Historical
23 Paulo aliwatazama wajumbe wa baraza na kusema, “Ndugu zangu, Nimeishi maisha yangu katika njia nzuri mbele za Mungu. Daima nimefanya yale niliyodhani ni haki.” 2 Anania,[a] kuhani mkuu alikuwa pale. Aliposikia hili, aliwaambia watu waliokuwa wamesisima karibu na Paulo wampige kwenye mdomo. 3 Paulo akamwambia Anania, “Mungu atakupiga wewe pia! Wewe ni kama ukuta mchafu uliopakwa rangi nyeupe. Umeketi hapa na kunihukumu, ukitumia Sheria ya Musa. Lakini unawaambia wanipige wakati ni kinyume cha sheria.”
4 Watu waliokuwa wamesimama karibu na Paulo wakamwambia, “Una uhakika unataka kumtukana kuhani mkuu wa Mungu namna hiyo?”
5 Paulo akasema, “Ndugu zangu, sikufahamu kuwa mtu huyu ni kuhani mkuu. Maandiko yanasema, ‘Usiseme mambo mabaya kuhusu kiongozi wa watu wako.’”(A)
6 Paulo alijua kuwa baadhi ya watu kwenye baraza lile ni Masadukayo na baadhi yao ni Mafarisayo. Hivyo akapaza sauti akasema, “Ndugu zangu, Mimi ni Farisayo na baba yangu ni Farisayo! Nimeshitakiwa hapa kwa sababu ninaamini kuwa watu watafufuka kutoka kwa wafu.”
7 Paulo alipolisema hili, mabishano makubwa yakaanza kati ya Mafarisayo na Masadukayo. Baraza likagawanyika. 8 (Masadukayo hawaamini katika ufufuo, malaika au roho. Lakini Mafarisayo wanaamini vyote.) 9 Wayahudi hawa wote wakaanza kubishana kwa kupaza sauti. Baadhi ya walimu wa sheria, waliokuwa Mafarisayo wakasimama na kusema, “Hatuoni kosa lolote kwa mtu huyu. Inawezekana kwa hakika malaika au roho alizungumza naye.”
10 Mabishano yaligeuka kuwa mapigano na kamanda aliogopa kwamba Wayahudi wangempasua Paulo vipande vipande. Hivyo akawaambia askari wateremke, wamwondoe Paulo na kumweka mbali na Wayahudi hao katika jengo la jeshi.
11 Usiku uliofuata Bwana Yesu akaja na kusimama pembeni mwa Paulo. Akamwambia, “Uwe jasiri! Umewaambia watu kuhusu mimi humu Yerusalemu. Ni lazima ufanye vivyo hivyo Rumi.”
Baadhi ya Wayahudi Wapanga Kumwua Paulo
12 Asubuhi iliyofuata baadhi ya Wayahudi walifanya mpango wa kumwua Paulo. Walijiapiza kuwa hawatakula wala kunywa kitu chochote mpaka watakapomwua Paulo. 13 Walikuwa watu zaidi ya 40 waliofanya mpango huu. 14 Walikwenda wakaongea na viongozi wa makuhani na viongozi wa wazee wa Wayahudi. Walisema, “Tumejiwekea nadhiri kwamba hatutakula wala kunywa mpaka tumemwua Paulo. 15 Tunataka mfanye hivi: Mtumieni kamanda ujumbe kutoka kwenu na baraza kuu. Mwambieni mnamtaka amlete Paulo kwenu. Semeni kwamba mnataka kumwuliza maswali zaidi, tutamwua akiwa njiani kuja hapa.”
16 Lakini mpwaye Paulo aliusikia mpango huu. Alikwenda kwenye jengo la jeshi na kumwambia Paulo. 17 Kisha Paulo akamwita mmoja wa maofisa wa jeshi na kumwambia, “Mchukue huyu kijana kwa kamanda. Ana ujumbe kwa ajili yake.” 18 Hivyo ofisa wa jeshi akampeleka mpwaye Paulo kwa kamanda. Ofisa wa jeshi akasema, “Mfungwa Paulo ameniomba nimlete kijana huyu kwako. Ana kitu cha kukueleza.”
19 Kamanda akamchukua kijana na kwenda naye mahali ambapo wangekuwa peke yao. Kamanda akamwuliza, “Unataka kuniambia nini?”
20 Kijana akasema, “Baadhi ya Wayahudi wameamua kukuomba umpeleke Paulo kwenye mkutano wa baraza lao kesho. Wanataka wewe udhani kuwa wamepanga kumwuliza Paulo maswali zaidi. 21 Lakini usiwaamini! Zaidi ya watu 40 miongoni mwao wamejificha na wanasubiri kumwua. Wote wameweka nadhiri kuwa hawatakula wala kunywa mpaka wamemwua Paulo. Sasa hivi wanasubiri wewe ukubali.”
22 Kamanda akamtoa kijana, akamwambia, “Usimwambie yeyote kuwa umeniambia kuhusu mpango wao.”
Paulo Apelekwa Kaisaria
23 Ndipo Kamanda akawaita maofisa wawili wa jeshi. Akawaambia, “Ninataka baadhi ya watu kwenda Kaisaria. Andaeni askari mia mbili. Pia andaeni askari sabini waendao kwa farasi na mia mbili wa kubeba mikuki. Iweni tayari kuondoka saa tatu usiku. 24 Andaeni baadhi ya farasi kwa ajili ya Paulo kuendesha ili aweze kupelekwa kwa Gavana Feliki salama.” 25 Kamanda aliandika barua kuhusu Paulo. Hivi ndivyo alivyosema:
26 Kutoka kwa Klaudio Lisiasi.
Kwenda kwa Mheshimiwa Gavana Feliki.
Salamu:
27 Baadhi ya Wayahudi walimkamata mtu huyu na walikuwa karibu ya kumwua. Lakini nilipogundua kuwa ni raia wa Rumi, nilikwenda pamoja na askari wangu tukamwokoa. 28 Nilitaka kufahamu kwa nini walikuwa wanamshitaki. Hivyo nikampeleka kwenye mkutano wa baraza lao. 29 Hivi ndivyo nilivyoona: Wayahudi walisema mtu huyu alifanya mambo mabaya. Lakini mashitaka haya yalihusu sheria zao za Kiyahudi, na hakukuwa kosa lolote linaloweza kusababisha kufungwa au kifo. 30 Nimeambiwa kuwa baadhi ya Wayahudi walikuwa wanafanya mpango wa kumwua. Hivyo nimeamua kumleta kwako. Pia nimewaambia Wayahudi hao wakwambie walichonacho dhidi yake.
31 Askari walifanya kile walichoambiwa. Walimchukua Paulo na kumpeleka kwenye mji wa Antipatri usiku ule. 32 Siku iliyofuata askari wa farasi walikwenda na Paulo mpaka Kaisaria, lakini askari wengine na wale wa mikuki walirudi kwenye jengo la jeshi mjini Yerusalemu. 33 Askari wa farasi waliingia Kaisaria, wakampa barua Gavana Feliki, kisha wakamkabidhi Paulo kwake.
34 Gavana akaisoma barua na kumwuliza Paulo, “Unatoka jimbo gani?” Gavana alitambua kuwa Paulo alikuwa anatoka Kilikia. 35 Gavana akasema, “Nitakusikiliza Wayahudi wanaokushitaki watakapokuja hapa pia.” Kisha gavana akaamuru Paulo awekwe kwenye jumba la kifalme. (Jengo hili lilijengwa na Herode.)
Baadhi ya Wayahudi Wamshitaki Paulo
24 Siku tano baadaye Anania, kuhani mkuu, alikwenda mjini Kaisaria. Aliwachukua pamoja naye baadhi ya viongozi wa wazee wa Kiyahudi na mwanasheria aitwaye Tertulo. Walikwenda Kaisaria kutoa ushahidi dhidi ya Paulo mbele ya gavana. 2-3 Paulo aliitwa kwenye mkutano, na Tertulo akaanza kueleza mashitaka.
Tertulo alisema, “Mheshimiwa Feliki, kwa muda mrefu watu wetu wamefurahia amani kwa sababu yako, na mambo mengi mabaya katika nchi yetu yanarekebishwa kutokana na msaada wako wa hekima. Kwa hili sisi sote tunaendelea kushukuru. 4 Lakini sitaki kuchukua muda wako mwingi. Hivyo nitasema maneno machache. Tafadhali uwe mvumilivu. 5 Mtu huyu ni mkorofi. Anasababisha vurugu kwa Wayahudi kila mahali ulimwenguni. Ni kiongozi wa kundi la Wanazorayo. 6-8 Pia, alikuwa anajaribu kulinajisi Hekalu, lakini tulimsimamisha.[b] Unaweza kuamua ikiwa haya yote ni kweli. Mwulize maswali wewe mwenyewe.” 9 Wayahudi wengine wakakubali na kusema ndivyo ilivyo.
Paulo Ajitetea Mbele ya Feliki
10 Gavana alifanya ishara ili Paulo aanze kuzungumza. Hivyo Paulo alijibu, “Gavana Feliki, ninafahamu kuwa umekuwa jaji wa nchi hii kwa muda mrefu. Hivyo ninafurahi kujitetea mimi mwenyewe mbele yako. 11 Nilikwenda kuabudu Yerusalemu siku kumi na mbili tu zilizopita. Unaweza kutambua wewe mwenyewe kuwa hii ni kweli. 12 Wayahudi hawa wanaonishitaki, hawakuniona nikibishana na mtu yeyote wala kukusanya kundi la watu Hekaluni. Na sikuwa nabishana au kufanya vurugu kwenye masinagogi au mahali popote katika mji. 13 Watu hawa hawawezi kuthibitisha mambo wanayoyasema dhidi yangu sasa.
14 Lakini nitakuambia hili: Ninamuabudu Mungu, Mungu yule yule aliyeabudiwa na baba zetu, na kama mfuasi wa Njia, ambayo wayahudi hawa wanasema si njia sahihi. Na ninaamini kila kitu kinachofundishwa katika Sheria ya Musa na yote yaliyoandikwa katika vitabu vya manabii. 15 Nina tumaini katika Mungu kama walilonalo Wayahudi hawa, kwamba watu wote, wema na wabaya, watafufuliwa kutoka kwa wafu. 16 Hii ndiyo sababu daima nimejaribu kufanya kile ninachoamini kuwa sahihi mbele za Mungu na kila mtu.
17-18 Nimekuwa mbali na Yerusalemu kwa miaka mingi. Nilikwenda kule nikiwa na fedha za kuwasaidia watu wangu. Pia nilikuwa na sadaka za kutoa Hekaluni. Nilipokuwa nafanya hivyo, baadhi ya Wayahudi waliponiona pale. Nilikuwa nimemaliza ibada ya utakaso.[c] Sikufanya vurugu yoyote, na hakuna watu waliokuwa wamekusanyika kunizunguka. 19 Lakini baadhi ya Wayahudi kutoka Asia walikuwa pale. Walipaswa kuwa hapa mbele yako wakinishtaki ikiwa wana ushahidi kuwa nilifanya kitu chochote kibaya. 20 Waulize watu hawa ikiwa waliona kosa lolote kwangu niliposimama mbele ya mkutano wa baraza kuu mjini Yerusalemu. 21 Jibu pekee watakaloweza kukujibu ni hili: Kwamba nilipokuwa mbele zao nilipaza sauti na kusema, ‘Mnanishitaki leo kwa sababu ninaamini watu watafufuka kutoka kwa wafu!’”
22 Feliki tayari alikuwa anaelewa mengi kuhusu Njia. Akasimamisha kesi na kusema, “Kamanda Lisiasi atakapokuja hapa, nitaamua nini cha kufanya.” 23 Feliki alimwambia ofisa wa jeshi kumlinda Paulo lakini wampe uhuru kiasi na wawaruhusu rafiki zake wamletee chochote atakachohitaji.
Paulo Azungumza na Feliki na Mkewe
24 Baada ya siku chache, Feliki alikuja na mke wake Drusila, aliyekuwa Myahudi. Feliki akaagiza Paulo apelekwe kwake. Alimsikiliza Paulo akiongea kuhusu kumwamini Yesu Kristo. 25 Lakini Feliki aliogopa Paulo alipoongelea kuhusu vitu kama kutenda haki, kuwa na kiasi, na hukumu itakayokuja baadaye. Akasema, “Unaweza kwenda sasa. Nitakapokuwa na muda mwingi, nitakuita.” 26 Lakini Feliki alikuwa na sababu nyingine ya kuzungumza na Paulo. Alitegemea Paulo angempa rushwa, hivyo alimwita Paulo mara nyingi na kuzungumza naye.
27 Lakini baada ya miaka miwili, Porkio Festo akawa gavana. Hivyo Feliki hakuwa gavana tena. Lakini alimwacha Paulo gerezani ili kuwaridhisha Wayahudi.
Paulo Aomba Kumwona Kaisari
25 Festo akawa gavana na siku tatu baadaye akasafiri kwenda Yerusalemu kutoka Kaisaria. 2 Viongozi wa makuhani na viongozi maarufu wa Kiyahudi wakatoa mashitaka dhidi ya Paulo mbele ya Festo. 3 Walimwomba Festo awasaidie. Walitaka amrudishe Paulo Yerusalemu kwa sababu walipanga kumwua akiwa njiani. 4 Lakini Festo alijibu, “Hapana, Paulo ataendelea kuwekwa Kaisaria. Nitaenda huko mimi mwenyewe hivi karibuni, 5 na viongozi wenu wanaweza kufuatana nami. Kama mtu huyu hakika amefanya chochote kibaya, wanaweza kumshitaki huko.”
6 Festo alikaa Yerusalemu kwa siku nane au kumi zaidi kisha alirudi Kaisaria. Siku iliyofuata Festo akawaambia askari wamlete Paulo mbele yake. Festo alikuwa amekaa kwenye kiti cha hukumu. 7 Paulo aliingia kwenye chumba na Wayahudi waliokuja kutoka Yerusalemu walisimama kumzunguka. Walileta mashitaka mengi mazito dhidi yake, lakini hawakuweza kuthibitisha chochote. 8 Paulo alijitetea mwenyewe, akasema, “Sijatenda kitu chochote kibaya kinyume na sheria ya Kiyahudi, kinyume na Hekalu au kinyume na Kaisari.”
9 Lakini Festo alitaka kuwaridhisha Wayahudi. Hivyo alimwuliza Paulo, “Unataka kwenda Yerusalemu ili nikakuhukumu huko kutokana na mashitaka haya?”
10 Paulo akasema, “Kwa sasa nimesimama kwenye kiti cha hukumu cha Kaisari. Hapa ndipo ninatakiwa kuhukumiwa. Sijatenda lolote baya kwa Wayahudi na unafahamu hilo. 11 Ikiwa nilitenda chochote kibaya na sheria inasema ni lazima nife, basi ninakubali kuwa ninapaswa kufa. Siombi kuokolewa kutokana na kifo. Lakini kama mashitaka haya siyo ya kweli, basi hakuna anayeweza kunikabidhi kwa watu hawa. Hapana, Nataka Kaisari aisikilize kesi yangu!”
12 Festo alijadiliana na washauri wake kuhusu hili. Kisha akasema, “Umeomba kumwona Kaisari, basi utakwenda kwa Kaisari!”
Festo Amwuliza Mfalme Agripa Kuhusu Paulo
13 Siku chache baadaye Mfalme Agripa pamoja na dada yake aliyeitwa Bernike[d] walikuja Kaisaria kumtembelea Festo. 14 Walikaa huko kwa siku nyingi, na Festo akamwambia mfalme kuhusu kesi ya Paulo. Festo alisema, “Kuna mtu ambaye Feliki alimwacha gerezani. 15 Nilipokwenda Yerusalemu, viongozi wa makuhani na viongozi wa wazee wa Kiyahudi walitengeneza mashitaka dhidi yake. Walinitaka nimhukumu kifo. 16 Lakini niliwaambia, ‘Mtu anaposhitakiwa kuwa ametenda jambo baya, Warumi hawampeleki kwa watu wengine ili ahukumiwe. Kwanza, ni lazima aonane na watu wanaomshtaki. Na kisha ni lazima aruhusiwe kujitetea yeye mwenyewe dhidi ya mashitaka yao.’
17 Hivyo Wayahudi walipokuja hapa kwa ajili ya kesi, sikupoteza muda. Siku iliyofuata nilikaa kwenye kiti cha hukumu na kuamuru Paulo aletwe ndani. 18 Wayahudi walisimama na kumshitaki. Lakini hawakumshitaki kwa makosa niliyodhani wangemshitaki. 19 Mashitaka yao yote yalihusu dini yao wenyewe na kuhusu mtu anayeitwa Yesu. Yesu alikufa lakini Paulo anasema bado yuko hai. 20 Baada ya kuona kuwa sijui jinsi ya kuyachunguza mambo haya. Hivyo nilimwuliza Paulo, ‘Unataka kwenda Yerusalemu ili ukahukumiwe huko?’ 21 Lakini Paulo aliomba abaki mahabusu hapa Kaisaria. Anataka uamuzi kutoka kwa mfalme mkuu. Hivyo niliamua aendelee kushikiliwa hapa mpaka nitakapompeleka kwa Kaisari huko Rumi.”
22 Agripa akamwambia Festo, “Ningependa kumsikiliza mtu huyu pia.”
Festo akasema, “Utaweza kumsikiliza kesho.”
23 Siku iliyofuata Agripa na Bernike walikuja kwenye mkutano kwa fahari kubwa, wakijifanya watu wa muhimu sana. Waliingia kwenye chumba pamoja na viongozi wa kijeshi na watu maarufu wa mji. Festo akawaamuru askari wamwingize Paulo ndani.
24 Festo akasema, “Mfalme Agripa nanyi nyote mliokusanyika hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu. Wayahudi wote, hapa na Yerusalemu wamelalamika kwangu juu yake. Wanapolalamika, wanapaza sauti zao wakisema kwamba anapaswa kuuawa. 25 Nilipochunguza, sikuona ikiwa alitenda kosa lolote linalostahili hukumu ya kifo. Lakini ameomba kuhukumiwa na Kaisari, hivyo niliamua apelekwe Rumi. 26 Hata hivyo, sifahamu kwa hakika ni nini cha kumwandikia bwana wangu Kaisari kama sababu ya kumpeleka mtu huyu kwake. Hivo nimemleta mbele yenu ninyi nyote, hasa wewe, Mfalme Agripa. Ninatumaini kwamba utamwuliza maswali na kunipa kitu cha kumwandikia Kaisari. 27 Nafikiri ni upumbavu kupeleka mfungwa kwa Kaisari bila kuainisha mashitaka dhidi yake.”
© 2017 Bible League International