Chronological
Mkutano Yerusalemu
15 Kisha baadhi ya watu kutoka Uyahudi wakaja Antiokia na kuanza kuwafundisha jamii ya waamini wasio Wayahudi, wakisema, “Hamwezi kuokolewa ikiwa hamkutahiriwa kama Musa alivyotufundisha.” 2 Paulo na Barnaba wakayapinga mafundisho haya na wakahojiana na kubishana na watu hawa juu ya hili. Hivyo kundi la waamini likaamua kuwatuma Paulo, Barnaba, na baadhi ya watu wengine Yerusalemu ili kujadiliana na mitume na wazee kuhusu suala hili.
3 Kanisa liliwapa wale waliotumwa kila kitu walichohitaji kwa ajili ya safari yao. Walisafiri kupitia maeneo ya Foeniki na Samaria, ambako walieleza kwa undani mambo yote namna ambavyo wasio Wayahudi wamemgeukia Mungu wa kweli. Habari hii iliwafurahisha waamini wote. 4 Walipofika Yerusalemu, mitume, wazee na kanisa lote waliwakaribisha. Paulo, Barnaba, na wengine wakaeleza yote ambayo Mungu alitenda kupitia wao. 5 Baadhi ya waamini mjini Yerusalemu waliokuwa Mafarisayo,[a] walisimama na kusema, “Waamini wasio Wayahudi lazima watahiriwe. Ni lazima tuwaambie waitii Sheria ya Musa!”
6 Ndipo mitume na wazee wakakusanyika kulichunguza jambo hili. 7 Baada ya majadiliano ya muda mrefu, Petro akasimama na kuwaambia, “Ndugu zangu, nina uhakika mnakumbuka kilichotokea siku za nyuma. Mungu alinichagua kutoka miongoni mwenu kuzihubiri Habari Njema kwa watu wasio Wayahudi. Kupitia mimi walisikia Habari Njema na kuamini. 8 Mungu anamfahamu kila mtu, hata mawazo yao, na amewakubali watu hawa wasio Wayahudi. Amelionyesha hili kwetu kwa kuwapa Roho Mtakatifu kama alivyotupa sisi. 9 Mbele za Mungu, wasio Wayahudi hawako tofauti na sisi. Mungu aliisafisha mioyo yao walipoamini. 10 Kwa nini sasa mnawatwisha mzigo mzito kwenye shingo zao? Je, mnajaribu kumkasirisha Mungu? Sisi na baba zetu hatukuweza kuubeba mzigo huo. 11 Hapana, tunaamini kuwa sisi na watu hawa tutaokolewa kwa namna moja iliyo sawa, ni kwa neema ya Bwana Yesu.”
12 Ndipo kundi lote likawa kimya. Waliwasikiliza Paulo na Barnaba walipokuwa wanaeleza kuhusu ishara na maajabu ambayo kupitia wao Mungu aliwatendea watu wasio Wayahudi. 13 Walipomaliza kusema, Yakobo akasema, “Ndugu zangu, nisikilizeni. 14 Simoni Petro ametueleza namna ambavyo siku za mwanzoni Mungu alilionyesha pendo lake kwa watu wasio Wayahudi, kwa kuwakubali na kuwafanya kuwa watu wake. 15 Maneno ya manabii yanakubaliana na hili:
16 ‘Nitarudi baada ya hili.
Nitaijenga nyumba ya Daudi tena.
Imeanguka chini.
Nitazijenga tena sehemu za nyumba yake zilizoangushwa chini.
Nitaifanya nyumba yake kuwa mpya.
17 Kisha wanadamu wengine wote,
watu niliowachagua kutoka mataifa mengine,
watataka kunifuata mimi, Bwana.
Hivi ndivyo Bwana anasema,
naye ndiye afanyaye mambo haya yote.’(A)
18 ‘Haya yote yalijulikana tangu zamani.’[b]
19 Hivyo nadhani tusiyafanye mambo kuwa magumu kwa wasio Wayahudi waliomgeukia Mungu. 20 Badala yake, tuwatumie barua kuwaambia mambo ambayo hawapaswi kutenda:
Wasile chakula kilichotolewa kwa sanamu maana chakula hiki huwa najisi.[c]
Wasijihusishe na dhambi ya zinaa.
Wasile nyama inayotokana na wanyama walionyongwa au nyama ambayo bado ina damu ndani yake.
21 Wasitende mojawapo ya mambo haya, kwa sababu bado kuna watu katika kila mji wanaofundisha Sheria ya Musa. Maneno ya Musa yamekuwa yakisomwa katika masinagogi kila siku ya Sabato kwa miaka mingi.”
Barua kwa Waamini Wasio Wayahudi
22 Mitume, wazee na kanisa lote wakataka kuwatuma baadhi ya watu wafuatane na Paulo na Barnaba kwenda Antiokia. Wakawachagua baadhi ya watu kutoka miongoni mwao wenyewe. Waliwachagua Yuda (ambaye pia aliitwa Barsaba) na Sila, watu walioheshimiwa na waamini. 23 Kundi la waamini likaandika barua na kuwatuma watu hawa. Barua ilisema:
Kutoka kwa mitume na wazee, ndugu zenu.
Kwa ndugu wote wasio Wayahudi katika mji wa Antiokia na katika majimbo ya Shamu na Kilikia.
Ndugu Wapendwa:
24 Tumesikia kuwa baadhi ya watu kutoka kwetu walikuja kwenu. Walichosema kiliwasumbua na kuwaudhi. Lakini hatukuwaambia kufanya hili. 25 Sisi sote tumekubaliana kuwachagua baadhi ya watu na kuwatuma kwenu. Watakuwa na rafiki zetu wapendwa, Barnaba na Paulo. 26 Barnaba na Paulo wameyatoa maisha yao kumtumikia Bwana wetu Yesu Kristo. 27 Hivyo tumewatuma Yuda na Sila pamoja nao. Watawaambia mambo yanayofanana. 28 Imempendeza Roho Mtakatifu na sisi kwamba tusiwatwishe mizigo ya ziada, isipokuwa kwa mambo haya ya muhimu:
29 Msile chakula kilichotolewa kwa sanamu.
Msile nyama inayotokana na wanyama walionyongwa au nyama ambayo bado ina damu ndani yake.
Msijihusishe na uzinzi.
Mkijitenga na mambo haya, mtakuwa mnaenenda vyema.
Wasalamu.
30 Hivyo Paulo, Barnaba, Yuda, na Sila waliondoka Yerusalemu na kwenda Antiokia. Walipofika huko walilikusanya kundi la waamini pamoja na wakawapa barua. 31 Waamini walipoisoma, wakafurahi na kufarijika. 32 Yuda na Sila ambao pia walikuwa manabii, waliwatia moyo waamini kwa maneno mengi na kuwafanya waimarike katika imani yao. 33 Baada ya Yuda na Sila kukaa pale kwa muda, waliondoka. Waamini waliwaruhusu waende kwa amani kisha wakarudi Yerusalemu kwa wale waliowatuma. 34 [d]
35 Lakini Paulo na Barnaba walikaa Antiokia. Wao na wengine wengi waliwafundisha waamini na kuwahubiri watu wengine Habari Njema kuhusu Bwana.
Paulo na Barnaba Watengana
36 Wakati fulani baadaye, Paulo akamwambia Barnaba, “Turudi katika miji yote tulikowahubiri watu ujumbe wa Bwana. Tuwatembelee waamini tuone wanaendeleaje.”
37 Barnaba alitaka Yohana Marko afuatane nao pia. 38 Lakini Yohana Marko hakukaa nao mpaka mwisho katika safari ya kwanza. Aliwaacha Pamfilia. Hivyo Paulo alisisitiza kuwa wasiende pamoja naye wakati huu. 39 Paulo na Barnaba walikuwa na mjadala mkali kuhusu hili. Ulikuwa mbaya sana ikabidi watengane na kwenda njia tofauti. Barnaba akatweka tanga kwenda Kipro, akamchukua Marko pamoja naye.
40 Paulo alimchagua Sila kwenda naye. Waamini Antiokia walimweka Paulo katika uangalizi wa Bwana na kumtuma. 41 Paulo na Sila walikwenda kwa kupitia katika majimbo ya Shamu na Kilikia, wakiyasaidia makanisa kuimarika.
Timotheo Afuatana na Paulo na Sila
16 Paulo alikwenda Derbe kisha Listra, ambako mfuasi wa Yesu aliyeitwa Timotheo aliishi. Mamaye Timotheo alikuwa mwamini wa Kiyahudi, lakini baba yake alikuwa Myunani. 2 Waamini katika miji ya Listra na Ikonia walimsifu Timotheo kwa mambo mema. 3 Paulo alitaka kusafiri pamoja na Timotheo, lakini Wayahudi wote walioishi katika eneo lile walijua kuwa baba yake alikuwa Myunani. Hivyo ikamlazimu Paulo amtahiri Timotheo ili kuwaridhisha Wayahudi.
4 Kisha Paulo na wale waliokuwa pamoja naye wakasafiri kupitia miji mingine. Wakawapa waamini kanuni na maamuzi yaliyofikiwa na mitume na wazee wa Yerusalemu. Wakawaambia wazitii kanuni hizo. 5 Hivyo makanisa yakawa yanaongezeka katika imani, na idadi ya waamini iliongezeka kila siku.
Paulo Aitwa Makedonia
6 Paulo na wale waliokuwa pamoja naye walisafiri kwa kupita katika maeneo ya Frigia na Galatia kwa sababu Roho Mtakatifu hakuwaruhusu kuzihubiri Habari Njema katika jimbo la Asia. 7 Walipofika kwenye mpaka wa Misia, walijaribu kwenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu kwenda huko. 8 Hivyo wakapita Misia na kwenda katika mji wa Troa.
9 Usiku ule Paulo aliona maono kwamba mtu kutoka Makedonia alimjia Paulo. Mtu huyo alisimama mbele yake na kumsihi akisema, “Vuka njoo Makedonia utusaidie.” 10 Baada ya Paulo kuona maono yale, tulijiandaa[e] haraka na tukaondoka kwenda Makedonia. Tulielewa kuwa Mungu ametuita ili tukahubiri Habari Njema huko Makedonia.
Kuongoka kwa Lydia
11 Tulisafiri kwa merikebu kutoka Troa na tukaabili kwenda katika kisiwa cha Samothrake. Siku iliyofuata tukasafiri kwenda katika mji wa Neapoli. 12 Kisha tulisafiri kwa nchi kavu mpaka Filipi, koloni la Rumi na mji maarufu katika la Makedonia. Tulikaa pale kwa siku chache.
13 Siku ya Sabato tulikwenda mtoni, nje ya lango la mji. Tulidhani tungepata mahali ambapo Wayahudi hukutana mara kwa mara kwa ajili ya kuomba. Baadhi ya wanawake walikuwa wamekusanyika huko, na hivyo tulikaa chini na kuzungumza nao. 14 Miongoni mwao alikuwepo mwanamke aliyeitwa Lydia kutoka katika mji wa Thiatira. Alikuwa mwuza rangi ya zambarau. Alikuwa mwabudu Mungu wa kweli. Lydia alimsikiliza Paulo, na Bwana akaufungua moyo wake kuyakubali yale Paulo alikuwa anasema. 15 Yeye na watu wote waliokuwa wakiishi katika nyumba yake walibatizwa. Kisha akatualika nyumbani mwake. Alisema, “Ikiwa mnaona mimi ni mwamini wa kweli wa Bwana Yesu, njooni mkae nyumbani mwangu.” Alitushawishi tukae nyumbani mwake.
Paulo na Sila Wakiwa Gerezani
16 Siku moja tulipokuwa tunakwenda pale mahali pa kufanyia kuomba, mtumishi mmoja msichana alikutana nasi. Msichana huyu alikuwa na roho ya ubashiri[f] ndani yake iliyompa uwezo wa kutabiri mambo yatakayotokea baadaye. Kwa kufanya hivi alipata fedha nyingi kwa ajili ya waliokuwa wanammiliki. 17 Akaanza kumfuata Paulo na sisi sote kila mahali akipaza sauti na kusema, “Watu hawa ni watumishi wa Mungu Aliye Juu! Wanawaambia mnavyoweza kuokolewa!” 18 Aliendelea kufanya hivi kwa siku kadhaa na ikamuudhi Paulo, akageuka na kumkemea yule roho akisema, “Kwa uwezo wa Yesu Kristo, ninakuamuru utoke ndani yake!” Mara ile roho chafu ikamtoka.
19 Wamiliki wa mtumishi yule msichana walipoona hili, wakatambua kuwa hawataweza kumtumia tena ili kupata pesa. Hivyo wakawakamata Paulo na Sila na kuwaburuta mpaka kwa watawala. 20 Wakawaleta Paulo na Sila mbele ya maofisa wa Kirumi na kusema, “Watu hawa ni Wayahudi, wanafanya vurugu katika mji wetu. 21 Wanafundisha desturi ambazo sisi raia wa Rumi haturuhusiwi kuzifuata wala kutenda.”
22 Umati wote wa watu ukawa kinyume na Paulo na Sila. Maofisa wakawachania nguo Paulo na Sila na wakaamuru wapigwe bakora. 23 Walichapwa sana kisha wakawekwa gerezani. Maofisa wakamwambia mkuu wa gereza, “Walinde watu hawa kwa umakini!” 24 Mkuu wa gereza aliposikia amri hii maalumu, aliwaweka Paulo na Sila ndani zaidi gerezani na kuwafunga miguu yao kwenye nguzo kubwa za miti.
25 Usiku wa manane Paulo na Sila walipokuwa wakiomba na kumwimbia Mungu nyimbo za sifa, wafungwa wengine wakiwa wanawasikiliza. 26 Ghafla kulitokea tetemeko kubwa lililotikisa msingi wa gereza. Milango yote ya gereza ilifunguka, na minyororo waliyofungwa wafungwa wote ikadondoka. 27 Mkuu wa gereza alipoamka na kuona milango ya gereza imefunguliwa. Alidhani wafungwa wametoroka, hivyo alichukua upanga wake ili ajiue.[g] 28 Lakini Paulo alipaza sauti akamwambia, “Usijidhuru! Sote tuko hapa!”
29 Mkuu wa gereza akaagiza aletewe taa. Kisha akakimbia kuingia ndani, akitetemeka kwa woga, akaanguka mbele ya Paulo na Sila. 30 Kisha akawatoa nje na kusema, “Nifanye nini ili niokoke?”
31 Wakamwambia, “Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokolewa pamoja na watu wote waishio katika nyumba yako.” 32 Hivyo Paulo na Sila wakamhubiri ujumbe wa Bwana mkuu wa gereza na watu wote walioishi katika nyumba yake. 33 Ilikuwa usiku sana, lakini mkuu wa gereza aliwachukua Paulo na Sila na akawaosha majeraha yao. Kisha mkuu wa gereza na watu wote katika nyumba yake wakabatizwa. 34 Baada ya hili mkuu wa gereza akawachukua Paulo na Sila nyumbani kwake akawapa chakula. Watu wote walifurahi kwa sababu sasa walikuwa wanamwamini Mungu.
35 Asubuhi iliyofuata maofisa wa Kirumi waliwatuma baadhi ya askari kwenda gerezani na wakamwambia mkuu wa gereza, “Waachie watu hawa huru.”
36 Mkuu wa gereza akamwambia Paulo, “Maofisa wamewatuma askari hawa ili kuwaachia huru. Mnaweza kuondoka sasa. Nendeni kwa amani.”
37 Lakini Paulo akawaambia askari, “Wale maofisa hawakuthibitisha kuwa tulifanya chochote kibaya, lakini walitupiga kwa bakora hadharani na kutuweka gerezani. Nasi ni raia wa Rumi.[h] Na sasa wanataka tuondoke kimya kimya. Haiwezekani, ni lazima waje hapa wao wenyewe kisha watutoe nje!”
38 Askari wakawaambia maofisa alichosema Paulo. Waliposikia kwamba Paulo na Sila ni raia wa Rumi, waliogopa. 39 Hivyo walikwenda gerezani kuwaomba msamaha. Waliwatoa nje ya gereza na kuwaomba waondoke mjini. 40 Lakini Paulo na Sila walipotoka gerezani, walikwenda nyumbani kwa Lydia. Wakawaona baadhi ya waamini pale, wakawatia moyo. Kisha wakaondoka.
© 2017 Bible League International