M’Cheyne Bible Reading Plan
Dhambi na Msamaha
(Mt 18:6-7,21-22; Mk 9:42)
17 Yesu akawaambia wafuasi wake, “Mambo yanayosababisha watu kutenda dhambi yatatokea hakika. Lakini ole wake mtu anayesababisha hili litokee. 2 Ingekuwa vizuri kwa mtu huyo kama jiwe la kusagia lingefungwa shingoni mwake, na akatupwa baharini, kuliko kusababisha mmojawapo wa wanyenyekevu hawa kutenda dhambi. 3 Hivyo iweni waangalifu!
Ikiwa ndugu au dada yako katika familia ya Mungu akikukosea, umwonye. Akitubu, msamehe. 4 Hata kama akikukosea mara saba katika siku moja, lakini akakuomba msamaha kila anapokukosea, msamehe.”
Imani Yako Ni Kubwa Kiasi Gani?
5 Kisha mitume wakamwambia Bwana, “Tuongezee imani.”
6 Bwana akasema, “Imani yenu ingekuwa kubwa kama mbegu ya haradali, mngeuambia mforosadi huu, ‘Ng'oka, ukajipandikize baharini,’ nao ungewatii.
Iweni Watumishi Wema
7 Chukulia mmoja wenu ana mtumishi ambaye amekuwa shambani akilima au akichunga kondoo shambani. Akirudi kutoka shambani au machungani, utamwambia nini? Je, utamwambia, ‘Njoo ndani, keti, ule chakula’? 8 Hapana! Utamwambia mtumishi wako, ‘Nitayarishie chakula nile. Jitayarishe na unihudumie. Nitakapomaliza kula na kunywa, ndipo utakula.’ 9 Mtumishi asipewe shukrani maalumu kwa kufanya kazi yake. Anafanya kile alichoagizwa na mkuu wake. 10 Vivyo hivyo nanyi. Mkimaliza kufanya yote mliyoamriwa kufanya, mseme, ‘Sisi ni watumwa, hatustahili shukrani yoyote maalumu. Tumefanya kazi tunayotakiwa kufanya.’”
Yesu Awaponya Baadhi ya Wayahudi na Msamaria
11 Yesu alikuwa anasafiri kwenda Yerusalemu. Alipotoka Galilaya alisafiri akipita kando ya mpaka wa Samaria. 12 Aliingia katika mji mdogo, na wanaume kumi walimwendea. Hawakumkaribia, kwa sababu wote walikuwa na ugonjwa mbaya sana wa ngozi. 13 Lakini watu wale wakaita kwa kupaza sauti wakisema, “Yesu! Mkuu! Tafadhali utusaidie!”
14 Yesu alipowaona, akasema, “Nendeni mkajioneshe kwa makuhani.”[a]
Wale watu kumi walipokuwa wanakwenda kujionesha kwa makuhani, waliponywa. 15 Mmoja wao alipoona kuwa amepona, alirudi kwa Yesu huku akimsifu Mungu kwa kupaza sauti. 16 Akaanguka kifudifudi miguuni pa Yesu, akamshukuru. (Alikuwa Msamaria.) 17 Yesu akasema, “Watu kumi wameponywa, wengine tisa wako wapi? 18 Mtu huyu wala si mmoja wa watu wetu. Ni yeye peke yake aliyerudi kumsifu Mungu?” 19 Ndipo Yesu akamwambia, “Inuka! Unaweza kwenda. Umeponywa kwa sababu uliamini.”
Kuja Kwa Ufalme Wa Mungu
(Mt 24:23-28,37-41)
20 Baadhi ya Mafarisayo walimuuliza Yesu, “Ufalme wa Mungu utakuja lini?” Yesu akajibu, “Kuja kwa ufalme wa Mungu si kitu unachoweza kuona. 21 Watu hawatasema, ‘Tazama ufalme wa Mungu uko hapa’ au ‘Ule pale!’ Hapana, Ufalme wa Mungu upo hapa pamoja nanyi.”[b]
22 Kisha Yesu akawaambia wafuasi wake, “Wakati utakuja, ambapo mtatamani angalau kuwa na Mwana wa Adamu hata kwa siku moja, lakini hamtaweza. 23 Watu watawaambia, ‘Tazameni, yuko kule!’ au ‘Tazameni, yuko hapa!’ Kaeni pale mlipo; msitoke kwenda kumtafuta. 24 Iweni na subira kwa sababu Mwana wa Adamu atakaporudi, mtatambua. Siku hiyo atang'aa kama mwanga wa radi umulikavyo angani kutoka upande mmoja hadi mwingine. 25 Lakini kwanza, ni lazima Mwana wa Adamu ateseke kwa mambo mengi na watu wa leo watamkataa.
26 Mwana wa Adamu atakaporudi, itakuwa kama ilivyokuwa Nuhu alipoishi. 27 Watu walikuwa wakila, wakinywa, wakioa na kuolewa hata siku Nuhu alipoingia katika safina. Ndipo gharika ilikuja na kuwaangamiza wote.
28 Ilikuwa vivyo hivyo katika wakati wa Lutu, Mungu alipoteketeza Sodoma. Watu wa Sodoma walikuwa wakila, wakinywa, wakinunua, wakiuza, wakipanda na kujijengea nyumba. 29 Lakini siku ambayo Lutu alitoka Sodoma, moto na baruti vilinyesha kutoka mbinguni na kuwaua wote. 30 Hivi ndivyo itakavyokuwa siku ambayo Mwana wa Adamu atarudi.
31 Siku hiyo, ikiwa mtu atakuwa juu ya paa ya nyumba yake, hatakuwa na muda wa kushuka kwenda ndani ya nyumba kuchukua vitu vyake. Ikiwa atakuwa shambani, hataweza kurudi nyumbani. 32 Kumbukeni yaliyompata mke wa Lutu![c]
33 Kila atakayejaribu kutunza maisha aliyonayo atayaangamiza. Lakini yeyote atakayeyasalimisha maisha yake atayaokoa. 34 Usiku ule watu wawili wataweza kuwa wamelala katika chumba kimoja, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. 35 Wanawake wawili watakuwa wanasaga nafaka pamoja, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.” 36 [d]
37 Wafuasi wake wakamuuliza, “Hii itakuwa wapi Bwana?”
Yesu akajibu, “Ni kama kuutafuta mzoga, utaupata pale ambapo tai wamekusanyika.”
2 Hivyo niliamua moyoni mwangu mwenyewe kuwa sitafanya safari nyingine ya huzuni kuja kwenu. 2 Ikiwa nitawafanya muwe na huzuni nani atanifanya niwe na furaha? Ni ninyi tu ndiyo mnaweza kunifanya niwe na furaha. Ni ninyi ambao niliwahuzunisha. 3 Naliwaandikia barua ili kwamba nijapo kwenu nisihuzunishwe na wale ambao wanapaswa kunifanya niwe na furaha. Nilijisikia kuwa na hakika ya kuwa ninyi nyote mtashiriki furaha yangu. 4 Nilipowaandikia barua ya kwanza, niliiandika macho yangu yakibubujika machozi mengi. Sikuandika ili kuwafanya muwe na huzuni, bali kuwafanya mjue kwa jinsi gani ninavyowapenda.
Msamehe Mtu Aliye Fanya Kosa
5 Mtu mmoja katika kusanyiko lenu amesababisha maumivu, ila si kwangu, bali amesababisha maumivu kwenu nyote kwa kiwango fulani. Nina maanisha amewakwaza nyote kwa namna fulani. (Sitaki ionekane kuwa mbaya sana kuliko ilivyo) 6 Adhabu ambayo walio wengi miongoni mwa kusanyiko lenu walimpa inatosha. 7 Lakini msameheni na kumtia moyo sasa. Hili litamsaidia asiwe na huzuni sana na asikate tamaa kabisa. 8 Hivyo ninawasihi mwonesheni kuwa mnampenda. 9 Hii ndiyo sababu niliandika ile barua. Nilitaka kuwapima na kuona ikiwa mna utii katika kila kitu. 10 Mkimsamehe mtu, ndipo nami husamehe pia. Na kile nilichosamehe, kama nilikuwa na jambo la kusamehe, nilisamehe kwa ajili yenu. Na Kristo akithibitisha. 11 Nilifanya hivi ili Shetani asipate ushindi wowote kutoka kwetu. Tunafahamu sote mipango yake ilivyo.
Mungu Anatupa Ushindi Dhidi ya Masumbufu
12 Nilikwenda Troa kuwaambia watu Habari Njema juu ya Kristo. Bwana alinipa fursa ya pekee kule. 13 Lakini sikuwa na amani kwa sababu sikumwona Tito pale. Hivyo niliaga na kwenda Makedonia.
14 Lakini ashukuriwe Mungu ambaye siku zote hutuongoza katika gwaride la ushindi la Kristo. Mungu anatutumia sisi kueneza ufahamu juu ya Kristo kila mahali kama vile marashi yanayonukia vizuri. 15 Maisha yetu ni sadaka ya harufu nzuri ya manukato ya Kristo inayotolewa kwa Mungu. Harufu nzuri ya sadaka hii huwaendea wale wanaokolewa na kwa wale wanaopotea. 16 Kwao wanaopotea, marashi haya yananukia kama mauti, na huwaletea kifo. Ila kwao wanaookolewa, ina harufu nzuri ya uzima, na inawaletea afya ya uzima. Kwa hiyo ni nani aliye bora kuifanya kazi hii? 17 Kwa hakika sio wale wanaozunguka wakiuuza ujumbe wa Mungu ili kupata faida! Lakini sisi hatufanyi hivyo. Kwa msaada wa Kristo tunaisema kweli ya Mungu kwa uaminifu, tukifahamu kuwa tunazungumza kwa ajili yake na mbele zake.
© 2017 Bible League International