Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

New Testament in a Year

Read the New Testament from start to finish, from Matthew to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Mathayo 21:1-22

Yesu Aingia Yerusalemu Kama Mfalme

(Mk 11:1-11; Lk 19:28-38; Yh 12:12-19)

21 Yesu na wafuasi wake walipokaribia Yerusalemu, walisimama Bethfage kwenye kilima kinachoitwa Mlima wa Mizeituni. Wakiwa hapo Yesu aliwatuma wafuasi wake wawili mjini. Aliwaambia, “Nendeni kwenye mji mtakaoweza kuuona huko. Mtakapoingia katika mji huo, mtamwona punda na mwanapunda wake.[a] Wafungueni wote wawili, kisha waleteni kwangu. Mtu yeyote akiwauliza kwa nini mnawachukua punda, mwambieni, ‘Bwana anawahitaji. Atawarudisha mapema.’”

Hili lilitimiza maneno yaliyosemwa na nabii:

“Waambie watu wa Sayuni,[b]
    ‘Mfalme wako anakuja sasa.
Ni mnyenyekevu na amempanda punda.
    Na amempanda mwana punda dume tena safi.’”(A)

Wafuasi walikwenda na kufanya yale walioambiwa na Yesu. Waliwaleta kwake punda jike na mwanapunda. Waliwafunika punda kwa nguo zao na Yesu akaketi juu yao. Akiwa njiani kuelekea Yerusalemu, watu wengi walitandaza mavazi yao barabarani kwa ajili Yake. Wengine walikata matawi ya miti na kuyatandaza barabarani ili kumkaribisha. Wengine walimtangulia Yesu, na wengine walikuwa nyuma yake. Wote walipaza sauti wakisema:

“Msifuni[c] Mwana wa Daudi!
‘Karibu! Mungu ambariki yeye
    ajaye katika jina la Bwana!’(B)
Msifuni Mungu wa mbinguni!”

10 Kisha Yesu aliingia Yerusalemu. Watu wote mjini wakataharuki. Wakauliza, “Mtu huyu ni nani?”

11 Kundi la watu waliomfuata Yesu wakajibu, “Huyu ni Yesu. Ni nabii kutoka katika mji wa Nazareti ulio Galilaya.”

Yesu Asafisha Eneo la Hekalu

(Mk 11:15-19; Lk 19:45-48; Yh 2:13-22)

12 Yesu alipoingia katika eneo la Hekalu, aliwatoa nje wote waliokuwa wanauza na kununua vitu humo. Alizipindua meza za watu waliokuwa wanabadilishana pesa. Na alipindua viti vya watu waliokuwa wanauza njiwa. 13 Yesu aliwaambia, “Maandiko yanasema, ‘Hekalu langu litaitwa nyumba ya sala.’(C) Lakini mmelibadilisha na kuwa ‘maficho ya wezi’.(D)

14 Baadhi ya watu waliokuwa wasiyeona na walemavu wa miguu walimjia Yesu alipokuwa eneo la Hekalu, naye aliwaponya. 15 Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria waliona mambo ya ajabu aliyokuwa anatenda. Na waliona watoto walivyokuwa wanamsifu wakisema, “Sifa kwa Mwana wa Daudi.” Mambo haya yote yaliwakasirisha makuhani na walimu wa sheria.

16 Wakamwuliza Yesu, “Unasikia wanayosema watoto hawa?”

Akajibu, “Ndiyo. Maandiko yanasema,

‘Umewafundisha watoto wadogo na watoto
    wanyonyao kusifu.’(E)

Hamjasoma Maandiko haya?”

17 Kisha Yesu akawaacha na akaenda katika mji wa Bethania akalala huko.

Yesu Aulaani Mtini

(Mk 11:12-14,20-24)

18 Mapema asubuhi iliyofuata, Yesu alikuwa anarudi mjini Yerusalemu naye alikuwa na njaa. 19 Aliuona mtini karibu na njia na akaenda kuchuma tini kwenye mti huo. Yalikuwepo maua tu. Hivyo Yesu akauambia mti ule, “Hautazaa matunda tena!” Mtini ukakauka na kufa hapo hapo.

20 Wafuasi wake walipoona hili, walishangaa sana. Wakauliza, “Imekuwaje mtini ukakauka na kufa haraka hivyo?”

21 Yesu akajibu, “Ukweli ni kuwa, mkiwa na imani na msiwe na mashaka, mtaweza kufanya kama nilivyofanya kwa mti huu. Na mtaweza kufanya zaidi ya haya. Mtaweza kuuambia mlima huu, ‘Ng'oka na ujitupe baharini.’ Na ikiwa una imani, litafanyika. 22 Mkiamini, mtapokea kila mnachoomba.”

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International