Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Historical

Read the books of the Bible as they were written historically, according to the estimated date of their writing.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Matendo 17-19

Paulo na Sila Wakiwa Thesalonike

17 Paulo na Sila walisafiri kupitia miji ya Amfipoli na Apolonia. Wakafika katika mji wa Thesalonike, ambako kulikuwa sinagogi la Kiyahudi. Paulo aliingia katika sinagogi kuwaona Wayahudi kama alivyokuwa akifanya. Wiki tatu zilizofuatia, kila siku ya Sabato alijadiliana nao kuhusu Maandiko. Alifafanua Maandiko kuwaonesha kuwa Masihi ilikuwa afe na kufufuka kutoka kwa wafu. Aliwaambia, “Huyu Yesu ninayewaambia habari zake ndiye Masihi.” Baadhi ya Wayahudi pale waliwaamini Paulo na Sila na waliamua kujiunga nao. Idadi kubwa ya Wayunani waliokuwa wanamwabudu Mungu wa kweli na wanawake wengi maarufu walijiunga nao pia.

Lakini Wayahudi ambao hawakuamini wakaingiwa na wivu, hivyo wakawakusanya baadhi ya watu wabaya katikati ya mji ili kufanya vurugu. Wakaunda kundi na wakanzisha vurugu mjini. Walikwenda nyumbani kwa Yasoni kuwatafuta Paulo na Sila. Walitaka kuwaleta mbele ya watu. Walipowakosa wakamkamata na kumburuta Yasoni na baadhi ya waamini wengine na kuwapeleka kwa viongozi wa mji. Watu wakapasa sauti na kusema, “Watu hawa Wamesababisha matatizo mengi kila mahali ulimwenguni, na sasa wamekuja hapa pia! Yasoni amewaweka nyumbani mwake. Wanavunja sheria za Kaisari. Wanasema kuna mfalme mwingine anayeitwa Yesu.”

Viongozi wa mji na watu wengine waliposikia hili waliudhika sana. Wakawalazimisha Yasoni na waamini wengine kuweka dhamana ya fedha kuthibitisha kuwa hakutakuwa vurugu tena. Kisha wakawaruhusu kuondoka.

Paulo na Sila Waenda Berea

10 Usiku ule ule waamini wakawapeleka Paulo na Sila katika mji mwingine ulioitwa Berea. Walipofika pale, walikwenda katika sinagogi la Kiyahudi. 11 Watu wa Berea walikuwa radhi kujifunza kuliko watu wa Thesalonike. Walifurahi waliposikia ujumbe aliowaambia Paulo. Waliyachunguza Maandiko kila siku ili kuhakikisha kuwa waliyoyasikia ni ya kweli. 12 Matokeo yake ni kuwa watu wengi miongoni mwao waliamini, wakiwemo wanawake maarufu Wayunani na wanaume.

13 Lakini Wayahudi wa Thesalonike walipojua kuwa Paulo alikuwa anawahubiri Ujumbe wa Mungu katika mji wa Berea, walikwenda huko pia. Waliwakasirisha watu na kufanya vurugu. 14 Hivyo waamini walimpeleka Paulo sehemu za pwani, lakini Sila na Timotheo walibaki Berea. 15 Wale waliokwenda na Paulo walimpeleka katika mji wa Athene. Waliporudi Berea, waliwapa ujumbe kutoka kwa Paulo Timotheo na Sila kuwa waende kuungana naye haraka kadiri watakavyoweza.

Paulo Akiwa Athene

16 Paulo alipokuwa akiwasubiri Sila na Timotheo katika mji wa Athene, aliudhika kwa sababu aliona mji ulikuwa umejaa sanamu. 17 Alipokuwa katika sinagogi alizungumza na Wayahudi na Wayunani waliokuwa wakimwabudu Mungu wa kweli. Alikwenda pia katika sehemu za wazi za umma za mikutano na kuzungumza na kila aliyekutana naye. 18 Baadhi ya wanafalsafa Waepikureo[a] na baadhi ya wanafalsafa Wastoiko[b] walibishana naye.

Baadhi yao walisema, “Mtu huyu hakika hajui anachokisema. Anajaribu kusema nini?” Paulo alikuwa anawaambia Habari Njema kuhusu Yesu na ufufuo. Hivyo walisema, “Anaonekana anatueleza kuhusu baadhi ya miungu wa kigeni.”

19 Walimchukua Paulo kwenye mkutano wa baraza la Areopago. Wakasema, “Tafadhali tufafanunile hili wazo jipya ambalo umekuwa ukifundisha. 20 Mambo unayosema ni mapya kwetu. Hatujawahi kusikia mafundisho haya, na tunataka kufahamu yana maana gani.” 21 (Watu wa Athene na wageni walioishi pale walitumia muda wao bila kufanya kazi yoyote isipokuwa kusikiliza na kuzungumza kuhusu mawazo mapya.)

22 Ndipo Paulo alisimama mbele ya mkutano wa baraza la Areopago na kusema, “Watu wa Athene, kila kitu ninachokiona hapa kinanionyesha kuwa ninyi ni watu wa dini sana. 23 Nilikuwa natembea katika mji wenu na nimeona mambo mnayoyaabudu. Niliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya juu yake: ‘Kwa Mungu Asiyejulikana.’ Mnamwabudu mungu msiyemjua. Huyu ni Mungu ninayetaka kuwaambia habari zake.

24 Ni Mungu aliyeumba ulimwengu na kila kitu ndani yake. Ni Bwana wa mbingu na nchi. Haishi katika mahekalu yaliyojengwa kwa mikono ya kibinadamu. 25 Ndiye anayewapa watu uzima, pumzi na kila kitu wanachohitaji. Hahitaji msaada wowote kutoka kwao. Ana kila kitu anachohitaji. 26 Mungu alianza kwa kumwumba mtu mmoja, na kutoka kwake aliumba mataifa yote mbalimbali, na akawaweka kila mahali ulimwenguni. Na aliamua ni wakati gani na wapi ambapo angewaweka ili waishi.

27 Mungu alitaka watu wamtafute yeye, na pengine kwa kumtafuta kila mahali, wangempata. Lakini hayuko mbali na kila mmoja wetu. 28 Ni kupitia Yeye tunaweza kuishi, kufanya yale tunayofanya na kuwa kama tulivyo. Kama baadhi ya methali zenu zilivyokwisha sema, ‘Sote tunatokana naye.’

29 Huo ndio ukweli. Sote tunatokana na Mungu. Hivyo ni lazima msifikiri kuwa Yeye ni kama kitu ambacho watu hukidhania au kukitengeneza. Hivyo ni lazima tusifikiri kuwa ametengenezwa kwa dhahabu, fedha au jiwe. 30 Hapo zamani watu hawakumwelewa Mungu, naye Mungu hakulijali hili. Lakini sasa anawaagiza wanadamu kila mahali kubadilika na kumgeukia Yeye. 31 Amekwisha chagua siku ambayo atawahukumu watu wote ulimwenguni katika namna isiyo na upendeleo. Atafanya hili kwa kumtumia mtu aliyemchagua zamani zilizopita. Na alithibitisha kwa kila mtu kwamba huyu ndiye mtu atakayefanya. Alilithibitisha kwa kumfufua kutoka kwa wafu!”

32 Watu waliposikia kuhusu mtu kufufuliwa kutoka kwa kifo, baadhi yao walicheka. Lakini wengine walisema, “Tutasikiliza mengi kuhusu hili kutoka kwako baadaye.” 33 Hivyo Paulo akaondoka kwenye mkutano wa baraza. 34 Lakini baadhi ya watu waliungana na Paulo na kuwa waamini. Miongoni mwao walikuwa Dionisi, ambaye alikuwa mjumbe wa baraza la Areopago, na mwanamke aliyeitwa Damari na baadhi ya wengine.

Paulo Akiwa Korintho

18 Baadaye, Paulo aliondoka Athene na kwenda katika mji wa Korintho. Akiwa huko alikutana na Myahudi aliyeitwa Akila, aliyezaliwa katika jimbo la Ponto. Lakini yeye na mke wake aliyeitwa Prisila, walikuwa tu ndiyo wamehamia Korintho kutoka Italia. Waliondoka Italia kwa sababu Kaisari Klaudio alikuwa ametoa amri Wayahudi wote waondoke Rumi. Paulo alikwenda kuwatembelea Akila na Prisila. Walikuwa watengenezaji wa mahema,[c] kama alivyokuwa Paulo, hivyo alikaa na kufanya kazi pamoja nao.

Kila siku ya Sabato Paulo alikwenda kwenye sinagogi na kuzungumza na Wayahudi na Wayunani, akijaribu kuwashawishi wamwamini Yesu. Lakini baada ya Sila na Timotheo kufika kutoka Makedonia, Paulo alitumia muda wake wote kuuhubiri ujumbe wa Mungu kwa Wayahudi, akiwaeleza kuwa Yesu ndiye Masihi. Lakini walimpinga Paulo na wakaanza kumtukana. Hivyo Paulo akakung'uta mavumbi kutoka kwenye nguo zake.[d] Akawaambia, “Msipookolewa, itakuwa makosa yenu ninyi wenyewe! Nimefanya yote ninayoweza kufanya. Baada ya hili nitawaendea watu wasio Wayahudi tu.”

Paulo aliondoka katika sinagogi na kuhamia nyumbani kwa Tito Yusto, mtu aliyekuwa anamwabudu Mungu wa Kweli, nyumba yake ilikuwa jirani na sinagogi. Krispo aliyekuwa kiongozi wa sinagogi lile, pamoja na watu wote waliokuwa wanaishi nyumbani mwake walimwamini Bwana Yesu. Watu wengi katika mji wa Korintho walimsikiliza Paulo, wakaamini na wakabatizwa.

Wakati wa usiku, Paulo aliona maono. Bwana alimwambia, “Usiogope, na usiache kuzungumza na watu. 10 Niko pamoja nawe, na hakuna atakayeweza kukudhuru. Kuna watu wangu wengi katika mji huu.” 11 Paulo alikaa pale kwa mwaka mmoja na nusu akiwafundisha watu ujumbe wa Mungu.

Paulo Afikishwa Mbele ya Galio

12 Galio alipokuwa gavana wa Akaya, baadhi ya Wayahudi walikusanyika wakawa kinyume cha Paulo. Wakampeleka mahakamani. 13 Wakamwambia Galio, “Mtu huyu anawafundisha watu kumwabudu Mungu kwa namna ambavyo ni kunyume na sheria yetu!”

14 Paulo alikuwa tayari kuzungumza, lakini Galio aliwaambia Wayahudi, “Ningewasikiliza ikiwa malalamiko yenu yangehusu dhuluma au kosa jingine. 15 Lakini yanahusu maneno na majina tu, mabishano yanayohusu sheria zenu wenyewe. Ni lazima mtatue tatizo hili ninyi wenyewe. Sitaki kuwa mwamuzi wa jambo hili.” 16 Hivyo Galio akawafanya waondoke mahakamani.

17 Kisha wote kwa pamoja wakamkamata Sosthenesi, kiongozi wa sinagogi. Wakampiga mbele ya mahakama. Lakini Galio hakulijali hili pia.

Paulo Arudi Antiokia

18 Paulo alikaa na waamini kwa siku nyingi. Kisha aliondoka na kusafiri majini kwenda Shamu. Prisila na Akila walikuwa pamoja naye pia. Walipofika Kenkrea Paulo akanyoa nywele zake kwa sababu aliweka nadhiri[e] kwa Mungu. 19 Kisha walikwenda Efeso, ambako Paulo aliwaacha Prisila na Akila. Paulo alipokuwa Efeso alikwenda katika sinagogi na kuzungumza na Wayahudi. 20 Walimwomba akae kwa muda mrefu lakini alikataa. 21 Aliwaacha na kusema, “Nitarudi tena kwenu ikiwa Mungu atataka nirudi.” Na hivyo akaabili kwenda Efeso.

22 Alipofika Kaisaria, alikwenda Yerusalemu na kulitembelea kanisa pale. Baada ya hapo alikwenda Antiokia. 23 Alikaa Antiokia kwa muda kisha akaondoka akipita katika nchi za Galatia na Frigia. Alisafiri kutoka mji mmoja hadi mji mwingine katika mikoa hii, akiwasaidia wafuasi wa Yesu kuimarika katika imani yao.

Apolo Akiwa Efeso na Korintho

24 Myahudi aliyeitwa Apolo alikuja Efeso. Alizaliwa katika mji wa Iskanderia, alikuwa msomi aliyeyajua Maandiko vizuri. 25 Alikuwa amefundishwa kuhusu Bwana na daima alifurahia[f] kuwaeleza watu kuhusu Yesu. Alichofundisha kilikuwa sahihi, lakini ubatizo alioufahamu ni ubatizo aliofundisha Yohana. 26 Apolo alianza kuzungumza kwa ujasiri katika sinagogi. Prisila na Akila walipomsikia akizungumza, walimchukua wakaenda naye nyumbani mwao kisha wakamsaidia kuielewa njia ya Mungu vizuri zaidi.

27 Apolo alitaka kwenda Akaya. Hivyo waamini wa Efeso wakamsaidia. Waliwaandikia barua wafuasi wa Bwana waliokuwa Akaya wakiwaomba wampokee Apolo. Alipofika pale, alikuwa msaada mkubwa kwa wale waliomwamini Yesu kwa sababu ya neema ya Mungu. 28 Alibishana kwa ujasiri na Wayahudi mbele ya watu wote. Alithibitisha kwa uwazi kuwa wayahudi walikuwa wanakosea. Alitumia Maandiko kuonesha kuwa Yesu ndiye Masihi.

Paulo Akiwa Efeso

19 Apolo alipokuwa katika mji wa Korintho, Paulo alikuwa anatembelea baadhi ya sehemu akiwa njiani kwenda Efeso. Alipofika Efeso waliwakuta baadhi ya wafuasi wa Bwana. Akawauliza, “Mlimpokea Roho Mtakatifu mlipoamini?”

Wafuasi hao wakamwambia, “Hatujawahi hata kusikia kuhusu Roho Mtakatifu!”

Paulo akawauliza, “Kwa hiyo ni mlibatizwa kwa ubatizo gani?”

Wakasema, “Kwa ubatizo aliofundisha Yohana.”

Paulo akasema, “Yohana aliwaambia watu wabatizwe kuonesha kuwa walidhamiria kubadili maisha yao. Aliwaambia watu kuamini katika yule atakaye kuja baada yake, naye huyo ni Yesu.”

Wafuasi hawa waliposikia hili, wakabatizwa katika jina la Bwana Yesu. Kisha Paulo akawawekea mikono, na Roho Mtakatifu akaja juu yao. Wakaanza kuzungumza na kutabiri katika lugha tofauti. Walikuwepo wanaume kama kumi na mbili katika kundi hili.

Paulo akaingia katika sinagogi na akazungumza kwa ujasiri. Aliendelea kufanya hivi kwa miezi mitatu. Alizungumza na Wayahudi, akijaribu kuwashawishi kukubali alichokuwa anawaambia kuhusu ufalme wa Mungu. Lakini baadhi yao wakawa wakaidi, wakakataa kuamini. Waliikashifu Njia[g] ya Bwana mbele ya kila mtu. Hivyo Paulo aliwaacha Wayahudi hawa na kuwachukua wafuasi wa Bwana pamoja naye. Alikwenda mahali ambapo mtu aitwaye Tirano alikuwa na shule. Hapo Paulo alizungumza na watu kila siku. 10 Alifanya hivi kwa miaka miwili na kila mtu aliyeishi Asia, Wayahudi na Wayunani alilisikia neno la Bwana.

Wana wa Skewa

11 Mungu alimtumia Paulo kufanya miujiza ya kipekee. 12 Baadhi ya watu walichukua vitambaa vya mkononi na nguo zilizovaliwa na Paulo na kuziweka juu ya wagonjwa. Wagonjwa waliponywa na pepo wabaya waliwatoka watu.

13-14 Pia baadhi ya Wayahudi walikuwa wanasafiri huku na huko wakiwatoa pepo wabaya kwa watu. Wana saba wa Skewa, mmoja wa viongozi wa makuhani, walikuwa wakifanya hili. Wayahudi hawa walijaribu kutumia jina la Bwana kuyatoa mapepo kwa watu. Wote walikuwa wanasema, “Katika jina la Bwana Yesu anayezungumzwa na Paulo ninakuamuru utoke!”

15 Lakini wakati fulani pepo akawaambia Wayahudi hawa, “Ninamfahamu Yesu, na ninafahamu kuhusu Paulo, na ninyi ni nani?”

16 Kisha mtu aliyekuwa na pepo ndani yake akawarukia. Alikuwa na nguvu kuliko wote. Akawapiga, akawachania nguo za na kuwavua, nao wakakimbia kutoka katika nyumba ile wakiwa uchi.

17 Watu wote katika Efeso, Wayahudi na Wayunani wakafahamu kuhusu hili. Wakaogopa na kumtukuza Bwana Yesu. 18 Waamini wengi walianza kukiri, wakisema mambo yote maovu waliyotenda. 19 Baadhi yao walikuwa wametumia uchawi huko nyuma. Waamini hawa walileta vitabu vyao vya uchawi na kuvichoma mbele ya kila mtu. Vitabu hivi vilikuwa na thamani ya sarafu hamsini elfu za fedha.[h] 20 Hivi ndivyo ambavyo neno la Bwana lilikuwa linasambaa kwa nguvu, likisababisha watu wengi kuamini.

Paulo Apanga Safari

21 Baada ya hili, Paulo alipanga kwenda Yerusalemu. Alipanga kupitia katika majimbo ya Makedonia na Akaya kisha kwenda Yerusalemu. Alisema, “Baada ya kwenda Yerusalemu, ni lazima niende Rumi pia.” 22 Timotheo na Erasto walikuwa wasaidizi wake wawili. Paulo aliwatuma watangulie Makedonia. Lakini yeye alikaa Asia kwa muda.

Tatizo Katika Mji wa Efeso

23 Lakini katika wakati huo huo kulikuwepo tatizo kuhusiana na Njia. Hivi ndivyo ilivyotokea: 24 Alikuwepo mtu aliyeitwa Demetrio aliyekuwa mfua fedha. Alikuwa akitengeneza sanamu ndogo za fedha zilizofanana na hekalu la Artemi, mungu mke. Wanaume waliokuwa wakifanya kazi hii walijipatia pesa nyingi sana.

25 Demetrio alifanya mkutano na watu hawa pamoja na wengine waliokuwa wanafanya kazi ya aina hiyo. Akawaambia, “Ndugu, mnafahamu kuwa tunapata pesa nyingi kutokana na kazi yetu. 26 Lakini angalieni kitu ambacho mtu huyu Paulo anafanya. Sikilizeni anachosema. Amewashawishi watu wengi katika Efeso na karibu Asia yote kubadili dini zao. Anasema miungu ambayo watu wanatengeneza kwa mikono si miungu wa kweli. 27 Ninaogopa hili litawafanya watu kuwa kinyume na biashara yetu. Lakini kuna tatizo jingine pia. Watu wataanza kufikiri kuwa hekalu la Artemi, mungu wetu mkuu halina maana. Ukuu wake utaharibiwa. Na Artemi ni mungu mke anayeabudiwa na kila mtu katika Asia na ulimwengu wote.”

28 Waliposikia hili, walikasirika sana. Wakapaza sauti zao wakisema, “Artemi, mungu mke wa Efeso ni mkuu!” 29 Mji wote ukalipuka kwa vurugu. Watu wakawakamata Gayo na Aristarko, waliotoka Makedonia waliokuwa wanasafiri na Paulo, wakawapeleka kwenye uwanja wa mji. 30 Paulo alitaka kwenda ili azungumze na watu, lakini wafuasi wa Bwana walimzuia. 31 Pia, baadhi ya viongozi katika jimbo la Asia waliokuwa rafiki zake walimtumia ujumbe wakimwambia asiende uwanjani.

32 Watu wengi walikuwa akipiga kelele kusema hili na wengine walisema jambo jingine. Mkutano ukawa na vurugu kubwa. Watu wengi hawakujua ni kwa nini walikwenda pale. 33 Baadhi ya Wayahudi wakamshawishi mtu mmoja aliyeitwa Iskanda asimame mbele ya umati, wakamwelekeza cha kusema. Iskanda alipunga mkono wake, akijaribu kuwaeleza watu jambo. 34 Lakini watu walipoona kuwa Iskanda ni Myahudi, wote wakaanza kupiga kelele ya aina moja. Kwa masaa mawili waliendelea kusema, “Artemi, mungu mke wa Efeso ni mkuu!”

35 Ndipo karani wa mji akawashawishi watu kunyamaza. Akawaambia, “Watu wa Efeso, kila mtu anafahamu kwamba Efeso ndiyo mji unaotunza hekalu la mungu mkuu mke Artemi. Kila mtu anafahamu pia kwamba tunatunza mwamba wake mtakatifu.[i] 36 Hakuna anayeweza kupinga hili, hivyo mnyamaze. Ni lazima mtulie na kufikiri kabla hamjafanya kitu chochote.

37 Mmewaleta watu[j] hawa hapa, lakini hawajasema kitu chochote kibaya kinyume na mungu wetu mke. Hawajaiba kitu chochote kutoka kwenye hekalu lake. 38 Tuna mahakama za sheria na wapo waamuzi. Je, Demetrio na watu hawa wanaofanya kazi pamoja naye wana mashitaka dhidi ya yeyote? Wanapaswa kwenda mahakamani wakawashtaki huko.

39 Kuna kitu kingine mnataka kuzungumzia? Basi njooni kwenye mikutano ya kawaida ya mji mbele ya watu. Litaweza kuamuriwa huko. 40 Ninasema hivi kwa sababu mtu mwingine anaweza kuona tukio hili la leo na akatushtaki kwa kuanzisha ghasia. Hatutaweza kufafanua vurugu hii, kwa sababu hakuna sababu za msingi za kuwepo mkutano huu.” 41 Baada ya karani wa mji kusema hili, aliwaambia watu kwenda majumbani mwao.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International