M’Cheyne Bible Reading Plan
Yesu Amponya Mtu Mwenye Pepo
5 Wakafika upande wa pili wa ziwa wakaingia katika jimbo la Wagerasi. 2 Yesu alipotoka kwenye mashua, mtu mmoja mwenye pepo mchafu alitoka makaburini akaja kukutana naye. 3 Mtu huyu aliishi makaburini wala hakuna aliyeweza kumfunga hata kwa minyororo , 4 kwa maana mara nyingi alipofungwa kwa minyororo mikononi na vyuma miguuni, aliivunjavunja na hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda. 5 Usiku na mchana alikaa makaburini na milimani aki piga makelele na kujikatakata kwa mawe.
6 Alipomwona Yesu kwa mbali, alimkimbilia akapiga magoti mbele yake, 7 akapiga kelele kwa nguvu akasema, “Unataka nini kwangu, Yesu, Mwana wa Mungu Mkuu? Ninakusihi kwa jina la Mungu, usinitese!” 8 Alisema hivi kwa kuwa Yesu alikuwa akimwambia, “Mtoke huyu mtu! Wewe pepo mchafu!”
9 Yesu akamwuliza, “Jina lako ni nani?” Akamjibu, “Jina langu ni jeshi, kwa maana tupo wengi.” 10 Akamwomba sana Yesu asiwapeleke nje ya jimbo lile. 11 Hapo hapo lilikuwapo kundi la nguruwe likilisha kando ya mlima. 12 Wale pepo wakamsihi Yesu, “Turuhusu tukawaingie wale nguruwe.” 13 Basi akawaruhusu. Wakamtoka yule mtu wakaenda wakawaingia wale nguruwe na kundi lote la nguruwe wapatao elfu mbili likatimka kasi kwenye mteremko ule, wakazama ziwani, wakafa.
14 Wale waliokuwa wakichunga hao nguruwe wakakimbilia mjini na vijijini kueleza yaliyotokea. Watu wakatoka kwenda kujionea mambo hayo.
15 Wakaja kwa Yesu, wakamwona yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo akiwa ameketi, amevaa nguo na pia akiwa na akili timamu. Wakaogopa. 16 Wale walioyaona mambo haya waliwaeleza wengine yaliyomto kea yule aliyekuwa na pepo na lile kundi la nguruwe. 17 Basi watu wakaanza kumwomba Yesu aondoke katika wilaya yao.
18 Yesu alipoanza kuingia kwenye mashua, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo akamsihi Yesu waende pamoja. 19 Yesu akamka talia. Badala yake akamwambia, “Nenda nyumbani kwa jamaa yako ukawaeleze mambo makuu aliyokutendea Bwana na jinsi alivyokuhuru mia.” 20 Yule mtu akaenda akaanza kutangaza katika Dekapoli - yaani miji kumi, mambo makuu aliyomtendea Bwana. Na watu wote wakastaajabu.
Yesu Amponya Mama Aliyetokwa Damu
21 Yesu alipokwisha vuka tena na kufika ng’ambo ya pili, umati mkubwa wa watu ukamzunguka, yeye akiwa kando ya ziwa. 22 Kisha kiongozi mmoja wa sinagogi aliyeitwa Yairo akamjia Yesu akapiga magoti miguuni pake, 23 akamsihi, “Binti yangu mdogo ni mgonjwa mahututi. Tafadhali njoo umguse kwa mikono yako apate kupona na kuishi.” 24 Basi Yesu akaongozana naye. Umati mkubwa wa watu waliomfuata wakawa wanamsonga.
25 Na alikuwepo mama mmoja aliyekuwa amesumbuliwa na tatizo la kutokwa damu kwa miaka kumi na miwili. 26 Mama huyu alikuwa amehangaika sana, akiwa ametibiwa na waganga wa kila aina na kutumia fedha yake yote kwa waganga lakini hakupata nafuu. Hali yake ilizidi kuwa mbaya. 27 Alikuwa amesikia habari za Yesu kwa hiyo alimfuata kwa nyuma, akapenyeza kati ya watu, akaligusa vazi lake. 28 Maana alisema moyoni mwake, “Nikiligusa vazi lake tu, nitapona.” 29 Mara damu iliyokuwa inamtoka ikakauka; akajisikia amepona kabisa.
30 Yesu akafahamu kuwa nguvu zimemtoka. Akageuka, akawauliza wale watu, “Ni nani amenigusa?”
31 Wanafunzi wake wakamjibu, “Mbona unauliza ni nani ameku gusa? Huoni umati huu ulivyokusonga?” 32 Lakini Yesu alizidi kutazama aone ni nani aliyemgusa. 33 Kisha yule mwanamke, akijua kilichomtokea, akaja, akaanguka miguuni kwake akitetemeka kwa hofu, akamweleza ukweli wote. 34 Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako.”
Yesu Amfufua Binti Yairo
35 Alipokuwa akiongea, watu wakafika kutoka nyumbani kwa Yairo wakamwambia, “Usimsumbue tena mwalimu, binti yako amefar iki. ” 36 Lakini Yesu hakuyatilia maanani maneno hayo, akamwam bia Yairo, “Usiogope, bali amini tu.”
37 Hakumruhusu mtu mwingine amfuate isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, nduguye Yakobo.
38 Walipofika nyumbani kwa yule kiongozi wa sinagogi, Yesu aliona vurugu na watu wengi wakilia na kuomboleza kwa nguvu. 39 Alipoingia ndani, aliwaambia, “Kwa nini mnafanya vurugu na kuomboleza? Mtoto hakufariki bali amelala.” 40 Wale watu wakam cheka kwa dharau. Lakini yeye akawatoa wote nje, akawachukua baba na mama wa yule mtoto pamoja na wale wanafunzi aliokuwa nao, wakaenda pale alipokuwa yule mtoto. 41 Akamwinua mtoto akamwam bia, “Talitha kumi!” Maana yake, “Binti mdogo, nakwambia amka!’ ’
42 Mara yule mtoto akasimama, akaanza kutembea. Alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili. Walipoona haya, walistaajabu sana. 43 Yesu akawaamuru wasimweleze mtu jambo hili, na akawaambia wampe yule mtoto chakula.
Kuwa Na Amani Na Mungu
5 Basi, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo. 2 Kwa kupitia kwake tumepata njia ya kufikia neema hii ambayo inatuwezesha kusimama imara, tukifurahia tumaini letu la kushiriki utukufu wa Mungu. 3 Zaidi ya hayo, pia tunafurahia mateso yetu kwa sababu tunafahamu kuwa mateso huleta subira; 4 na subira huleta uthabiti wa moyo; na uthabiti wa moyo hujenga tumaini. 5 Tukiwa na tumaini hatuwezi kukata tamaa kwa sababu Mungu amekwisha kumimina upendo wake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ni zawadi tuliyopewa na Mungu.
6 Tulipokuwa tungali wanyonge, wakati aliochagua Mungu, Kristo aliwafia wenye dhambi. 7 Ni vigumu sana kwa mtu kujitolea kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa yawezekana mtu akajitolea kufa kwa ajili ya mtu mwema. 8 Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo ali kufa kwa ajili yetu.
9 Basi, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa damu yake, bila shaka atatuokoa kutoka katika ghadhabu ya Mungu. 10 Kwa kuwa kama tulipokuwa maadui wa Mungu tulipatanishwa kwa kifo cha Mwanae, bila shaka sasa kwa kuwa tumepatanishwa, tutaokolewa kwa uzima wake. 11 Si hivyo tu, bali pia tunamfurahia Mungu katika Bwana wetu Yesu Kristo ambaye kwa ajili yake tumepokea upatanisho wetu.
Adamu Alileta Kifo, Yesu Ameleta Uzima
12 Kwa hiyo kama vile ambavyo dhambi iliingia ulimwenguni kupitia kwa mtu mmoja, na dhambi ikaleta kifo, na kwa njia hiyo kifo kikawajia watu wote kwa kuwa wote walitenda dhambi -
13 kwa maana kabla sheria haijatolewa dhambi ilikuwepo ulimwenguni. Lakini dhambi haihesabiwi ambapo hakuna sheria. 14 Hata hivyo tangu wakati wa Adamu hadi wakati wa Musa, kifo kiliwatawala watuwote hata wale ambao dhambi zao hazikuwa kama uasi wa Adamu. Adamu alikuwa mfano wa yule ambaye angalikuja. 15 Lakini zawadi iliyotolewa bure haiwezi kulinganishwa na ule uasi. Kwa maana ikiwa watu wengi walikufa kwa sababu ya uasi wa mtu mmoja, basi neema ya Mungu na zawadi iliyotolewa kwa ajili ya mtu mmoja, Yesu Kristo, imemiminika kwa wingi zaidi kwa watu wengi. 16 Pia zawadi ya Mungu sio kama matukio ya ile dhambi ya mtu mmoja. Kwa maana hukumu iliyotokana na uasi huo ilileta laana, lakini zawadi iliyopatikana bure baada ya dhambi nyingi, inaleta haki ya Mungu. 17 Na ikiwa kutokana na uasi wa mtu mmoja kifo kilitawala kupitia huyo mtu mmoja, wale wanaopokea wingi wa neema na zawadi ya bure ya kuhesabiwa haki, watatawala zaidi sana katika maisha kwa ajili ya huyo mtu mmoja, Yesu Kristo. 18 Kwa hiyo, kama vile uasi wa mtu mmoja ulivyoleta hukumu kwa watu wote, hali kadhalika, tendo la haki la mtu mmoja linawafanya watu wote waachiliwe huru na kupewa uzima. 19 Na kama vile ambavyo watu wengi walifanywa kuwa wenye dhambi kwa ajili ya kutokutii kwa mtu mmoja, vivyo hivyo wengi watahesabiwa haki na Mungu kwa ajili ya utii wa mtu mmoja.
20 Sheria ililetwa ili dhambi iongezeke. Lakini dhambi ili poongezeka, neema iliongezeka zaidi. 21 Kama vile ambavyo dhambi ilitawala kwa njia ya kifo, vivyo hivyo neema ya Mungu iweze kutawala kwa njia ya haki, ikileta uzima wa milele katika Yesu
Copyright © 1989 by Biblica