Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Read the New Testament in 24 Weeks

A reading plan that walks through the entire New Testament in 24 weeks of daily readings.
Duration: 168 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Waebrania 10-11

Yesu Kristo, Dhabihu Pekee Tunayoihitaji

10 Sheria ya Musa ilitupa sisi picha tu isiyo wazi sana ya mambo yaliyokuwa yanakuja baadaye. Sheria siyo picha kamili ya mambo halisi. Sheria huwaambia watu kutoa sadaka zile zile kila mwaka. Wale wanaokuja kumwabudu Mungu wanaendelea kutoa sadaka. Lakini sheria haiwezi kamwe kuwakamilisha wao. Kama sheria ingeweza kuwakamilisha watu, sadaka hizi zingekuwa zimekoma. Tayari wao wangekuwa safi kutoka katika dhambi, na bado wasingehukumiwa moyoni mwao. Lakini hayo siyo yanayotokea. Dhabihu zao zinawafanya wazikumbuke dhambi zao kila mwaka, kwa sababu haiwezekani kwa damu ya fahali na mbuzi kuondoa dhambi.

Hivyo baada ya Kristo kuja ulimwenguni alisema:

“Huhitaji sadaka na sadaka,
    lakini umeandaa mwili kwa ajili yangu.
Hukuridhishwa na sadaka za kuteketezwa
    na sadaka kuondoa dhambi.
Kisha nikasema, ‘Nipo hapa, Mungu.
    Imeandikwa juu yangu katika kitabu cha sheria.
    Nimekuja kufanya yale unayopenda.’”(A)

Kwanza Kristo alisema, “Wewe hufurahishwi na sadaka na sadaka. Hukuridhishwa na sadaka za kuteketezwa na sadaka ili kuondoa dhambi.” (Hizi ndizo sadaka zote ambavyo sheria inaagiza.) Kisha akasema, “Niko hapa, Mungu. Nimekuja kufanya yale unayopenda.” Hivyo Mungu akafikisha mwisho wa mfumo wa zamani wa utoaji sadaka na akaanzisha njia mpya. 10 Yesu Kristo alifanya mambo ambayo Mungu alimtaka ayafanye. Na kwa sababu ya hilo, tunatakaswa kwa njia ya sadaka ya mwili wa Kristo. Kristo aliitoa sadaka hiyo mara moja, inayotosha kwa nyakati zote.

11 Kila siku makuhani husimama na kutekeleza shughuli zao za kidini. Tena na tena hutoa sadaka zilezile, ambazo kamwe haziwezi kuondoa dhambi. 12 Lakini Kristo alitoa sadaka moja tu kwa ajili ya dhambi, na sadaka hiyo ni nzuri kwa nyakati zote. Kisha akakaa mkono wa kuume wa Mungu. 13 Na sasa Kristo anawasubiria hapo adui zake wawekwe chini ya mamlaka yake.[a] 14 Kwa sadaka moja Kristo akawakamilisha watu wake milele. Ndio wale wanaotakaswa.

15 Roho Mtakatifu pia anatuambia juu ya hili. Kwanza anasema:

16 “Hili ndilo agano[b] nitakaloweka
    na watu wangu baadaye, asema Bwana.
Nitaziweka sheria zangu ndani ya mioyo yao.
    Nitaziandika sheria zangu katika fahamu zao.”(B)

17 Kisha anasema,

“Nitazisahau dhambi zao
    na nisikumbuke kamwe uovu walioutenda.”(C)

18 Na baada ya kila kitu kusamehewa, hakuna tena haja ya sadaka ili kuziondoa dhambi.

Mkaribieni Mungu

19 Hivyo ndugu na dada, tuko huru kabisa kupaingia Patakatifu pa Patakatifu. Tunaweza kufanya hivi bila hofu kwa sababu ya sadaka ya damu ya Yesu. 20 Tunaingia kwa njia mpya ambayo Yesu alitufungulia. Ni njia iliyo hai inayotuelekeza kupitia pazia; yaani mwili wa Yesu. 21 Na tunaye kuhani mkuu zaidi anayeisimamia nyumba ya Mungu. 22 Ikiwa imenyunyiziwa kwa damu ya Kristo, mioyo yetu imewekwa huru kutokana na dhamiri yenye hukumu, na miili yetu imeoshwa kwa maji safi. Hivyo mkaribieni Mungu kwa moyo safi, mkijaa ujasiri kwa sababu ya imani katika Kristo. 23 Tunapaswa kuling'ang'ania tumaini tulilonalo, bila kusitasita kuwaeleza watu juu yake. Tunaweza kumwamini Mungu kuwa atatimiza aliyoahidi.

Saidianeni Ninyi kwa Ninyi Kuwa Imara

24 Tunahitaji kumfikiria kila mtu kuona jinsi tunavyoweza kuhamasishana kuonesha upendo na kazi njema. 25 Tusiache kukutana pamoja, kama wanavyofanya wengine. Hapana, tunahitaji kuendelea kuhimizana wenyewe. Hili linazidi kuwa muhimu zaidi na zaidi kadri mnavyoona ile Siku inakaribia.

Msigeuke Mbali ya Mwana wa Mungu

26 Kama tutaamua kuendelea kutenda dhambi baada ya kujifunza ukweli, ndipo hakutakuwa sadaka nyingine itakayoondoa dhambi. 27 Tukiendelea kutenda dhambi, kitakachokuwa kimebaki kwetu ni wakati wa kutisha wa kuingoja hukumu na moto wa hasira utakaowaangamiza wale wanaoishi kinyume na Mungu. 28 Yeyote aliyekataa kuitii Sheria ya Musa alipatikana ana hatia kutokana na ushuhuda uliotolewa na mashahidi wawili au watatu. Watu wa jinsi hiyo hawakusamehewa. Waliuawa. 29 Hivyo fikiri jinsi watu watakavyostahili kuhukumiwa zaidi ambao wanaonesha kumchukia mwana wa Mungu; watu wanaoonesha kuwa hawana heshima kwa sadaka ya damu iliyoanzisha agano jipya na mara moja ikawatakasa au wale wanaomkashifu Roho wa neema ya Mungu. 30 Tunajua kuwa Mungu alisema, “Nitawaadhibu watu kwa ajili ya makosa wanayofanya”;(D) nitawalipa tu Pia alisema, “BWANA atawahukumu watu wake.”(E) 31 Ni jambo la kutiisha kukutana na hukumu kutoka kwa Mungu aliye hai.

Endeleeni na Ujasiri na Uvumilivu Mlionao

32 Zikumbukeni siku za kwanza mlipojifunza kweli. Mlikuwa na mashindano magumu pamoja na mateso mengi, lakini mkaendelea kuwa imara. 33 Mara zingine watu waliwasemea mambo ya chuki na kuwatesa hadharani. Na nyakati zingine mliwasaidia wengine waliokuwa wakitendewa vivyo hivyo. 34 Ndiyo, mliwasaidia magerezani na kushiriki katika mateso yao. Na bado mlikuwa na furaha wakati kila kitu mlichokimiliki kilipochukuliwa kutoka kwenu. Mkaendelea kufurahi, kwa sababu mlijua kwamba mnacho kitu kilicho bora zaidi; kitu kitakachoendelea milele.

35 Hivyo msipoteze ujasiri mliokuwa nao zamani. Ujasiri wenu utalipwa sana. 36 Mnahitajika kuwa na subira. Baada ya kufanya yale anayotaka Mungu, mtapata aliyowaahidi.

37 “Karibu sana sasa, yeye ajaye
    atakuja wala hatachelewa.
38 Mtu aliye sahihi mbele zangu
    ataishi akiniamini mimi.
Lakini sitafurahishwa na yule
    anayegeuka nyuma kwa ajili ya woga.”(F)

39 Lakini sisi siyo wale wanaogeuka nyuma na kuangamia. Hapana, sisi ni watu walio na imani na tunaokolewa.

Imani

11 Imani inaleta uthabiti wa mambo tunayoyatarajia. Ni uthibitisho wa yale tusiyoweza kuyaona. Mungu alifurahishwa na watu walioishi muda mrefu uliopita kwa sababu walikuwa na imani ya namna hii.

Imani hutusaidia sisi kufahamu kwamba Mungu aliumba ulimwengu wote kwa amri yake. Hii inamaanisha kwamba vitu tunavyoviona viliumbwa kwa kitu kisichoonekana.

Kaini na Habili wote walitoa sadaka kwa Mungu. Lakini Habili alitoa sadaka bora zaidi kwa Mungu kwa sababu alikuwa na imani. Mungu akasema alifurahishwa na kile alichotoa Habili. Na hivyo Mungu akamwita kuwa mtu mwema kwa sababu alikuwa na imani. Habili akafariki, lakini kupitia imani yake bado anazungumza.

Henoko alitwaliwa kutoka duniani, hivyo kamwe yeye hajafariki. Maandiko yanatueleza kwamba kabla ya kuchukuliwa, alikuwa mtu aliyempendeza Mungu. Baadaye, hayupo yeyote aliyejua kule alikokuwa, kwa sababu Mungu alimchukua Henoko ili awe pamoja naye. Haya yote yakatokea kwa vile alikuwa na imani. Bila kuwa na imani hakuna anayeweza kumfurahisha Mungu. Yeyote anayemjia Mungu anatakiwa kuamini kwamba yeye ni hakika na kwamba anawalipa wale ambao kwa uaminifu wanajitahidi kumtafuta.

Nuhu alionywa na Mungu juu ya mambo ambayo hakuwa ameyaona bado. Lakini alikuwa na imani na heshima kwa Mungu, hivyo akaijenga meli kubwa ili kuiokoa familia yake. Kwa imani yake, Nuhu alionesha kwamba ulimwengu ulikuwa umekosea. Na akawa ni mmoja wa wale waliohesabiwa haki na Mungu kwa njia ya imani.

Mungu alimwita Ibrahimu kusafiri kwenda sehemu ingine aliyoahidi kumpa. Ibrahimu hakujua hiyo sehemu ingine ilikuwa wapi. Lakini alimtii Mungu na akaanza kusafiri kwa sababu alikuwa na imani. Ibrahimu akaishi katika nchi ambayo Mungu aliahidi kumpa. Akaishi humo kama mgeni tu asiyekuwa mwenyeji. Alifanya hivi kwa sababu alikuwa na imani. Akaishi katika mahema pamoja na Isaka na Yakobo, ambao pia walipokea ahadi ile ile kutoka kwa Mungu. 10 Ibrahimu alikuwa anaungoja mji[c] ambao ulikuwa na misingi halisi. Alikuwa anaungoja mji ulibuniwa na kujengwa na Mungu.

11 Sara hakuwa na uwezo wa kupata watoto, na Ibrahimu alikuwa amezeeka sana. Lakini alikuwa anamwamini Mungu, akimwamini kuwa anaweza kutenda yale aliyoahidi. Hivyo Mungu akawawezesha kupata watoto. 12 Ibrahimu alikuwa amezeeka sana karibu ya kufa. Lakini kupitia kwa mtu huyo mmoja vikaja vizazi vingi kama zilivyo nyota za angani. Hivyo watu wengi wakaja kutoka kwake wakiwa kama punje za mchanga katika ufukwe wa bahari.

13 Watu hawa wote mashuhuri wakaendelea kuishi kwa imani hadi walipofariki. Hawakuwa wamepata mambo ambayo Mungu aliwaahidi watu wake. Lakini walikuwa na furaha kuona tu kwamba ahadi hizi zilikuwa zinakuja kwa mbali siku zijazo. Waliukubali ukweli kwamba wao walikuwa kama wageni na wasafiri hapa duniani. 14 Watu wanapolikubali jambo la namna hiyo, wanaonesha kuwa wanaingojea nchi itakayokuwa yao wenyewe. 15 Kama wangekuwa wanaifikiria nchi walikotoka, wangekuwa wamerejea. 16 Lakini walikuwa wanaingoja nchi iliyo bora zaidi, nchi ya mbinguni. Hivyo Mungu haoni aibu kuitwa Mungu wao. Naye amewaandalia mji.

17-18 Mungu aliijaribu imani ya Ibrahimu. Mungu alimtaka amtoe Isaka kama sadaka. Ibrahimu akatii kwa sababu alikuwa na imani. Tayari alikuwa na ahadi kutoka kwa Mungu. Na Mungu tayari alikuwa amekwishamwambia, “Ni kupitia kwa Isaka kwamba vizazi vyako watakuja.”(G) Lakini Ibrahimu alikuwa tayari kumtoa mwana wake wa pekee. Alifanya hivi kwa sababu alikuwa na imani. 19 Aliamini kwamba Mungu angeweza kuwafufua watu kutoka kifoni. Na hakika, Mungu alipomzuia Ibrahimu katika kumuua Isaka, ilikuwa ni kama vile alimpata tena kutoka kifoni.

20 Isaka akayabariki maisha ya mbeleni ya Yakobo na Esau. Alifanya hivyo kwa sababu alikuwa na imani. 21 Na Yakobo, pia kwa vile alikuwa na imani, alimbariki kila mmoja wa wana wa Yusufu. Alifanya haya wakati alipokuwa akifa, akaiegemea fimbo yake akimwabudu Mungu.

22 Na Yusufu alipokuwa karibu amefariki, alizungumza kuhusu watu wa Israeli kuondoka Misri. Na aliwaambia yale waliyotakiwa kuufanyia mwili wake. Alifanya haya kwa sababu alikuwa na imani.

23 Na mama na baba wa Musa wakaona kwamba alikuwa ni mtoto mzuri hivyo wakamficha kwa miezi mitatu baada ya kuzaliwa kwake. Hili lilikuwa kinyume na agizo la mfalme. Lakini hawakuogopa kwa sababu walikuwa na imani.

24-25 Musa akakua na akawa mwanaume. Akakataa kuitwa mwana wa binti Farao. Akachagua kutokujifurahisha katika raha na dhambi zinazodumu kwa muda mfupi tu. Badala yake, akachagua kuteseka pamoja na watu wa Mungu. Alifanya hivi kwa sababu alikuwa na imani. 26 Alifikiri kuwa ni bora kuteseka kwa ajili ya Masihi kuliko kuwa na hazina zote za Misri. Alikuwa anaisubiri malipo ambayo Mungu angempa.

27 Musa akaondoka Misri kwa sababu alikuwa na imani. Hakuiogopa hasira ya mfalme. Aliendelea kuwa jasiri kama vile angemwona Mungu ambaye hakuna mtu mwingine angeweza kumwona. 28 Na kwa sababu alikuwa na imani, Musa akaandaa mlo wa Pasaka. Na akanyunyiza damu ya mwanakondoo katika miimo ya milango ya watu wake, ili kwamba malaika wa kifo[d] asiwaue wazaliwa wao wa kwanza wa kiume.

29 Na watu wa Mungu wote wakatembea kuvuka Bahari ya Shamu kama vile ilikuwa ni ardhi kavu. Waliweza kufanya hivi kwa sababu walikuwa na imani. Lakini wakati Wamisri walipojaribu kuwafuata, wote wakazama majini.

30 Na kuta za Yeriko zilianguka kwa ajili ya imani ya watu wa Mungu. Walitembea kuuzunguka ukuta kwa siku saba, na kisha kuta zikaanguka.

31 Na Rahabu, yule kahaba, aliwakaribisha wapelelezi wa Kiisraeli kama marafiki. Na kwa sababu ya imani yake, hakuuawa pamoja na wale waliokataa kutii.

32 Je, nahitaji niwape mifano zaidi? Sina muda wa kutosha kuwaeleza kuhusu Gidioni, Baraki, Samsoni, Yefta, Daudi, Samweli na manabii. 33 Wote walikuwa na imani kuu. Na kwa njia ya imani hiyo wakaziangusha falme. Wakafanya kilichokuwa sahihi, na Mungu akawasaidia katika njia alizoahidi. Kwa imani zao watu wengine waliifunga midomo ya simba. 34 Na wengine waliweza kuizuia miali ya moto. Wengine wakaepuka katika kuuawa kwa upanga. Wengine waliokuwa dhaifu wakafanywa wenye nguvu. Wakawa na nguvu katika vita na kuyaangusha majeshi mengine. 35 Walikuwepo wanawake waliowapoteza wapendwa wao lakini wakawapata tena walipofufuliwa kutoka wafu. Wengine waliteswa lakini wakakataa kuukubali uhuru wao. Walifanya hivi ili waweze kufufuliwa kutoka kifoni kuingia katika maisha bora zaidi. 36 Wengine walichekwa na kupigwa. Wengine walifungwa na kutiwa magerezani. 37 Waliuawa kwa mawe. Walikatwa vipande viwili. Waliuawa kwa panga. Mavazi pekee wengine wao waliyokuwa nayo yalikuwa ni ngozi za kondoo au za mbuzi. Walikuwa maskini, waliteswa, na kutendewa mabaya na wengine. 38 Ulimwengu haukustahili kuwa na watu wakuu na waaminifu kama hawa. Hawa waliweza kuzunguka jangwani na milimani, wakiishi katika mapango na mashimo ardhini.

39 Mungu alifurahishwa nao wote kwa sababu ya imani zao. Lakini hakuna hata mmoja wao aliyepokea ahadi ya Mungu. 40 Mungu alikusudia kitu bora zaidi kwa ajili yetu. Alitaka kutukamilisha sisi. Hakika, pia alitaka watu hawa wakuu wakamilishwe, lakini siyo kabla ya sisi wote kuzifurahia baraka pamoja.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International