Historical
Paulo Asimama Mbele ya Mfalme Agripa
26 Agripa[a] akamwambia Paulo, “Unaweza sasa kujitetea wewe mwenyewe.” Paulo akanyoosha mkono wake ili wamsikilize kwa makini na akaanza kusema. 2 “Mfalme Agripa, najisikia heshima kusimama hapa mbele yako leo ili nijibu mashitaka yote yaliyotengenezwa na Wayahudi dhidi yangu. 3 Ninafurahi kuzungumza nawe, kwa sababu unafahamu sana kuhusu desturi za Kiyahudi na mambo ambayo Wayahudi hubishana. Tafadhali uwe mvumilifu kunisikiliza.
4 Wayahudi wote wanafahamu maisha yangu yote. Wanafahamu namna nilivyoishi tangu mwanzo miongoni mwa watu mwangu na baadaye Yerusalemu. 5 Wayahudi hawa wamenifahamu kwa muda mrefu. Wakitaka wanaweza kukwambia kwamba nilikuwa Farisayo mzuri. Na Mafarisayo wanazitii sheria za dini ya Kiyahudi kwa uangalifu kuliko kundi lolote. 6 Na sasa nimeshitakiwa kwa sababu ninatumaini ahadi ambayo Mungu aliiweka kwa baba zetu. 7 Hii ni ahadi ambayo makabila yote kumi na mbili ya watu wetu yanatumaini kuipokea. Kwa sababu ya tumaini hili Wayahudi wanamtumikia Mungu usiku na mchana. Ee Mfalme wangu, Wayahudi wamenishitaki kwa sababu ninatumaini ahadi hii hii. 8 Kwa nini ninyi watu mnadhani Mungu hawezi kuwafufua watu kutoka kwa wafu?
9 Huko nyuma nilidhani kuwa ninapaswa kufanya kinyume na Yesu kutoka Nazareti kwa kadri ninavyoweza. 10 Na ndivyo nilivyofanya, kuanzia Yerusalemu. Viongozi wa makuhani walinipa mamlaka ya kuwaweka gerezani watu wa Mungu wengi. Na walipokuwa wanauawa nilikubali kuwa lilikuwa jambo zuri. 11 Nilikwenda katika masinagogi yote na kuwaadhibu, nikijaribu kuwafanya wamlaani[b] Yesu. Hasira yangu dhidi ya watu hawa ilikuwa kali sana kiasi kwamba nilikwenda katika miji mingine kuwatafuta na kuwaadhibu.
Paulo Aeleza Alivyomwona Yesu
12 Wakati fulani viongozi wa makuhani walinipa ruhusa na mamlaka kwenda katika mji wa Dameski. 13 Nikiwa njiani, mchana, niliona mwanga kutoka mbinguni, unaong'aa kuliko jua. Uling'aa kunizunguka mimi pamoja na wale waliokuwa wanasafiri pamoja nami. 14 Sote tulianguka chini. Kisha nilisikia sauti iliyozungumza nami kwa Kiaramu. Sauti ilisema, ‘Sauli, Sauli, kwa nini unanitesa? Unajiumiza wewe mwenyewe kwa kunipinga mimi.’
15 Nilisema, ‘Wewe ni nani, Bwana?’
Bwana alisema, ‘Mimi ni Yesu. Unayemtesa. 16 Simama! Nimekuchagua wewe kuwa mtumishi wangu. Utawaambia watu habari zangu, ulichoona leo na yale nitakayokuonesha. Hii ndiyo sababu nimekuja kwako. 17 Nitakulinda dhidi ya watu wako na dhidi ya watu wasio Wayahudi, ninaokutuma kwao. 18 Utawafanya waielewe kweli. Watatoka gizani na kuja kwenye mwanga. Watageuka kutoka kwenye mamlaka ya Shetani na kumgeukia Mungu. Ndipo dhambi zao zitasamehewa, na wataweza kupewa nafasi miongoni mwa watu wa Mungu, walifanywa watakatifu kwa kuniamini.’”
Paulo Aeleza Kuhusu Kazi Yake
19 Paulo aliendelea kusema: “Mfalme Agripa, baada ya kuona maono haya kutoka mbinguni, nilitii. 20 Nilianza kuwaambia watu kubadili mioyo na maisha yao na kumgeukia Mungu. Niliwaambia kufanya yale yatakayoonyesha kwamba hakika wamebadilika. Kwanza nilikwenda kwa watu waliokuwa Dameski. Kisha nikaenda Yerusalemu na kila sehemu ya Uyahudi na nikawaambia watu huko. Nilikwenda pia kwa watu wasio Wayahudi.
21 Hii ndiyo sababu Wayahudi walinikamata na kujaribu kuniua Hekaluni. 22 Lakini Mungu alinisaidia, na bado ananisaidia leo. Kwa msaada wa Mungu nimesimama hapa leo na kuwaambia watu kile nilichokiona. Lakini sisemi chochote kipya. Ninasema kile ambacho Musa na manabii walisema kingetokea. 23 Walisema kwamba Masihi atakufa na kuwa wa kwanza kufufuka kutoka kwa wafu. Walisema kwamba ataleta mwanga wa kweli[c] ya Mungu inayowaokoa wote, Wayahudi na wasio Wayahudi.”
Paulo Ajaribu Kumshawishi Agripa
24 Paulo alipokuwa bado anajitetea, Festo alipaza sauti akasema, “Paulo, umerukwa na akili! Kusoma kwingi kumekufanya kichaa.” 25 Paulo akasema, “Mheshimiwa Festo, mimi si kichaa. Ninachokisema ni kweli na kinaingia akilini. 26 Mfalme Agripa analifahamu hili, na ninaweza kuzungumza naye kwa uhuru. Ninafahamu kwamba amekwisha kusikia kuhusu mambo haya, yalitokea mahali ambako kila mtu aliyaona. 27 Mfalme Agripa, unaamini yale ambayo manabii waliandika? Ninajua unaamini!”
28 Mfalme Agripa akamwambia Paulo, “Unadhani unaweza kunishawishi kirahisi kiasi hicho ili niwe Mkristo?”
29 Paulo akasema, “Haijalishi kwangu, ikiwa ni vigumu au rahisi. Ninaomba tu kwa Mungu kwamba si wewe peke yako lakini kila mtu anayenisikiliza leo angeokolewa ili awe kama mimi, isipokuwa kwa minyororo hii!”
30 Mfalme Agripa, Gavana Festo, Bernike, na watu wote waliokaa pamoja nao wakasimama 31 na kuondoka chumbani. Walikuwa wanaongea wenyewe. Walisema, “Mtu huyu hajafanya chochote kinachostahili kuuawa au kuwekwa gerezani.” 32 Kisha Agripa akamwambia Festo, “Tungemwachia huru, lakini ameomba kumwona Kaisari.”
Paulo Aenda Rumi
27 Iliamriwa kwamba tutakwenda Italia. Ofisa wa Jeshi aliyeitwa Yulio, aliyetumika katika jeshi maalumu la mfalme mkuu, aliwekwa kuwa kiongozi wa kumlinda Paulo na baadhi ya wafungwa wengine safarini. 2 Tuliingia kwenye meli katika mji wa Adramatio. Meli hiyo ilikuwa inasafiri kupitia sehemu mbalimbali za Asia. Aristarko, mtu Thesalonike katika makedonia alisafiri pamoja nasi.
3 Siku iliyofuata tulifika kwenye mji wa Sidoni. Yulio alikuwa mwema sana kwa Paulo na akampa uhuru wa kwenda kuwatembelea rafiki zake pale, walimpa chochote alichohitaji. 4 Tuliondoka katika mji ule na tukatweka tanga tukasafiri karibu na kisiwa cha Kipro kwa sababu upepo ulikuwa unavuma kinyume nasi. 5 Tulikwenda kwa kukatisha bahari upande wa Kilikia na Pamfilia. Kisha tukafika katika mji wa Mira katika jimbo la Likia. 6 Tulipofika hapo ofisa wa jeshi akapata meli iliyotoka katika mji wa Iskanderia iliyokuwa inakwenda Italia. Akatupandisha humo.
7 Tulitweka tanga na kusafiri taratibu kwa siku nyingi. Ilikuwa vigumu kwetu kufika katika mji wa Nido kwa sababu upepo ulikuwa unavuma kinyume chetu. Hatukuweza kuendelea zaidi kwa kupitia njia hiyo, hivyo tulitweka tanga tukasafiri kupitia upande wa kusini mwa kisiwa cha Krete karibu na Salmone. 8 Tulisafiri sambamba na pwani, lakini kwa shida. Ndipo tukafika mahali palipoitwa Bandari Salama, karibu na mji wa Lasea.
9 Tulikuwa tumepoteza muda mwingi, na ilikuwa hatari kutweka tanga, kwa sababu tayari ilikuwa baada ya siku ya Kiyahudi ya kufunga.[d] Hivyo Paulo aliwaonya akasema, 10 “Ndugu zangu, ninaona kuwa kutakuwa shida nyingi katika safari hii. Meli, kila kitu ndani yake na pia hata maisha yetu yanaweza kupotea!” 11 Lakini nahodha na mmiliki wa meli hawakukubaliana na Paulo. Hivyo ofisa wa jeshi alikubali walichokisema badala ya kumwamini Paulo. 12 Pia, bandari ile haikuwa mahali pazuri kwa meli kukaa majira ya baridi, hivyo watu karibu wote wakaamua kwamba ni lazima tuondoke pale. Walitegemea kuwa tungeweza kufika Foeniki, ambako meli ingekaa majira ya baridi. Foeniki ulikuwa mji katika kisiwa cha Krete. Ulikuwa na bandari iliyotazama Kusini-Magharibi na Kaskazini-Magharibi.
Dhoruba
13 Ndipo upepo mzuri ukaanza kuvuma kutoka kusini. Watu ndani ya meli wakafikiri, “Huu ndio upepo tulioutaka, na sasa tumeupata!” Hivyo wakavuta nanga. Tulitweka tanga tukasafiri karibu na kisiwa cha Krete. 14 Lakini upepo wenye nguvu unaoitwa “Kaskazini-Mashariki” ulikuja kwa kukikatisha kisiwa. 15 Upepo huu uliichukua meli na kuisukumia mbali. Meli haikuweza kwenda kinyume na upepo, hivyo tulisimama tukijaribu kuuacha upepo utusukume.
16 Tulikwenda upande wa chini wa kisiwa kidogo kilichoitwa Kauda. Kisiwa kikatukinga dhidi ya upepo, tulichukua mtumbwi wa kuokolea watu, lakini ilikuwa vigumu sana kufanya hivyo. 17 Baada ya watu kuleta mtumbwi wa kuokolea, wakaifunga meli kamba kuizungushia ili iendelee kushikamana isipasuke. Waliogopa kwamba meli ingekwama kwenye mchanga wa pwani ya Sirti.[e] Hivyo walishusha tanga na kuiacha meli ichukuliwe na upepo.
18 Siku iliyofuata upepo ulivuma kinyume nasi kwa nguvu kiasi kwamba watu walitupa baadhi ya vitu kutoka katika shehena ya meli.[f] 19 Siku moja baadaye wakatupa vifaa vya meli. 20 Kwa siku nyingi hatukuweza kuliona jua au nyota. Dhoruba ilikuwa mbaya sana. Tulipoteza matumaini yote ya kuendelea kuwa hai, tulidhani tutakufa.
21 Watu hawakula kwa muda mrefu. Ndipo siku moja Paulo akasimama mbele yao na kusema, “Ndugu zangu, niliwaambia tusiondoke Krete. Mngenisikiliza msingepata tatizo hili na hasara hii. 22 Lakini sasa ninawaambia iweni na furaha. Hakuna hata mmoja wenu atakayekufa, lakini meli itapotea. 23 Usiku uliopita malaika kutoka kwa Mungu ninayemwabudu na ambaye mimi ni wake. 24 Aliniambia, ‘Paulo, usiogope! Ni lazima utasimama mbele ya Kaisari. Mungu amekupa ahadi hii: Ataokoa maisha ya wote wanaosafiri pamoja nawe.’ 25 Hivyo ndugu, msihofu kitu chochote. Ninamwamini Mungu, na nina uhakika kila kitu kitatokea kama malaika wake alivyoniambia. 26 Lakini tutajigonga kwenye kisiwa.”
27 Usiku wa kumi na nne tulikuwa bado tunasukumwa na upepo katika bahari ya Adriatiki. Mabaharia wakadhani tulikuwa karibu na nchi kavu. 28 Wakatupa kamba iliyofungwa kitu kizito kwenye ncha yake. Wakakuta kwamba kina cha maji ni futi mia moja na ishirini.[g] Wakaendelea mbele kidogo na kutupa kamba tena. Kina kilikuwa futi tisini.[h] 29 Mabaharia waliogopa kwa kudhani kwamba tungegonga miamba, hivyo wakatupa nanga nne kwenye maji. Kisha wakaomba mchana ufike. 30 Baadhi ya mabaharia walitaka kuiacha meli, waliishusha majini mtumbwi wa kuokolea. Walitaka watu wengine wadhani kuwa walikuwa wanatupa nanga upande wa mbele wa meli. 31 Lakini Paulo alimwambia ofisa wa jeshi na askari wengine, “Iwapo watu hawa hawatakaa ndani ya meli, mtapoteza matumaini yote ya kupona.” 32 Hivyo askari wakakata kamba na kuuacha mtumbwi uanguke majini.
33 Kabla ya kupambazuka Paulo alianza kuwashawishi watu wote kula. Alisema, “Kwa wiki mbili mmekuwa mnasubiri na kuangalia, hamjala kwa siku kumi na nne. 34 Sasa ninawasihi mle chakula, mnakihitaji ili kuishi. Hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza hata unywele mmoja kutoka kwenye kichwa chake.” 35 Baada ya kusema hili, Paulo alichukua baadhi ya mikate akamshukuru Mungu kwa ajili ya mikate hiyo mbele yao wote. Akakata kipande na kuanza kula. 36 Watu wote wakafarijika na kuanza kula pia. 37 (Walikuwemo watu mia mbili sabini na sita ndani ya meli.) 38 Tulikula kila tulichohitaji. Kisha tukaanza kumwaga nafaka baharini ili meli iwe nyepesi.
Meli Yaharibiwa
39 Mchana ulipofika, mabaharia waliiona nchi kavu, lakini hawakupafahamu mahali pale. Waliona ghuba yenye ufukwe na walitaka kuipeleka meli ufukweni ikiwa wangeweza. 40 Hivyo walikata kamba kwenye nanga na kuziacha nanga ndani ya bahari. Wakati huo huo walifungua kamba zilizokuwa zinaushikilia usukani. Kisha wakanyanyua tanga la mbele na kutweka tanga kuelekea ufukweni. 41 Lakini meli uligonga mwamba wa michanga. Sehemu ya mbele ya meli ilikwama pale na haikuweza kutoka. Kisha mawimbi makubwa yakaanza kuvunja sehemu ya nyuma ya meli vipande vipande.
42 Askari waliamua kuwaua wafungwa ili asiwepo mfungwa hata mmoja atakayeogelea na kutoroka. 43 Lakini Yulio, ofisa wa jeshi alitaka Paulo asiuawe. Hivyo hakuwaruhusu askari kuwaua wafunga. Aliwaambia watu wanaoweza kuogelea, waruke majini kwenda nchi kavu. 44 Wengine walitumia mbao au vipande vya meli. Hivi ndivyo ambavyo watu wote walifika nchi kavu wakiwa salama.
Paulo Katika Kisiwa cha Malta
28 Tulipokuwa salama nchi kavu, tukatambua kuwa kisiwa kile kinaitwa Malta. 2 Watu walioishi pale walikuwa wema sana kwetu. Mvua ilikuwa inanyesha na kulikuwa baridi sana, hivyo walitengeneza moto na kutukaribisha sote. 3 Paulo alikusanya kuni nyingi kwa ajili ya moto. Alipokuwa akiweka kuni kwenye moto, nyoka mwenye sumu kali akajitokeza kwa sababu ya joto na kumuuma kwenye mkono. 4 Wenyeji wa kisiwa kile walipomwona nyoka ananing'inia kwenye mkono wa Paulo, walisema, “Mtu huyu lazima ni mwuaji! Hakufa baharini, lakini Haki[i] hataki aishi.”
5 Lakini Paulo alimku'ngutia nyoka kwenye moto na hakudhurika. 6 Watu wakadhani atavimba au ataanguka na kufa. Walisubiri na kumwangalia kwa muda mrefu, lakini hakuna kibaya kilichomtokea. Hivyo wakabadili mawazo yao. Wakasema, “Paulo ni mungu!”
7 Yalikuwepo mashamba kuzunguka eneo lile. Yaliyomilikiwa na ofisa wa juu sana wa Rumi katika kisiwa hicho aliyeitwa Pablio. Alitukaribisha nyumbani kwake na alikuwa mwema sana kwetu. Tulikaa nyumbani kwake kwa siku tatu. 8 Baba yake Pablio alikuwa mgonjwa sana. Alikuwa na homa na alikuwa anaharisha damu, lakini Paulo alikwenda kwake na kumuombea. Aliweka mikono juu yake naye akapona. 9 Baada ya hili kutokea, wagonjwa wengine wote kisiwani walikuja kwa Paulo, naye aliwaombea na wakaponywa pia.
10-11 Watu katika kisiwa hiki walituheshimu sana. Na baada ya kuwa pale kwa miezi mitatu, tukawa tayari kuondoka, walitupa kila kitu tulichohitaji kwa ajili ya safari yetu.
Paulo Aenda Rumi
Tulipanda meli iliyotoka Iskanderia iliyokaa katika kisiwa cha Malta wakati majira ya baridi. Mbele ya meli kulikuwa alama ya miungu pacha.[j] 12 Tulisimama katika mji wa Sirakuse. Tulikaa pale kwa siku tatu kisha tukaondoka. 13 Tulifika katika mji wa Regio. Siku iliyofuata upepo ulianza kuvuma kutokea Kusini-Magharibi, hivyo tuliweza kuondoka. Baada ya siku moja tukafika katika mji wa Puteoli. 14 Tuliwapata baadhi ya waamini pale, walituomba tukae nao kwa wiki moja. Mwishowe tulifika Rumi. 15 Ndugu na dada waliokaa Rumi walisikia habari zetu, walikuja kutupokea kwenye Soko la Apio[k] na kwenye Migahawa Mitatu.[l] Paulo alipowaona waamini hawa, alimshukuru Mungu na alifarijika.
Paulo Akiwa Rumi
16 Tulipofika Rumi, Paulo aliruhisiwa kuishi peke yake. Lakini askari alikaa pamoja naye kumlinda.
17 Siku tatu baadaye Paulo aliagiza baadhi ya Wayahudi muhimu waje kwake. Walipokusanyika, akasema, “Ndugu zangu, sijafanya lolote kinyume na watu wetu au kinyume na desturi za baba zetu. Lakini nilikamatwa Yerusalemu na kukabidhiwa kwa Warumi. 18 Waliniuliza maswali mengi, lakini hawakupata sababu yoyote kwa nini niuawe. Hivyo walitaka kuniachia huru. 19 Lakini Wayahudi kule hawakutaka hilo. Hivyo ilinibidi niombe kuja Rumi kuweka mashitaka yangu mbele ya Kaisari. Kwa kufanya hivi haimaanishi kuwa ninawashutumu watu wangu kwa kufanya chochote kibaya. 20 Ndiyo sababu nilitaka kuonana na kuzungumza nanyi. Nimefungwa kwa minyororo hii kwa sababu ninaamini katika tumaini la Israeli.”
21 Wayahudi walimjibu Paulo, “Hakuna barua tuliyoipokea kutoka Uyahudi kuhusu wewe. Hakuna ndugu yetu yeyote Myahudi aliyesafiri kutoka huko aliyeleta habari zako au kutwambia chochote kibaya juu yako. 22 Tunataka kusikia mawazo yako. Tunafahamu kuwa watu kila mahali wanapinga kundi hili jipya.”
23 Paulo na Wayahudi walichagua siku kwa ajili ya mkutano. Siku hiyo Wayahudi wengi walikutana na Paulo katika nyumba yake. Aliwaambia kwa siku nzima, akawafafanulia kuhusu ufalme wa Mungu. Alitumia Sheria ya Musa na maandishi ya manabii kuwashawishi kumwamini Yesu. 24 Baadhi ya Wayahudi waliamini alichosema, lakini wengine hawakuamini. 25 Walibishana wao wenyewe na wakaanza kuondoka. Lakini aliwaambia kitu kimoja zaidi: “Roho Mtakatifu aliwaambia ukweli baba zenu kupitia nabii Isaya, aliposema,
26 ‘Nenda kwa watu hawa na uwaambie:
Mtasikiliza na kusikiliza,
lakini hamtaelewa.
Mtatazama na kutazama,
lakini hakika hamtaona.
27 Watu hawa hawawezi kuelewa.
Masikio yao yamezibwa.
Na macho yao yamefumbwa.
Hivyo hawawezi kuona kwa macho yao,
au kusikia kwa masikio yao;
au kuelewa kwa akili zao;
au kuelewa kwa akili zao.
Ikiwa wangeelewa, wangeweza kunirudia,
na ningewaponya.’(A)
28 Ninataka ninyi Wayahudi mjue kuwa Mungu ameupeleka wokovu wake kwa watu wasio Wayahudi. Watasikia!” 29 [m]
30 Paulo alikaa katika nyumba yake mwenyewe aliyopanga kwa miaka miwili kamili. Aliwakaribisha watu wote waliokuja kumtembelea. 31 Aliwaambia kuhusu ufalme wa Mungu na kuwafundisha kuhusu Bwana Yesu Kristo. Alikuwa na ujasiri sana, na hakuna aliyejaribu kumzuia asizungumze.
© 2017 Bible League International