Beginning
4 Ninalolisema ni hili: Wakati mrithi wa vyote alivyomiliki baba yake bado ni mdogo, hana tofauti yo yote na mtumwa. Haijalishi kuwa anamiliki vitu vyote. 2 Wakati wa utoto bado anapaswa kuwatii wale waliochaguliwa kumtunza. Lakini anapoufikia umri ambao baba yake ameuweka, anakuwa huru. 3 Ndivyo ilivyo hata kwetu sisi. Mwanzoni tulikuwa kama watoto, tukiwa watumwa wa mamlaka za uovu[a] zinazoutawala ulimwengu huu wa sasa. 4 Lakini wakati sahihi ulipofika, Mungu akamtuma Mwanaye, aliyezaliwa na mwanamke na akaishi chini ya sheria. 5 Mungu alifanya hivi ili aweze kuwaweka huru wale waliokuwa chini ya sheria. Kusudi la Mungu lilikuwa kutuasili[b] sisi kama watoto wake.
6 Ninyi sasa ni watoto wa Mungu. Na ndiyo sababu Mungu amemtuma Roho wa Mwanaye mioyoni mwetu. Huyo Roho aliye ndani yetu hulia “Aba,[c] yaani Baba.” 7 Sasa ninyi si watumwa kama mwanzo. Ni watoto wa Mungu, na mtapokea kila kitu ambacho Mungu aliwaahidi watoto wake. Hii yote ni kwa sababu ya yale ambayo Mungu amewatendea ninyi.
Upendo wa Paulo kwa Waamini wa Galatia
8 Zamani hamkumjua Mungu. Mlikuwa watumwa wa miungu isiyokuwa halisi. 9 Lakini sasa mnamjua Mungu wa kweli. Hakika, Mungu ndiye anayewajua ninyi. Hivyo kwa nini sasa mnavigeukia vikosi dhaifu na visivyo na manufuaa yoyote mlivyovifuata hapo mwanzo? Mnataka kuwa watumwa wa mambo haya tena? 10-11 Inanipa wasiwasi kwa kuwa mnaadhimisha siku, miezi, misimu na miaka. Nina hofu ya kuwa nimefanya kwa bidii kazi bure kwa ajili yenu.
12 Ndugu zangu, naomba mniige mimi kama ambavyo mimi nimekuwa kama ninyi. Hamkunikosea kwa jambo lololote. 13 Mnajua kuwa nilikuja kwenu mara ya kwanza kwa sababu nilikuwa mgonjwa. Ndipo nilipowaeleza ninyi Habari Njema. 14 Ugonjwa wangu uliwaelemea. Hata hivyo hamkunikataa kutokana na fadhaa ama hofu. Bali, mlinikaribisha kama vile nilikuwa malaika kutoka kwa Bwana. Mlinipokea kama vile nilikuwa Kristo Yesu mwenyewe! 15 Mlikuwa na furaha sana wakati huo. Nini kimetokea kwa imani yenu ya awali kwamba mimi nilikuwa mtu niliyebarikiwa kipekee na Mungu? Naweza kusema bila shaka yoyote kwamba mngeliweza kufanya kitu chochote kunisaidia. Kama ingeliwezekana, mngeliyang'oa hata macho yenu na kunipa mimi. 16 Je, nimekuwa sasa adui yenu kwa sababu nawaambia ukweli?
17 Watu hawa[d] wanajitahidi sana kuonesha kuvutiwa nanyi,[e] lakini hiyo siyo nzuri kwenu. Wanataka kuwashawishi ninyi ili mtugeuke sisi na kuambatana nao. 18 Inapendeza daima kuwa na mtu anayevutiwa nawe katika jambo lililo jema. Hivyo ndivyo nilivyofanya nilipokuwa pamoja nanyi. Siku zote inapendeza, na si pale tu mimi nikiwapo. 19 Watoto wangu wadogo, nasikia uchungu tena kwa ajili yenu, kama mama anayejifungua. Nitaendelea kusikia uchungu huu mpaka watu watakapofikia kumwona Kristo wawatazamapo ninyi. 20 Natamani ningekuwa nanyi sasa. Ndipo labda ninapoweza kubadilisha namna ninavyoongea nanyi. Sasa sielewi nifanye nini juu yenu.
Mfano wa Hajiri na Sara
21 Baadhi yenu mnataka kuwa chini ya sheria. Niambieni, mnajua sheria inavyosema? 22 Maandiko yanasema kwamba Ibrahimu alikuwa na wana wawili. Mama wa mwana mmoja alikuwa ni mjakazi, na mama wa mwana mwingine alikuwa wa mwanamke aliye huru. 23 Mwana wa Ibrahimu kutoka kwa mjakazi alizaliwa kwa namna ya kawaida ya kibinadamu. Lakini mwana kutoka kwa mwanamke aliyekuwa huru alizaliwa kwa sababu ya ahadi ambayo Mungu alimpa Ibrahimu.
24 Habari hii ina maana nyingine kwenu. Wanawake wawili ni sawa na maagano mawili baina ya Mungu na watu wake. Agano moja ni sheria ambayo Mungu aliifanya katika Mlima Sinai, inayowafanya watu wawe watumwa. Mwanamke aliyeitwa Hajiri yuko kama agano la kwanza. 25 Hivyo Hajiri anauwakilisha Mlima Sinai uliopo Arabia. Na anafanana na Yerusalemu wa sasa, kwa sababu mji huu uko utumwani pamoja na watu wake. 26 Lakini Yerusalemu ya mbinguni ulio juu uko kama mwanamke aliye huru, ambaye ndiye mama yetu. 27 Maandiko yanasema,
“Ufurahi mwanamke, wewe uliye tasa.
Ufurahi kwani hukuwahi kuzaa.
Piga kelele na ulie kwa furaha!
Hukupata uchungu wa kuzaa.
Mwanamke aliye peke yake atapata watoto zaidi
zaidi ya mwanamke aliye na mume.”(A)
28 Ndugu zangu, ninyi ni watoto mliozaliwa kwa sababu ya ahadi ya Mungu, kama Isaka alivyozaliwa. 29 Lakini mwana mwingine wa Ibrahimu, aliyezaliwa kwa njia ya kawaida, alisababisha matatizo kwa yule aliyezaliwa kwa nguvu ya Roho. Ndivyo ilivyo leo. 30 Lakini Maandiko yanasemaje? “Mfukuze mjakazi na mwanawe! Mwana wa mwanamke aliye huru atapokea kila kitu alicho nacho baba yake, lakini mwana wa mjakazi hatapokea kitu.”(B) 31 Hivyo, kaka na dada zangu, sisi si watoto wa mjakazi. Ni watoto wa mwanamke aliye huru.
Utunzeni Uhuru Wenu
5 Sasa tuko huru, kwa sababu Kristo alituweka huru ili tuweze kuishi tukiufurahia uhuru huo. Hivyo muwe imara katika uhuru huo. Msimruhusu mtu yeyote awaingize utumwani tena. 2 Sikilizeni! Mimi Paulo nawaambia kwamba ikiwa mtakubali kutahiriwa, basi Kristo hatakuwa na manufaa kwenu. 3 Tena, ninamwonya kila mtu atakayeruhusu atahiriwe, kwamba akifanya hivyo itampasa aifuate sheria yote. 4 Ikiwa utajaribu kufanyika mwenye haki mbele za Mungu kwa njia ya sheria, maisha yako na Kristo yamepotea, kwani umeiacha neema ya Mungu. 5 Ninasema hivi kwa sababu tumaini letu la kufanywa wenye haki mbele za Mungu huja kwa imani. Na kwa nguvu ya Roho kwa njia ya imani, tunangoja kwa utulivu na kwa matumaini yenye ujasiri hukumu ya Mungu inayotuweka huru. 6 Mtu anapokuwa wa Kristo Yesu, vyote kutahiriwa ama kutotahiriwa havina nguvu ya kuleta manufaa yoyote. Lakini kwa wale walio ndani ya Kristo Yesu imani inatenda kazi kupitia upendo.
7 Mlikuwa mnapiga mbio vizuri sana. Ni nani aliyewafanya mkaacha kuitii kweli? 8 Hakika hakuwa yule aliyewachagua. 9 Mjihadhari! “Chachu ndogo tu hufanya mkate wote mzima uumuke.”[f] 10 Nimeridhika moyoni mbele za Bwana kuwa hamtafikiri vinginevyo. Mtu yule anayewasumbua atahukumiwa hata angekuwa nani?
11 Kaka na dada zangu, sifundishi kuwa ni lazima mwanaume atahiriwe. Kama nitaendelea kuwafundisha wanaume watahiriwe, kwa nini watu bado wanaendelea kunitesa? Ikiwa bado nafundisha tohara, basi ujumbe wangu kuhusu msalaba hautaendelea kuwa tatizo. 12 Natamani watu hao wanaowasumbua wangeongeza na kuhasi[g] juu ya tohara yao.
13 Ndugu na dada zangu, Mungu aliwaita ili muwe huru. Lakini msiutumie uhuru wenu kama udhuru wa kutimiza yale yote mnayoyapenda, badala yake, msaidiane ninyi kwa ninyi kwa upendo. 14 Sheria yote imepewa muhtasari katika amri hii moja tu, “Mpende jirani yako[h] kama unavyojipenda mwenyewe.”(C) 15 Ikiwa mtaendelea kuumizana na kuraruana, muwe waangalifu, vinginevyo mtaangamizana ninyi kwa ninyi.
Roho na Asili ya Kibinadamu
16 Hivyo ninawaambieni, ishini kama Roho anavyowaongoza. Hapo hamtatenda dhambi kutokana na tamaa zenu mbaya. 17 Utu wenu wa dhambi unapenda yale yaliyo kinyume cha Roho, na Roho anataka yale yaliyo kinyume na utu wa dhambi. Hao siku zote hushindana wao kwa wao. Kwa jinsi hiyo ninyi hamko huru kufanya chochote mnachotaka kufanya. 18 Lakini mkimruhusu Roho awaongoze, hamtakuwa chini ya sheria.[i]
19 Mambo mabaya yanayofanywa na mwili wa dhambi ni dhahiri: uasherati, tabia chafu, kufanya mambo yenye kuleta aibu, 20 kuabudu miungu wa uongo, kushiriki mambo ya uchawi, kuwachukia watu, kuanzisha mafarakano, kuwa na wivu, hasira ama choyo, kusababisha mabishano na kujigawa kimakundi na kuwatenga wengine, 21 kujawa na husuda, kulewa pombe, kushiriki karamu zenye ulafi na uasi mwingi na kufanya mambo yanayofanana na hayo. Ninawatahadharisha mapema kama nilivyowatahadharisha mwanzo: Watu wanaofanya mambo hayo hawatahesabiwa kama watoto watakaourithi ufalme wa Mungu. 22 Lakini tunda linalozaliwa na Roho katika maisha ya mtu ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, 23 upole, na kiasi. Hakuna sheria juu ya mambo kama haya. 24 Wale walio wa Kristo Yesu wameusulubisha udhaifu wao wa kibinadamu pamoja na tamaa zake za dhambi na zile za mwili. Wameachana na utu wao wa kale wenye hisia za ubinafsi na uliotaka kufanya mambo maovu. 25 Tunayapata maisha yetu mapya kutoka kwa Roho, hivyo tunapaswa kuufuata uongozi wa Roho. 26 Tusijivune na kujisifu juu yetu wenyewe. Hatupaswi kuchokozana kwa mashindano baina yetu ama kuoneana wivu.
Tuishi kwa Kusaidiana Sisi kwa Sisi
6 Ndugu zangu, ikiwa mmoja wenu atakosea, ninyi mnaomfuata Roho mnapaswa kumwendea yule anayetenda dhambi. Msaidieni mtu huyo awe mwenye haki tena. Mfanye hivyo kwa njia ya upole, na muwe waangalifu, kwa maana nanyi pia mnaweza kujaribiwa kutenda dhambi. 2 Msaidiane ninyi kwa ninyi katika kubeba mizigo yenu. Mnapofanya hivi, mtakuwa mnatimiza yote ambayo sheria ya Kristo imewaagiza kufanya. 3 Maana mtu akijiona kuwa yeye ni wa muhimu sana na kumbe sio wa muhimu, anajidanganya mwenyewe. 4 Kila mmoja aipime kazi yake mwenyewe kuona ikiwa kuna chochote cha kujivunia. Kama ndivyo, uyatunze hayo moyoni mwako wala usijilinganishe na mtu mwingine yeyote. 5 Maana sisi sote tunawajibika kwa yale tunayofanya.
Msiache Kutenda Mema
6 Yule anayefundishwa neno la Mungu anapaswa kumshirikisha mwalimu wake mambo mema aliyonayo.
7 Ikiwa mnadhani mnaweza kumdanganya Mungu, mtakuwa mnajidanganya wenyewe. Mtavuna yale mnayopanda. 8 Yule anayepanda kwa kuiridhisha nafsi yake ya dhambi, mavuno yatakayopatikana ni uharibifu kabisa. Lakini mkipanda kwa kuiridhisha Roho, mavuno yenu katika Roho yatakuwa uzima wa milele. 9 Hatupaswi kuchoka katika kutenda mema. Tutapata mavuno yetu kwa wakati sahihi, tusipokata tamaa. 10 Tunapokuwa na nafasi ya kumtendea mema kila mtu, tufanye hivyo. Lakini tuzingatie zaidi kuwatendea mema wale walio wa familia ya waamini.
Paulo Amalizia Barua Yake
11 Huu ni mwandiko wa mkono wangu mwenyewe. Mnaweza kuona jinsi herufi zilivyo kubwa.[j] 12 Watu wale wanaojaribu kuwalazimisha ninyi kutahiriwa wanafanya hivyo ili wawaridhishe Wayahudi wenzao. Wanaogopa wasije wakateswa kwa sababu ya msalaba[k] wa Kristo. 13 Maana hata wale waliotahiriwa hawaitii sheria. Na bado wanawataka ninyi mtahiriwe ili waweze kujisifu kwa ajili ya yale waliyowatendea ninyi.
14 Mimi nisijisifu kwa ajili ya mambo kama haya. Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo ndiyo sababu pekee ya kujivuna kwangu. Kupitia kifo cha Yesu msalabani ulimwengu ukafa[l] kwangu, nami nimeufia ulimwengu. 15 Haijalishi kwamba mtu ametahiriwa au hajatahiriwa. Kinachojalisha ni uumbaji mpya wa Mungu katika Kristo.[m] 16 Amani iwe kwa wale wote wanaoifuata njia hii mpya. Na rehema za Mungu ziwe juu ya watu wake Israeli.
17 Kwa hiyo msinitaabishe kwa namna yoyote. Nina makovu mwilini mwangu yanayoonyesha[n] kuwa mimi ni wa Yesu.
18 Ndugu na dada zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi nyote. Amina.
© 2017 Bible League International