New Testament in a Year
22 Musa alielimishwa kwa elimu bora ya Kimisri. Wamisri walimfundisha kila kitu walichojua. Alikuwa mwenye nguvu katika yote aliyosema na kutenda.
23 Musa alipokuwa na umri wa miaka kama arobaini, aliamua kuwatembelea watu wake mwenyewe, watu wa Israeli. 24 Aliona mmoja wao ananyanyaswa na Mmisri, hivyo akamtetea; Musa akampiga na kumwua Mmisri ili kulipiza kwa kumwumiza Mwisraeli. 25 Musa alidhani kwamba watu wake wangeelewa kuwa Mungu alikuwa anamtumia kuwaokoa. Lakini hawakuelewa.
26 Siku iliyofuata, Musa akawaona wawili wa watu wake wakipigana. Alijaribu kuwapatanisha kwa kuwaambia, ‘Ninyi ni ndugu! Kwa nini mnataka kuumizana?’ 27 Aliyekuwa akimwumiza mwenzake akamsukuma Musa na akamwambia, ‘Nani amekufanya wewe uwe mtawala na mwamuzi wetu? 28 Unataka kuniua kama ulivyomwua yule Mmisri jana?’(A) 29 Musa alipomsikia akisema hili, alikimbia Misri. Alikwenda kuishi Midiani kama mgeni. Katika kipindi alichoishi huko, alipata wana wawili.
30 Miaka arobaini baadaye, Musa alipokuwa jangwani karibu na Mlima Sinai, malaika alimtokea katika mwali wa moto uliokuwa unawaka katika kichaka. 31 Musa alipoliona hili, alishangaa. Alisogea ili kuangalia kwa karibu. Akasikia sauti; ilikuwa sauti ya Bwana. 32 Bwana alisema, ‘Mimi ni Mungu yule yule aliyeabudiwa na baba zako. Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo.’(B) Musa akaanza kutetemeka kwa woga. Aliogopa kukitazama kichaka.
33 Kisha Bwana akamwambia, ‘Vua viatu vyako, kwa sababu mahali uliposimama ni ardhi takatifu. 34 Nimewaona watu wangu wanavyoteseka sana Misri. Nimesikia watu wangu wakilia na nimeshuka ili kuwaokoa. Njoo sasa, Musa, ninakutuma urudi Misri.’(C)
35 Huyu ni Musa ndiye aliyekataliwa na watu wake. Walisema, ‘Nani amekufanya uwe mtawala na mwamuzi wetu?’(D) Lakini ndiye aliyetumwa na Mungu kuwa mtawala na mwokozi. Mungu alimtuma pamoja na msaada wa malaika,[a] ambaye Musa alimwona katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto. 36 Hivyo Musa aliwaongoza watu kutoka Misri. Alitenda maajabu na ishara za miujiza Misri, katika bahari ya Shamu na jangwani kwa miaka arobaini.
37 Huyu ni Musa yule yule aliyewaambia maneno haya watu wa Israeli: ‘Mungu atakupa nabii. Nabii huyo atakuja kutoka miongoni mwa watu wako mwenyewe. Atakuwa kama mimi.’(E) 38 Musa huyo huyo alikuwa pamoja na kusanyiko la watu wa Mungu jangwani. Alikuwa na malaika aliyezungumza naye alipokuwa Mlima Sinai, na alikuwa pamoja na baba zetu. Alipokea maneno yaletayo uzima kutoka kwa Mungu, na Musa akatupa sisi Maneno hayo.
39 Lakini baba zetu hawakutaka kumtii Musa. Walimkataa, wakataka kurudi Misri. 40 Walimwambia Haruni, ‘Musa alituongoza kutoka katika nchi ya Misri. Lakini hatujui kilichompata. Hivyo tengeneza miungu ili iwe mbele yetu ituongoze.’(F) 41 Hivyo watu wakatengeneza kinyago kinachofanana na ndama. Kisha wakakitolea sadaka za kuteketezwa. Walifurahia kile walichotengeneza kwa mikono yao wenyewe. 42 Lakini Mungu akawaacha, nao wakaendelea kuabudu nyota na sayari.[b] Kitabu cha manabii[c] kinasema hivi:
‘Watu wa Israeli, hamkunipa dhabihu
jangwani kwa miaka arobaini.
43 Mlibeba hema kwa ajili ya kumwabudia Moleki,
na sanamu ya nyota ya mungu wenu Refani.
Hizi zilikuwa sanamu mlizotengeneza ili mziabudu.
Hivyo nitawahamishia mbali, kuvuka Babeli.’(G)
© 2017 Bible League International