M’Cheyne Bible Reading Plan
Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 5,000
(Mt 14:13-21; Mk 6:30-44; Lk 9:10-17)
6 Baadaye, Yesu akavuka Ziwa Galilaya (ambalo pia linaitwa Ziwa Tiberia). 2 Umati mkubwa wa watu ukamfuata kwa sababu waliona ishara za miujiza alizofanya kwa kuponya wagonjwa. 3 Yesu akapanda mlimani na kukaa pale pamoja na wafuasi wake. 4 Siku hizo sherehe ya Pasaka ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.
5 Yesu akainua macho yake na kuuona umati wa watu ukija kwake. Akamwambia Filipo, “Tunaweza kununua wapi mikate ya kuwatosha watu hawa wote?” 6 Alimwuliza Filipo swali hili ili kumjaribu. Yesu alikwishajua kile alichopanga kufanya.
7 Filipo akajibu, “Wote tunapaswa kufanya kazi kwa mwezi mmoja ili kununua mikate ya kutosha na kumpa kila mmoja aliyepo angalau kipande kidogo.”
8 Mfuasi mwingine aliyekuwepo alikuwa Andrea, ndugu yake Simoni Petro. Andrea akasema, 9 “Yupo hapa kijana mwenye mikate mitano ya shayiri na samaki wadogo wawili. Lakini hiyo haitoshi kwa umati huu wa watu.”
10 Yesu akasema, “Mwambieni kila mtu akae chini.” Sehemu hiyo ilikuwa yenye nyasi nyingi, na wanaume wapatao 5,000 walikaa hapo. 11 Yesu akaichukua ile mikate akamshukuru Mungu kwa ajili ya hiyo. Kisha akawapa watu waliokuwa wakisubiri kula. Alifanya vivyo hivyo kwa samaki. Akawapa watu kadiri walivyohitaji.
12 Wote hao wakawa na chakula cha kutosha. Walipomaliza kula, Yesu akawaambia wafuasi wake, “Kusanyeni vipande vya samaki vilivyobaki na mikate ambayo haikuliwa. Msipoteze chochote.” 13 Hivyo wakakusanya vipande vilivyobaki wakajaza vikapu 12 vikubwa vya mikate ya ngano iliyowabakia wale waliokula. Watu walikuwa wameanza kula wakiwa na vipande vitano tu vya mikate ya ngano.
14 Watu waliiona ishara hii aliyoifanya Yesu na kusema, “Huyu atakuwa ndiye yule Nabii[a] anayekuja ulimwenguni!”
15 Yesu akajua kwamba watu walipanga kuja kumchukua na kumfanya kuwa mfalme wao baada ya kuona muujiza alioufanya. Hivyo akaondoka na kwenda milimani peke yake.
Yesu Atembea Juu ya Maji
(Mt 14:22-27; Mk 6:45-52)
16 Jioni ile wafuasi wake wakashuka kwenda ziwani. 17 Ilikuwa giza sasa, wakati huo Yesu hakuwa pamoja na wafuasi wake. Wakapanda kwenye mashua na kuanza safari kuvuka ziwa kwenda Kapernaumu. 18 Upepo ulikuwa unavuma kwa nguvu sana. Mawimbi ziwani yakawa makubwa. 19 Wakaiendesha mashua kiasi cha kilomita tano au sita. Kisha wakamwona Yesu. Yeye alikuwa anatembea juu ya maji, akiifuata mashua. Nao wakaogopa. 20 Lakini Yesu akawaambia, “Msiogope. Ni mimi.” 21 Baada ya kusema hivyo, wakamkaribisha kwenye mashua. Kisha mashua ikafika ufukweni katika sehemu waliyotaka kwenda.
Watu Wamtafuta Yesu
22 Siku iliyofuata watu wengi walikuwa wamekaa upande mwingine wa ziwa. Nao walijua kuwa Yesu hakwenda pamoja na wafuasi wake kwenye mashua. Kwani walifahamu kuwa wafuasi wake waliondoka na mashua peke yao. Walijua pia kuwa ile ilikuwa ni mashua pekee iliyokuwepo pale. 23 Lakini baadaye mashua zingine kutoka Tiberia zilifika na kusimama karibu na mahali walipokula chakula jana yake. Hapo ni mahali pale walipokula mikate baada ya Yesu kushukuru. 24 Watu wakaona kuwa Yesu na wafuasi wake hawakuwa hapo. Hivyo wakaingia katika mashua zao na kuelekea Kapernaumu kumtafuta Yesu.
Yesu, Mkate wa Uzima
25 Watu wakamwona Yesu akiwa upande mwingine wa ziwa. Wakamwuliza, “Mwalimu, ulifika huku lini?”
26 Akawajibu, “Kwa nini mnanitafuta? Ni kwa sababu mliona ishara na miujiza iliyotendeka? Ukweli ni kwamba, mnanitafuta kwa vile mlikula ile mikate mkashiba. 27 Lakini chakula cha kidunia kinaharibika na hakidumu. Ninyi msifanye kazi ili kupata chakula cha aina hiyo kinachoharibika. Isipokuwa fanyeni kazi ili mpate chakula kinachodumu na kinachowapa uzima wa milele. Mwana wa Adamu atawapa hicho chakula. Yeye ndiye pekee aliyethibitishwa na Mungu Baba kuwapa.”
28 Watu wakamwuliza Yesu, “Mungu anatutaka tufanye nini?”
29 Yesu akajibu, “Kazi anayoitaka Mungu muifanye ni hii: kumwamini yule aliyemtuma.”
30 Hivyo watu wakamwuliza, “Ni ishara gani utakayotufanyia? Ili nasi tutakapokuona unafanya ishara basi tukuamini? Je, utafanya nini? 31 Baba zetu walipewa mana kula jangwani. Kama Maandiko yanavyosema, ‘Aliwapa mkate wa kula kutoka mbinguni.’”(A)
32 Yesu akasema, “Naweza kuwahakikishia kwamba Musa siye aliyewapa watu wenu mkate kutoka mbinguni. Bali Baba yangu huwapa ninyi mkate halisi unaotoka mbinguni. 33 Mkate wa Mungu ni ule unaoshuka kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.”
34 Watu wakasema, “Bwana, kuanzia sasa na kuendelea tupe mkate wa aina hiyo.”
35 Kisha Yesu akasema, “Mimi ndiye mkate unaoleta uzima. Hakuna ajaye kwangu atakayehisi njaa. Hakuna anayeniamini atakayepata kiu kamwe. 36 Nilikwisha kuwaambia mapema kuwa mmeona kile ambacho naweza kufanya,[b] lakini bado hamuniamini. 37 Vyote anavyonipa Baba vitakuja kwangu hata hivyo yeyote Yule atakayekuja kwangu sitamkataa kabisa. Nami kwa hakika daima nitawapokea. 38 Nilishuka kutoka mbinguni kuja kufanya yale Mungu anayopenda, siyo ninayoyapenda mimi. 39 Nami sitampoteza hata mmoja wa wale alionipa Mungu. Bali nataka nimfufue katika siku ya mwisho. Haya ndiyo Baba yangu anayoyataka. 40 Kila anayemtazama Mwana na kumwamini anao uzima wa milele. Nami nitamfufua katika siku ya mwisho. Hayo ndiyo anayoyataka Baba yangu.”
41 Baadhi ya Wayahudi walianza kumlalamikia Yesu kwa vile alisema, “Mimi ni mkate unaoshuka kutoka mbinguni.” 42 Wakasema, “Huyu ni Yesu. Tunawajua baba na mama yake. Yeye ni mtoto wa Yusufu. Anawezaje kusema, ‘Nilishuka kutoka mbinguni’?”
43 Lakini Yesu akawaambia, “Acheni kunung'unika miongoni mwenu. 44 Baba ndiye aliyenituma, na ndiye anayewaleta watu kwangu. Nami nitawafufua siku ya mwisho. Hakuna mtu anayeweza kuja kwangu asipoletwa na Baba yangu. 45 Hii iliandikwa katika vitabu vya manabii: ‘Mungu atawafundisha wote.’(B) Watu humsikiliza Baba na hujifunza kutoka kwake. Hao ndiyo wanaokuja kwangu. 46 Sina maana kwamba yupo yeyote aliyemwona Baba. Yule pekee aliyekwisha kumwona Baba ni yule aliyetoka kwa Mungu. Huyo amemwona Baba.
47 Hakika nawaambieni kila anayeamini anao uzima wa milele. 48 Maana mimi ni mkate unaoleta uzima. 49 Baba zenu walikula mana waliyopewa na Mungu kule jangwani, lakini haikuwazuia kufa. 50 Hapa upo mkate unaotoka mbinguni. Yeyote anayekula mkate huu hatakufa kamwe. 51 Mimi ni mkate ulio hai ulioshuka kutoka mbinguni. Yeyote atakayeula mkate huu ataishi milele. Mkate huu ni mwili wangu. Nitautoa mwili wangu ili watu wa ulimwengu huu waweze kupata uzima.”
52 Kisha Wayahudi hawa wakaanza kubishana wao kwa wao. Wakasema, “Yawezekanaje mtu huyu akatupa mwili wake tuule?”
53 Yesu akasema, “Mniamini ninaposema kwamba mnapaswa kuula mwili wa Mwana wa Adamu, na mnapaswa kuinywa damu yake. Msipofanya hivyo, hamtakuwa na uzima wa kweli. 54 Wale wanaoula mwili wangu na kuinywa damu yangu wanao uzima wa milele. Nitawafufua siku ya mwisho. 55 Mwili wangu ni chakula halisi, na damu yangu ni kinywaji halisi. 56 Wale waulao[c] mwili wangu na kuinywa damu yangu wanaishi ndani yangu, nami naishi ndani yao.
57 Baba alinituma. Yeye anaishi, nami naishi kwa sababu yake. Hivyo kila anayenila mimi ataishi kwa sababu yangu. 58 Mimi siyo kama ule mkate walioula baba zenu. Wao waliula mkate huo, lakini bado walikufa baadaye. Mimi ni mkate uliotoka mbinguni. Yeyote atakayeula mkate huu ataishi milele.”
59 Yesu aliyasema haya yote alipokuwa akifundisha kwenye Sinagogi katika mji wa Kapernaumu.
Wafuasi Wengi Wamwacha Yesu
60 Wafuasi wa Yesu waliposikia haya, wengi wao wakasema, “Fundisho hili ni gumu sana. Nani awezaye kulipokea?”
61 Yesu alikwishatambua kuwa wafuasi wake walikuwa wanalalamika juu ya hili. Hivyo akasema, “Je, fundisho hili ni tatizo kwenu? 62 Ikiwa ni hivyo mtafikiri nini mtakapomwona Mwana wa Adamu akipanda kurudi kule alikotoka? 63 Roho ndiye anayeleta uzima. Sio mwili. Lakini maneno niliyowaambia yanatoka kwa Roho, hivyo yanaleta uzima.” 64 Lakini baadhi yenu hamuamini. (Yesu aliwafahamu wale ambao hawakuamini. Alijua haya tangu mwanzo. Na alimjua yule ambaye angemsaliti kwa adui zake.) 65 Yesu akasema, “Ndiyo maana nilisema, ‘Hayupo hata mmoja ambaye anaweza kuja kwangu pasipo kusaidiwa na baba.’”
66 Baada ya Yesu kusema mambo hayo, wafuasi wake wengi wakamkimbia na wakaacha kumfuata.
67 Yesu akawauliza wale mitume kumi na wawili, “Nanyi pia mnataka kuondoka?”
68 Simoni Petro akamjibu, “Bwana, tutaenda wapi? Wewe unayo maneno yanayoleta uzima wa milele. 69 Sisi tunakuamini wewe. Tunafahamu kwamba wewe ndiye Yule Mtakatifu atokaye kwa Mungu.”
70 Kisha Yesu akajibu, “Niliwachagua nyote kumi na wawili. Lakini mmoja wenu ni Ibilisi.” 71 Alikuwa anazungumza juu ya Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Yuda alikuwa miongoni mwa mitume kumi na wawili, lakini baadaye angemkabidhi Yesu kwa adui zake.
Mitume Wengine Wamkubali Paulo
2 Baada ya miaka 14 nilirudi tena Yerusalemu nikiwa na Barnaba na nilimchukua Tito pia. 2 Nilikwenda kule maana Mungu alinionyesha kuwa ninapaswa kwenda. Niliwafafanulia Habari Njema kama nilivyoihubiri kwa watu wasio Wayahudi. Pia nilikutana faragha na wale waliokuwa wanatazamiwa kuwa viongozi. Nilitaka niwe na uhakika kuwa tulikuwa tunapatana ili kazi yangu ya nyuma na ile niliyokuwa naifanya sasa zisipotee bure.
3 Tito, aliyekuwa pamoja nami ni Myunani. Hata hivyo viongozi hawa hawakulazimisha kumtahiri. 4 Tulihitaji kuyazungumzia matatizo haya, kwa sababu wale waliojifanya kuwa ni ndugu zetu walikuja kwenye kundi letu kwa siri. Waliingia kama wapelelezi kutafiti kuhusu uhuru tuliokuwa nao ndani ya Kristo Yesu. Walitaka watufanye sisi watumwa, 5 lakini hatukujiweka chini ya chochote ambacho hawa ndugu wa uongo walikitaka. Tulitaka ukweli wa Habari Njema ubaki ule ule na hatimaye uwafikie na ninyi.
6 Na watu wale ambao walihesabiwa kuwa viongozi muhimu hawakuongeza lolote katika ujumbe wa Habari Njema niliyowahubiria watu. (Haijalishi kwangu kuwa walikuwa wa “muhimu” au la. Kwa Mungu binadamu wote ni sawa.) 7 Lakini viongozi hawa waliona kuwa Mungu alinipa kazi maalumu ya kuhubiri Habari Njema kwa wasio Wayahudi, kama vile alivyomwagiza Petro[a] kufanya kazi hiyo hiyo ya kuhubiri Habari Njema miongoni mwa Wayahudi. 8 Mungu alimpa Petro uwezo wa kufanya kazi kama mtume lakini kwa walio Wayahudi. Mungu akanipa mimi pia uwezo wa kufanya kazi kama mtume, lakini kwa wasiokuwa Wayahudi. 9 Yakobo, Petro na Yohana walikuwa viongozi muhimu kanisani. Hawa wakaona kuwa Mungu alinipa kipaji hiki maalumu cha huduma, hivyo wakatupa mkono wa shirika mimi pamoja na Barnaba. Wakakubali kuwa sisi tutaendelea kufanya kazi miongoni mwao wasio Wayahudi, na wao wataendelea kufanya kazi miongoni mwao walio Wayahudi. 10 Wakatuomba jambo moja tu, ya kwamba tukumbuke kuwahudumia waaminio walio maskini.[b] Na kwa hakika hili lilikuwa jambo nililojitahidi kufanya.
Paulo Aonesha Kuwa Petro Alikosea Kule Antiokia
11 Petro alipokuja Antiokia, alifanya kitu ambacho hakikuwa sahihi. Nami nikampinga, kwa sababu hakika alikuwa na hatia mbele za Mungu. 12 Hivi ndivyo ilivyotokea: Petro alipokuja Antiokia, hapo awali kabla ya Wayahudi kufika, alikula na kujumuika na wasio Wayahudi. Lakini baada ya Wayahudi kufika kutoka kwa Yakobo, Petro akajitenga na wasio Wayahudi. Akaacha kula pamoja nao kwa sababu aliwaogopa Wayahudi. 13 Hivyo Petro akafanya kama mnafiki, na waamini wengine pale Antiokia wakaungana naye katika unafiki huo. Wakamfanya hata Barnaba naye kuwa mnafiki kama wao. 14 Hawakuwa wakiifuata kweli ya Habari Njema. Nilipoona hili, nilimweleza Petro mbele ya kila mtu. Nilisema, “Petro, wewe ni Myahudi, lakini huenendi kama Myahudi. Unaenenda kama mtu asiye Myahudi. Hivyo kwa nini unajaribu kuwalazimisha wale wasio Wayahudi kuenenda kama Wayahudi?
15 Sisi ni Wayahudi kwa kuzaliwa. Hatukuzaliwa tukiwa ‘watenda dhambi’, kama vile Wayahudi wanavyowaita wale wasio Wayahudi. 16 Lakini tunajua kuwa hakuna mtu anayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa kuifuata sheria. Ni kwa kuamini katika[c] Yesu Kristo ndiko kunamfanya mtu ahesabiwe haki mbele za Mungu. Hivyo hata nasi Wayahudi tumeiweka imani yetu katika Kristo Yesu, kwa sababu tulitaka kuhesabiwa haki mbele za Mungu. Na tumehesabiwa haki kwa imani[d] ya Yesu Kristo, siyo kwa sababu tuliifuata sheria. Naweza kusema hili kwa sababu hakuna anayeweza kuhesabiwa haki kwa kuifuata Sheria ya Musa.
17 Kwa hiyo tunaamini uhusiano wetu kwa Kristo utatufanya tuhesabiwe haki mbele za Mungu. Ikiwa hiyo inatufanya tuonekane kama ‘watenda dhambi’ wasio Wayahudi, je itakuwa na maana kuwa Kristo anasababisha dhambi kuongezeka. Kwa hakika sivyo? 18 Sheria ilijenga ukuta baina yetu Wayahudi na watu wengine wote, ukuta ambao nilijitahidi kuuvunja. Kweli nitakosea sana kuujenga tena ukuta huo. 19 Sheria yenyewe iliyafikisha mwisho maisha yangu chini ya sheria. Nikafa katika sheria hiyo na kuwa huru ili niweze kuishi kwa ajili ya Mungu. Nimepigiliwa misumari msalabani pamoja na Kristo. 20 Hivyo siyo mimi ninayeishi sasa; ni Kristo ndiye anayeishi ndani yangu. Bado naishi katika mwili wangu, lakini naishi kwa imani katika Mwana wa Mungu aliyenipenda na kujitoa mwenyewe kuniokoa mimi. 21 Si mimi ninayeikataa neema ya Mungu kama vile haina manufaa yoyote. Kwa sababu ikiwa kwa kuifuata sheria ndivyo watu wanahesabiwa haki mbele za Mungu, basi Kristo alikufa pasipo faida!”
© 2017 Bible League International