Beginning
Uzima Katika Roho
8 Hivyo mtu yeyote aliye wa Kristo Yesu hana hukumu ya kifo. 2 Hiyo ni kwa sababu kwa njia ya Kristo Yesu sheria ya Roho inayoleta uzima imewaweka ninyi[a] huru kutoka katika sheria inayoleta dhambi na kifo. 3 Ndiyo, sheria haikuwa na nguvu ya kutusaidia kwa sababu ya udhaifu wetu wa kibinadamu. Lakini Mungu akafanya kile ambacho sheria haikuweza kufanya: Alimtuma Mwanaye duniani akiwa na mwili ule ule tunaoutumia kutenda dhambi. Mungu alimtuma ili awe njia ya kuiacha dhambi. Alitumia maisha ya mwanadamu ili kuipa dhambi hukumu ya kifo. 4 Mungu alifanya hivi ili tuweze kuishi kama sheria inavyotaka. Sasa tunaweza kuishi hivyo kwa kumfuata Roho na si kwa jinsi ya udhaifu wa kibinadamu.
5 Watu wanaoishi kwa kufuata udhaifu wa kibinadamu[b] huyafikiri yale wanayoyataka tu. Lakini wale wanaoishi kwa kumfuata Roho huyafikiri yale Roho anayotaka wafanye. 6 Ikiwa fikra zenu zinaongozwa na udhaifu wa kibinadamu, kuna kifo cha kiroho. Lakini ikiwa fikra zenu zinaongozwa na Roho, kuna uhai na amani. 7 Je, hili ni kweli? Kwa sababu kila mtu ambaye fikra zake zinaongozwa na udhaifu wa kibinadamu yuko kinyume na Mungu maana hukataa kuitii sheria ya Mungu. Na kwa hakika hawawezi kutii. 8 Wale wanaotawaliwa na udhaifu wa kibinadamu hawawezi kumpendeza Mungu.
9 Lakini ninyi hamtawaliwi na udhaifu wenu wa kibinadamu, bali mnatawaliwa na Roho, ikiwa Roho huyo wa Mungu anakaa ndani yenu. Na mtu yeyote asiye na Roho wa Kristo, huyo si wa Kristo. 10 Miili yenu inaelekea kifo kwa sababu ya dhambi. Lakini ikiwa Kristo anaishi ndani yenu, basi Roho anawapa uzima kwa sababu ya uaminifu wa wema wa Mungu.[c] 11 Mungu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu. Na ikiwa Roho wa Mungu anaishi ndani yenu, ataifanya hai tena miili yenu inayokufa. Ndiyo, Mungu ndiye aliyemfufua Kristo kutoka kwa wafu, naye atawafufua ninyi na kuwapa uzima kupitia Roho wake anayeishi ndani yenu.
12 Hivyo, kaka na dada zangu, ni lazima tusitawaliwe na udhaifu wa kibinadamu kwa kufuata tamaa zake. 13 Ikiwa mtayatumia maisha yenu kufanya yale ambayo udhaifu wenu wa kibinadamu unataka, mtakufa kiroho. Lakini ikiwa mtaupokea msaada wa Roho na mkaacha kutenda mambo mabaya mnayotenda na miili yenu, mtakuwa na uzima wa kweli.
14 Watoto wa kweli wa Mungu ni wale wanaokubali kuongozwa na Roho wa Mungu. 15 Roho tuliyempokea si roho anayetufanya kuwa watumwa tena na kutusababisha tuwe na hofu. Roho tuliye naye hutufanya tuwe watoto waliochaguliwa na Mungu. Na kwa Roho huyo twalia “Aba,[d] yaani Baba.” 16 Na Roho mwenyewe huzungumza na roho zetu na kutuhakikishia kuwa sisi ni watoto wa Mungu. 17 Nasi kwa kuwa ni watoto wa Mungu, basi sisi ni warithi, warithi wa Mungu na warithi pamoja na Kristo. Mungu atatupa yale yote aliyompa Kristo. Sisi tunaoteseka sasa kama Kristo alivyoteseka tutashiriki katika utukufu wake.
Wakati Wetu wa Utukufu Unakuja
18 Nanayachukulia mateso ya sasa kuwa si kitu ukilinganisha na utukufu mkuu tunaoutarajia. 19 Hata uumbaji una shauku kuu, ukisubiri kwa hamu wakati ambapo atawadhihirisha “watoto halisi wa Mungu”[e] kuwa ni na. 20 Kila alichokiumba Mungu kiliruhusiwa kuwa na mapungufu kana kwamba hakitafikia utimilifu wake. Hilo halikuwa kwa matakwa ya viumbe, lakini Mungu aliruhusu hayo yatokee kwa mtazamo wa tumaini hili: 21 kwamba uumbaji ungewekwa huru mbali na uharibifu, na kwamba kila alichokiumba Mungu kiwe na uhuru na utukufu ule ule ulio wa watoto wa Mungu.
22 Tunajua kuwa kila kitu alichoumba Mungu kimekuwa kikingoja hadi sasa katika kuugua na uchungu kama wa mwanamke aliye tayari kuzaa mtoto. 23 Siyo uumbaji tu, bali sisi pia tumekuwa tukingoja kwa kuugua na uchungu ndani yetu. Tunaye Roho kama sehemu ya kwanza ya ahadi ya Mungu. Kwa hiyo tunamngoja Mungu amalize kutufanya sisi watoto wake yeye mwenyewe. Nina maana kuwa tunasubiri kuwekwa huru kwa miili yetu. 24 Tuliokolewa ili tuwe na tumaini hili. Ikiwa tunaweza kuona kile tunachokisubiri, basi hilo siyo tumaini la kweli. Watu hawatumaini kitu ambacho tayari wanacho. 25 Lakini tunatumaini kitu tusichokuwa nacho, na hivyo tunakisubiri kwa uvumilivu.
26 Roho hutusaidia pia. Sisi ni dhaifu sana, lakini Roho hutusaidia katika udhaifu wetu. Hatujui jinsi ya kuomba kama Mungu anavyotaka, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa Mungu kwa kuungua kusikotamkika. 27 Tayari Mungu anayajua mawazo yetu ya ndani sana. Na anaelewa Roho anataka kusema nini, kwa sababu Roho huomba kwa ajili ya watu wa Mungu katika namna inayokubaliana na mapenzi ya Mungu.
28 Tunajua kwamba katika kila kitu Mungu[f] hufanya kazi ili kuwapa mema wale wanaompenda. Hawa ni watu aliowachagua Mungu, kwa sababu huo ndiyo ulikuwa mpango wake. 29 Mungu aliwajua kabla hajauumba ulimwengu. Na aliamua hao wangekuwa kama Mwanaye. Na Yesu angekuwa mzaliwa wa kwanza wa watoto wake wengi. 30 Mungu aliwakusudia wao wawe kama Mwanaye. Aliwachagua na kuwahesabia haki pamoja na Mungu. Na alipowahesabia haki, akawapa utukufu wake.
Mungu Huonesha Pendo lake Kupitia Yesu
31 Hivyo tuseme nini juu ya hili? Ikiwa Mungu yuko kwa ajili yetu, hakuna anayeweza kuwa kinyume nasi. 32 Naye alimwacha mwanae ateswe kwa ajili yetu. Mungu alimtoa Mwanaye kwa ajili yetu sisi sote. Sasa kwa kuwa tu wa Kristo, hakika Mungu atatupa mambo mengine yote. 33 Nani atakayewashitaki watu waliochaguliwa na Mungu? Hayupo! Mungu ndiye hutuhesabia haki. 34 Ni nani anaweza kuwahukumu watu wa Mungu kuwa wana hatia? Hayupo! Kristo Yesu alikufa kwa ajili yetu na alifufuliwa kutoka kwa wafu. Na sasa ameketi upande wa kulia wa Mungu na anazungumza na Mungu kwa ajili yetu. 35 Je, kuna kitu chochote kinachoweza kututenga na upendo wa Kristo? Je, ni matatizo au shida au mateso? Ikiwa hatuna chakula au mavazi au tunakabiliwa na hatari au kifo, je mambo hayo yatatutenga sisi kutoka katika upendo wake? 36 Kama Maandiko yanavyosema,
“Kwa ajili yako, tunakabiliana na kifo wakati wote.
Watu wanadhani hatuna thamani kama kondoo wanaowachinja.”(A)
37 Lakini katika shida zote hizo tuna ushindi kamili kupitia Mungu, aliyetuonyesha upendo wake. 38-39 Ndiyo, nina uhakika kuwa hakuna kitu kinachoweza kututenganisha sisi na upendo wa Mungu, si kifo, maisha, malaika, wala roho zinazotawala. Nina uhakika kuwa hakuna wakati huu, hakuna wakati ujao; hakuna mamlaka, hakuna kilicho juu yetu au chini yetu, hakuna katika ulimwengu wote ulioumbwa, kitakachoweza kututenganisha sisi na upendo wa Mungu ulioonyeshwa kwetu katika Kristo Yesu Bwana wetu.
Mungu na Wayahudi
9 Nazungumza nayi sasa kama mmojawapo niliye wa Kristo. Hivyo mnaweza kuwa na uhakika kuwa sisemi uongo. Dhamiri yangu, inayotawaliwa na Roho Mtakatifu, inakubali kwamba ninayowaambia sasa ni kweli. 2 Nimejawa na huzuni na maumivu ya moyoni yasiyokwisha 3 kwa ajili ya watu wangu. Wao ni kaka na dada zangu katika mwili. Natamani ningeweza kuwasaidia. Ningekuwa tayari pia kuomba kupokea laana ya kutengwa na Kristo kama hiyo itaweza kuwasaidia. 4 Ni Waisraeli, watoto waliochaguliwa na Mungu. Wameushuhudia utukufu wa Mungu na wanashiriki maagano aliyofanya Mungu na watu wake. Mungu aliwapa Sheria ya Musa, ibada ya Hekalu, na ahadi zake. 5 Ni wazaliwa wa mababa zetu wakuu, na ni familia ya kidunia ya Masihi,[g] ambaye ni Mungu aliye juu ya vyote. Yeye asifiwe milele![h] Amina.
6 Sina maana kuwa Mungu alishindwa kutimiza ahadi yake kwa Wayahudi. Lakini kwa hakika ni baadhi tu ya Waisraeli ndiyo watu wa Mungu[i]. 7 Na hivyo ni baadhi tu ya watoto wa Ibrahimu ndiyo wazaliwa wake halisi. Hivi ndivyo Mungu alimwambia Ibrahimu: “Wazaliwa wako halisi watakuwa wale waliotoka kwa Isaka.”(B) 8 Hii ina maana kuwa si watoto wote wa Ibrahimu walio watoto halisi wa Mungu. Wazaliwa halisi wa Ibrahamu ni wale wanaofanyika watoto wa Mungu kwa sababu ya agano ambalo Mungu alililiweka na Ibrahamu. 9 Hivi ndivyo Mungu alivyosema katika agano hilo: “Wakati kama huu mwaka ujao nitakujia tena, na Sara mke wako atazaa mwana.”(C)
10 Na si hivyo tu. Kitu kama hicho kilimtokea Rebeka ambaye baada ya kupata mimba ya wana wawili mapacha waliotokana na baba mmoja, baba yetu Isaka. 11-12 Ndiyo, kabla ya kuzaliwa wana hao mapacha, Mungu alimwambia Rebeka, “Mwana mkubwa atamtumikia mdogo.”(D) Hii ilikuwa kabla wavulana hawa hawajatenda jambo lolote jema au baya. Mungu alisema hivi kabla hawajazaliwa ili kwamba mvulana ambaye Mungu alimtaka atachaguliwa kutokana na mpango wa Mungu mwenyewe. Mvulana huyu alichaguliwa kwa sababu ndiye ambaye Mungu alitaka kumwita, si kwa sababu ya jambo lolote walilofanya wavulana hao. 13 Kama Maandiko yanavyosema, “Nilimpenda Yakobo lakini nilimchukia Esau.”(E)
14 Namsikia mtu akiuliza, “Hivyo hii ina maana gani? Je, Mungu si mwenye haki?” Hapana! 15 Mungu alimwambia Musa, “Nitampa rehema yeyote ninayetaka kumpa rehema. Nitamhurumia yeyote ninayemchagua.”(F) 16 Hivyo Mungu atamchagua yeyote anayeamua kumpa rehema pasipo kujali watu wanataka nini ama kwa jinsi gani wanapiga mbio. 17 Katika Maandiko Mungu anamwambia Farao: “Nilikuweka uwe mfalme kwa kusudi hili hasa: kuonesha nguvu zangu kupitia kwako. Nilitaka jina langu litangazwe ulimwenguni kote”(G) 18 Hivyo Mungu huwarehemu wale anaotaka kuwarehemu na huwafanya jeuri wale anaotaka wawe jeuri.
19 Hivyo utaniuliza, “Ikiwa unayosema ni kweli, kwa nini Mungu amlaumu mtu yeyote kwa kufanya makosa? Hayupo anayeweza kukataa kufanya yale anayotaka Mungu, Je, yupo?” 20 Hilo si la kuuliza. Wewe ni mwanadamu tu na huna haki ya kumhoji Mungu. Chungu hakiwezi kumhoji aliyekifinyanga. Hakiwezi kusema, “Kwa nini ulinifinyanga hivi?” 21 Yeye aliyefinyanga chungu anaweza kufinyanga kitu chochote anachotaka. Anautumia udongo ule ule wa mfinyanzi kufinyanga vitu mbalimbali. Anaweza kufinyanga kitu kimoja kwa makusudi maalumu na kingine kwa matumizi ya kila siku.
22 Ni kwa jinsi hiyo hiyo Mungu amefanya. Alitaka kuionesha hasira yake na kuwafanya watu waone nguvu zake. Lakini kwa uvumilivu wake aliwastahimili wale waliomuudhi, watu waliokuwa tayari kuangamizwa. 23 Alingoja kwa uvumilivu ili aweze kuutangaza utajiri wa utukufu wake kwa watu aliowachagua wapokee rehema zake. Mungu alikwisha waandaa kuushiriki utukufu wake. 24 Sisi ndiyo watu hao, ambao Mungu alituchagua si tu kutoka kwa Wayahudi lakini pia kutoka kwa wale wasio Wayahudi. 25 Kama Mungu anavyosema katika kitabu cha Hosea,
“Watu wasiokuwa wangu,
nitasema ni watu wangu.
Na watu ambao sikuwapenda,
nitasema ni watu ninaowapenda.(H)
26 Na pale Mungu aliposema zamani:
‘Ninyi si watu wangu’;
hapo wataitwa watoto wa Mungu aliye hai.”(I)
27 Na Isaya huililia Israeli:
“Wako watu wengi sana wa Israeli,
kuliko mchanga ulio pwani ya baharini.
Lakini wachache wao watakaookolewa.
28 Ndiyo, Bwana atakamilisha kwa haraka
aliyosema atayafanya duniani.”(J)
29 Ni kama vile alivyosema Isaya:
“Ikiwa Bwana Mwenye Uweza wote
asingewaruhusu watu wachache wakaishi,
tungekuwa tumeangamizwa kabisa,
kama vile miji miovu ya Sodoma, na Gomora.”(K)
30 Hivyo haya yote yanamaanisha nini? Je, tunasema kwamba watu wasio Wayahudi walifanikiwa kukipata kibali cha Mungu, hata kama hawakuwa wakijaribu kukipata kibali hicho? Ndiyo. Walipata kibali hicho kwa sababu ya imani kwa Mungu. 31 Na vipi kuhusu watu wa Israeli? Wao walitaka kujipatia kibali cha Mungu kwa kuifuata sheria. Je, tunasema kuwa hawakufanikiwa? 32 Ndiyo, na sababu yake ni hii: Walijitahidi kukipata kwa kufanya kwa usahihi mambo yote yaliyoamriwa katika sheria badala ya kumtumaini Mungu. Walijikwaa kwenye jiwe linalowafanya watu waanguke. 33 Maandiko yanazungumza kuhusu jiwe hilo:
“Tazama, ninaweka jiwe katika Sayuni litakalowafanya watu wajikwae.
Ni mwamba utakaowaangusha watu.
Lakini yeyote atakayemtumaini yeye
hataaibika kamwe.”(L)
10 Kaka na dada zangu, ninalotamani zaidi ni kwamba Waisraeli wote waokolewe. Hayo ndiyo maombi yangu kwa Mungu. 2 Naweza kusema hili juu yao: Kwa hakika wana bidii sana ya kumtii Mungu, lakini hawaijui njia iliyo sahihi. 3 Hawakuelewa kile ambacho Mungu alifanya ili kuwaokoa watu. Hivyo walijaribu kwa njia yao wenyewe kupata kibali kwa Mungu kwa kuishika sheria. Na wakakataa kuifuata njia ya Mungu ya kuwaokoa watu. 4 Sheria ilifikia mwisho wake wakati Kristo alipolikamilisha kusudi lake. Sasa kila mtu anayeiweka imani yake kwake anahesabiwa haki mbele za Mungu.
5 Musa anaandika juu ya kuhesabiwa haki kwa kuifuata sheria. Anasema: “Ili kupata uzima katika sheria imempasa mtu kuzitii.”(M) 6 Lakini Maandiko yanasema haya kuhusu kuhesabiwa haki kwa njia ya imani: “Usiyaseme haya kwako wewe mwenyewe, ‘Nani atapanda kwenda mbinguni?’” (Hii inamaanisha “Nani atapanda mbinguni kumchukua Kristo na kumleta chini duniani?”) 7 “Na usiseme, ‘Nani atashuka hadi ulimwengu uliopo chini huko?’” (Hii inamaanisha “Nani atashuka chini na kumchukua Kristo na kumfufua kutoka mauti?”)
8 Hivi ndivyo Maandiko yanavyosema: “Mafundisho ya Mungu yako karibu nawe; yako katika kinywa chako na katika moyo wako.”(N) Ni mafundisho ya imani tunayowaambia watu. 9 Ukikiri wazi kwa kinywa chako, kwamba “Yesu ni Bwana” na kuamini moyoni mwako kuwa Mungu alimfufua kutoka mauti, utaokolewa. 10 Ndiyo, tunamwamini Yesu mioyoni mwetu, na Mungu hutukubali kuwa wenye haki. Na tunakiri wazi wazi kwa vinywa vyetu kwamba tunamwamini Mungu na yeye anatuokoa.
11 Ndiyo, Maandiko yanasema, “Yeyote anayemwamini hataaibika.”(O) 12 Yanasema hivi kwa sababu hakuna tofauti kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi. Bwana yule yule ndiye Bwana wa watu wote. Naye humbariki sana kila amwombaye akitaka msaada. 13 Ndiyo, “kila mtu anayemwita Bwana[j] ili kupata msaada, ataokolewa.”[k]
14 Lakini watu watawezaje kumwita Bwana na kupata msaada wake ikiwa hawamwamini yeye? Na watawezaje kumwamini Bwana ikiwa hawajawahi kuzisikia habari zake? Na watawezaje kuzisikia habari zake ikiwa hayupo mtu wa kuwaambia? 15 Na mtu atawezaje kwenda na kuwaambia habari hizo ikiwa hajatumwa? Haya, hii ndiyo sababu Maandiko yanasema, “Ni jambo la kufurahisha kumwona mtu anayepeleka Habari Njema!”(P)
16 Lakini si watu wote walizipokea Habari Njema hizo. Na hii ndiyo sababu Isaya alisema, “Bwana, nani aliyeamini yale tuliyowaeleza?”(Q) 17 Kwa hiyo imani hupatikana kutokana na kusikia Habari Njema. Na watu husikia Habari Njema wakati mtu anapowaeleza kuhusu Kristo.
18 Lakini nauliza, “Je, watu hao walizisikia Habari Njema?” Ndio Kwa kweli walizisikia kama Maandiko yanavyosema,
“Sauti zao zilitoka na kuenea duniani kote.
Maneno yao yakaenda kila mahali ulimwenguni.”(R)
19 Lakini tena nauliza, “Je, watu wa Israeli hawakuelewa?” Ndiyo, walielewa. Musa alikuwa wa kwanza kujibu swali hili. Na anasema haya kwa ajili ya Mungu:
“Nitawatumia wale ambao siyo Taifa halisi ili liwafanye muone wivu.
Nitalitumia taifa ambalo halielewi ili mkasirike.”(S)
20 Kisha Isaya ana ujasiri wa kutosha kusema haya kwa ajili ya Mungu:
“Watu walionipata mimi hawakuwa wakinitafuta.
Nilijitambulisha kwa watu ambao hawakuwa wakinitafuta.”(T)
21 Lakini kuhusu watu wa Israeli Mungu anasema,
“Kutwa nzima nilisimama nikiwa tayari kuwakubali watu hawa,
lakini ni wakaidi na wamekataa kunitii.”(U)
© 2017 Bible League International