweka mbali na dhambi maisha yenu. Yeyote ambaye maisha yake siyo matakatifu hawezi kumwona Bwana. 15 Muwe makini ili mtu asije akakosa kuipata neema ya Mungu. Muwe makini ili asiwepo atakayepoteza imani yake na kuwa kama gugu chungu linalomea miongoni mwenu. Mtu wa jinsi hiyo anaweza kuharibu kundi lenu lote. 16 Muwe makini ili asiwepo yeyote atakayefanya dhambi ya uzinzi au kushindwa kumheshimu Mungu moyoni kama alivyofanya Esau. Kama kijana mkubwa katika nyumba ya babaye, Esau angerithi sehemu kubwa ya vitu kutoka kwa baba yake. Lakini akauza kila kitu kwa mlo mmoja tu. 17 Mnakumbuka kwamba baada ya Esau kufanya hivi, akataka kupata baraka za baba yake. Akaitamani sana baraka ile kiasi kwamba akalia. Lakini baba yake akakataa kumpa baraka hiyo, kwa sababu Esau hakupata njia ya kubadili yale aliyotenda.

18 Ninyi ni watu wa Mungu, kama watu wa Israeli walipofika katika Mlima Sinai. Lakini hamjaufikia mlima halisi wa kuweza kushikwa. Mlima huo haupo kama ule waliouona, uliokuwa ukiwaka moto na kufunikwa na giza, utusitusi na dhoruba. 19 Haipo sauti ya tarumbeta au sauti iliyoyasema maneno kama hayo waliyoyasikia. Walipoisikia sauti, wakasihi kamwe wasisikie neno lingine. 20 Hawakutaka kusikia amri: “Kama chochote, hata mnyama, akigusa mlima, lazima kiuawe kwa kupigwa mawe.”(B) 21 Kile walichoona kilikuwa cha kutisha kiasi kwamba Musa akasema, “Natetemeka kwa hofu.”(C)[a]

22 Lakini mmeufikia Mlima Sayuni, kwenye mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni.[b] Mmefika mahali ambapo maelfu wa malaika wamekusanyika kusherehekea. 23 Mmefika katika kusanyiko la watoto wazaliwa wa kwanza wa Mungu. Majina yao yameandikwa mbinguni. Mmemfikia Mungu, hakimu wa watu wote. Na mmefika kwenye roho za watu wema ambao wamekamilishwa. 24 Mmemfikia Yesu; yeye aliyelileta kutoka kwa Mungu agano jipya kwenda kwa watu wake. Mmefika kwenye damu iliyonyunyizwa[c] ambayo inasema habari za mema zaidi kuliko damu ya Habili.

25 Muwe makini na msijaribu kupuuza kusikiliza Mungu anaposema. Watu wale walipuuza kumsikiliza yeye alipowaonya hapa duniani. Nao hawakuponyoka. Sasa Mungu anasema kutoka mbinguni. Hivyo sasa itakuwa vibaya zaidi kwa wale watakaopuuza kumsikiliza yeye. 26 Alipozungumza pale mwanzoni, sauti yake iliitetemesha dunia. Lakini sasa ameahidi, “Kwa mara nyingine tena nitaitetemesha dunia, lakini pia nitazitetemesha mbingu.”(D) 27 Maneno “Kwa mara nyingine” yanatuonyesha kwa uwazi kwamba kila kitu kilichoumbwa kitaangamizwa; yaani, vitu vinavyoweza kutetemeshwa. Na ni kile tu kisichoweza kutetemeshwa kitakachobaki.

28 Hivyo tunahitajika kuwa na shukrani kwa sababu tunao ufalme ambao hauwezi kutetemeshwa. Na kwa sababu sisi ni watu wa shukrani, tunahitajika kumwabudu Mungu kwa njia itakayompendeza yeye. Tunahitajika kufanya hivi kwa heshima na hofu, 29 kwa sababu “Mungu wetu yuko kama moto unaoweza kutuangamiza sisi.”(E)

Ibada Inayompendeza Mungu

13 Endeleeni kupendana ninyi kwa ninyi kama kaka na dada katika Kristo. Mkikumbuka kuwasaidia watu kwa kuwakaribisha majumbani mwenu. Watu wengine wamefanya hivyo na wakawa wamewasaidia malaika pasipo wao kujua. Msiwasahau wale walioko magerezani. Wakumbukeni kama vile mko magerezani pamoja nao. Na msiwasahau wale wanaoteseka. Wakumbukeni kama vile mnateseka pamoja nao.

Ndoa iheshimiwe na kila mmoja. Na kila ndoa itunzwe kwa usafi kati ya mume na mke. Mungu atawahukumu kuwa na hatia wale wanaofanya uzinzi na uasherati. Yatunzeni maisha yenu yawe huru kutokana na kupenda fedha. Na mridhike na kile mlichonacho. Mungu amesema: “Sitakuacha kamwe; Sitakukimbia kamwe.”(F) Hivyo tunaweza kuwa na uhakika na kusema:

“Bwana ndiye msaidizi wangu;
    Sitaogopa.
Watu hawawezi kunifanya chochote.”(G)

Wakumbukeni viongozi wenu. Waliwafundisha ujumbe wa Mungu. Kumbukeni jinsi walivyoishi na walivyokufa, na muiige imani yao. Yesu Kristo ni yule yule jana, leo na hata milele. Msiruhusu aina yoyote ya mafundisho mageni yawaongoze hadi katika njia isiyo sahihi. Itegemeeni neema ya Mungu pekee kwa ajili ya nguvu za kiroho, siyo katika sheria kuhusu vyakula. Kuzitii sheria hizi hakumsaidii yeyote.

10 Tunayo sadaka. Na wale makuhani waliotumika ndani ya Hema Takatifu hawawezi kula sadaka tuliyo nayo. 11 Kuhani mkuu hubeba damu za wanyama hadi Patakatifu pa Patakatifu na hutoa damu hiyo kwa ajili ya dhambi. Lakini miili ya wanyama hao huchomwa nje ya kambi. 12 Hivyo Yesu naye alitesekea nje ya mji. Alikufa ili awatakase watu wake kwa damu yake mwenyewe. 13 Hivyo tumwendee Yesu nje ya kambi na kuikubali aibu hiyo hiyo aliyoipata yeye. 14 Hatuna mji unaodumu milele hapa duniani. Lakini tunaungoja mji tutakaoupata hapo baadaye. 15 Hivyo kwa njia ya Yesu hatupaswi kuacha kumtolea Mungu sadaka zetu. Dhabihu hizo ni sifa zetu, zinazotoka katika vinywa vyetu vinavyolisema jina lake. 16 Na msisahau kutenda mema na kushirikishana na wengine mlivyo navyo, kwa sababu sadaka kama hizi zinamfurahisha sana Mungu.

17 Muwatii viongozi wenu. Muwe tayari kufanya yale wanayowaambia. Wanawajibika katika maisha yenu ya kiroho, hivyo nyakati zote wanaangalia jinsi ya kuwalinda ninyi. Muwatii ili kazi yao iwafurahishe wao, siyo kupata majonzi. Haitawasaidia ninyi mnapowasababishia matatizo.

18 Endeleeni kutuombea. Tunajisikia tuko sahihi katika tunayoyafanya, kwa sababu nyakati zote tunajitahidi kadri tuwezavyo. 19 Na nawasihi muombe ili Mungu anirudishe tena kwenu mapema. Nalitamani sana hili kuliko kitu chochote.

20-21 Ninawaombea Mungu wa amani awape ninyi mambo mazuri mnayohitaji ili muweze kufanya anayoyapenda. Mungu ndiye aliyemfufua Bwana Yesu kutoka katika kifo, Mchungaji Mkuu wa kondoo wake. Alimfufua kwa sababu Yesu aliitoa sadaka ya damu yake ili kulianza agano jipya lisilo na mwisho. Namwomba Mungu atuwezeshe kwa njia ya Yesu Kristo kufanya mambo yanayompendeza yeye. Utukufu ni wake milele. Amina.

22 Ndugu na dada zangu, nawasihi msikilize kwa uvumilivu katika yale niliyoyasema. Niliandika barua hii ili kuwatia moyo. Na siyo ndefu sana. 23 Nawataka mjue kwamba ndugu yetu Timotheo ametoka gerezani. Akija kwangu mapema, sote tutakuja kuwaona ninyi.

24 Fikisheni salama zangu kwa viongozi wote na kwa watu wote wa Mungu. Wote walioko Italia wanawasalimuni.

25 Naomba neema ya Mungu iwe nanyi nyote.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International