Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Beginning

Read the Bible from start to finish, from Genesis to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Warumi 1-3

Salamu kutoka kwa Paulo, mtumishi wa Kristo Yesu.[a]

Mungu alinichagua niwe mtume na akanipa kazi ya kuhubiri Habari Njema yake. Tangu zamani, kwa vinywa vya manabii katika Maandiko Matakatifu, Mungu aliahidi kwamba angewaletea Habari Njema watu wake. Habari Njema hii inahusu Mwana wa Mungu, ambaye kama mwanadamu, alizaliwa katika ukoo wa Mfalme Daudi. Na alipofufuliwa na Roho Matakatifu[b] kutoka kwa wafu, alipewa mamlaka kamili ya kutawala kama Mwana wa Mungu. Ni Yesu Kristo, Bwana wetu.

Kupitia kwa Yesu, Mungu amenionyesha wema wake. Na amenipa mamlaka ya kuwaendea watu wa mataifa yote na kuwaongoza kumwamini na kumtii yeye. Kazi yote hii ni kwa ajili yake. Nanyi pia ni miongoni mwa waliochaguliwa na Mungu ili mmilikiwe na Yesu Kristo.

Waraka huu ni kwa ajili yenu ninyi nyote mlio huko Rumi. Kwani Mungu anawapenda na amewachagua kuwa watu wake watakatifu.

Ninamwomba Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo, wawape ninyi neema na amani.

Maombi ya Shukrani

Kwanza, ninamshukuru Mungu wangu kupitia Yesu Kristo kwa ajili yenu ninyi nyote. Ninamshukuru yeye kwa sababu kila mahali ulimwenguni watu wanazungumza kuhusu imani yenu kuu. 9-10 Kila wakati ninapoomba, ninawakumbuka ninyi daima. Mungu anajua kuwa hii ni kweli. Yeye ndiye ninayemtumikia kwa moyo wangu wote nikiwaambia watu Habari Njema kuhusu Mwanaye. Hivyo ninaendelea kuomba kwamba mwishowe Mungu atanifungulia njia ili niweze kuja kwenu. 11 Ninataka sana niwaone na niwape zawadi ya kiroho ili kuimarisha imani yenu. 12 Ninamaanisha kuwa ninataka tusaidiane sisi kwa sisi katika imani tuliyo nayo. Imani yenu itanisaidia mimi, na imani yangu itawasaidia ninyi.

13 Kaka zangu na dada zangu, ninataka mjue kwamba nimepanga mara nyingi kuja kwenu, lakini jambo fulani hutokea na kubadili mipango yangu kila ninapopanga kuja. Juu ya kazi yangu miongoni mwenu, ningependa kuona matokeo yale yale mazuri yakitokea ya kazi yangu miongoni mwa watu wengine wasio Wayahudi.

14 Imenilazimu kuwatumikia watu wote; waliostaarabika na wasiostaarabika,[c] walioelimika na wasio na elimu. 15 Ndiyo sababu ninataka sana kuzihubiri Habari Njema kwenu ninyi pia mlio huko Rumi.

16 Kwa mimi hakuna haya[d] katika kuhubiri Habari Njema. Ninayo furaha kwa sababu Habari Njema ni nguvu ya Mungu inayomwokoa kila anayeamini, yaani inawaokoa Wayahudi kwanza, na sasa inawaokoa Mataifa.[e] 17 Ndiyo, wema wa uaminifu wa Mungu umedhihirishwa katika Habari Njema kwa uaminifu wa mmoja, ambao huongoza imani ya wengi. Kama Maandiko yanavyosema, “Aliye na haki mbele za Mungu[f] ataishi kwa imani.”[g]

Mungu ni Mwaminifu Na Atauadhibu Uovu

18 Mungu huonesha hasira yake kutokea mbinguni dhidi ya mambo mabaya ambayo waovu hutenda. Hawamheshimu na wanatendeana mabaya. Maisha yao maovu yanasababisha ukweli kuhusu Mungu usijulikane. 19 Hili humkasirisha Mungu kwa sababu wamekwisha oneshwa Mungu alivyo. Ndiyo, Mungu ameliweka wazi kwao.

20 Yapo mambo yanayoonekana kuhusu Mungu, kama vile nguvu zake za milele na yale yote yanayomfanya awe Mungu. Lakini tangu kuumbwa kwa ulimwengu, mambo haya yamekuwa rahisi kwa watu kuyaona. Maana yake ni kuwa, watu wanaweza kumwelewa Mungu kwa kuangalia yale aliyoumba. Hivyo watu hawana udhuru kwa uovu wanaotenda.

21 Watu walimjua Mungu, lakini hawakumheshimu kama Mungu. Na hawakumpa shukrani. Badala yake waliyageukia mambo ya hovyo yasiyo na manufaa. Akili zao zilichochanganyikiwa zilijaa giza. 22 Walisema kuwa wana hekima, lakini wakawa wajinga. 23 Hawakuuheshimu ukuu wa Mungu, anayeishi milele. Wakaacha kumwabudu Mungu wakaanza kuabudu sanamu, vitu vilivyotengenezwa vikaonekana kama wanadamu, ambao wote mwisho hufa, au kwa mfano wa ndege na wanyama wanaotembea na wanaotambaa.

24 Hivyo Mungu akawaacha wazifuate tamaa zao chafu. Wakawa najisi na wakaivunjia heshima miili yao kwa njia za uovu walizotumia. 25 Waliibadili kweli kuhusu Mungu kwa uongo. Wakasujudu na kuabudu vitu alivyoviumba Mungu badala ya kumwabudu Mungu aliyeviumba vitu hivyo. Yeye ndiye anayepaswa kusifiwa milele yote. Amina.

26 Hivyo, kwa kuwa watu hawakumheshimu Mungu, Mungu akawaacha wafuate tamaa zao za aibu. Wanawake wao wakabadili namna ya kujamiiana na wakawatamani wanawake wenzao na wakajamiiana wao kwa wao. 27 Wanaume wakafanya vivyo hivyo. Wakaacha kujamiiana na wanawake kwa mfumo wa asili, wakaanza kuwawakia tamaa wanaume wenzao. Wakafanya mambo ya aibu na wanaume na wavulana. Wakajiletea aibu hii juu yao wenyewe, wakapata yale waliyostahili kwa kutelekeza kweli.

28 Watu hawa waliona kuwa haikuwa muhimu kwao kumkubali Mungu katika fikra zao. Hivyo Mungu akawaacha wayafuate mawazo yao mabaya. Hivyo hufanya mambo ambayo mtu yeyote hapaswi kufanya. 29 Maisha yao yamejaa kila aina ya matendo mabaya, uovu, tamaa na chuki. Wamejaa wivu, uuaji, ugomvi, uongo na hamu ya kuwadhuru wengine. Wanasengenya 30 na kusemana maovu wao wenyewe. Wanamchukia Mungu. Ni wakorofi, wana kiburi na hujivuna. Hubuni njia za kufanya maovu. Hawawatii wazazi wao. 31 Ni wapumbavu, hawatimizi ahadi zao. Hawawaoneshi wema wala huruma wengine. 32 Wanajua amri ya Mungu kuwa yeyote anayeishi kwa namna hiyo lazima afe. Lakini si tu kwamba wanaendelea kufanya mambo haya wenyewe, bali wanakubaliana na wengine wanaofanya mambo hayo.

Huwezi Kuwahukumu Wengine

Je, unadhani unaweza kuwahukumu watu wengine? Unakosea. Wewe pia una hatia ya dhambi. Unawahukumu kwa kuwa wanatenda mabaya, lakini wewe unatenda yale wanayotenda. Hivyo unapowahukumu, unajihukumu wewe mwenyewe. Lakini tunajua kwamba Mungu yuko sahihi kwa kuwahukumu wote wanaotenda mambo ya jinsi hiyo! Lakini kwa kuwa unatenda mambo sawa na wale unaowahukumu, hakika unaelewa kuwa Mungu atakuadhibu nawe pia. Unawezaje kufikiri kuwa utaiepuka hukumu yake? Mungu amekuwa mwema kwako. Na amekuwa mvumilivu sana, akisubiri ubadilike. Lakini haufikirii jambo lolote kuhusu wema wake mkuu. Pengine huelewi kwamba Mungu ni mwema kwako ili ubadili moyo na maisha yako.

Lakini wewe ni mkaidi sana! Unakataa kubadilika. Hivyo unaikuza hukumu yako wewe mwenyewe zaidi na zaidi. Utahukumiwa siku ile ambapo Mungu ataonesha hasira yake. Siku ambayo kila mtu ataona Mungu anavyowahukumu watu kwa haki.[h] Kama anavyosema, “Atamlipa au kumwadhibu kila mtu kutokana na matendo yale.”(A) Watu wengine hawachoki kutenda mema. Wanaishi kwa ajili ya utukufu na heshima kutoka kwa Mungu na kwa ajili ya maisha yasiyoweza kuharibiwa. Mungu atawapa watu hao uzima wa milele. Lakini wengine hutenda mambo yanayowafurahisha wao wenyewe. Hivyo hukataa yaliyo haki na huchagua kutenda mabaya. Watateseka kwa hukumu ya Mungu yenye hasira. Matatizo na mateso yatampata kila mmoja anayetenda uovu; kuanzia Wayahudi kwanza kisha wale wasio Wayahudi. 10 Lakini atampa utukufu, heshima na amani kila atendaye mema; wale wote wanaotenda mema; kuanzia Wayahudi kwanza kisha wale wasio Wayahudi. 11 Ndiyo, Mungu humhukumu kila mtu pasipo upendeleo, bila kujali yeye ni nani.

12 Watu walio na sheria na wote ambao hawajawahi kuisikia sheria, wote wako sawa wanapotenda dhambi. Watu wasio na sheria na ni watenda dhambi wataangamizwa. Vivyo hivyo, wale walio na sheria na ni watenda dhambi watahukumiwa kuwa na hatia kwa kutumia sheria. 13 Kuisikia sheria hakuwafanyi watu wawe wenye haki kwa Mungu. Wanakuwa wenye haki mbele zake, pale wanapotekeleza kile kinachoagizwa na sheria.

14 Fikirini kuhusu wasio Wahayudi ambao hawakukua wakiwa na sheria. Wanapotenda kama sheria inavyoamuru,[i] wanakuwa kielelezo cha sheria, ijapokuwa hawana sheria iliyoandikwa. 15 Wanaonesha kuwa wanafahamu kilicho sahihi na kibaya, kama sheria inavyoamuru na dhamiri zao zinakubali. Lakini wakati mwingine mawazo yao huwaambia kuwa wamekosea au wamefanya sahihi. 16 Hivi ndivyo itakavyokuwa siku ambayo Mungu atazihukumu siri za watu kupitia Yesu Kristo, sawasawa na Habari Njema ninayoihubiri.

Wayahudi na Sheria

17 Wewe unajiita Myahudi, na unajiona upo salama kwa kuwa tu una sheria. Kwa majivuno unadai kuwa wewe ni mmoja wa wateule wa Mungu. 18 Unajua yale ambayo Mungu anataka ufanye. Na unajua yaliyo muhimu, kwa sababu umejifunza sheria. 19 Unadhani kuwa wewe ni kiongozi wa watu wasioweza kuiona njia sahihi, na nuru kwa wale walio gizani. 20 Unafikiri unaweza kuwaonesha wajinga kilicho sahihi. Na unadhani kuwa wewe ni mwalimu wa wanaoanza kujifunza. Unayo sheria, na hivyo unadhani unajua kila kitu na una kweli yote. 21 Unawafundisha wengine, sasa kwa nini usijifundishe wewe wenyewe? Unawaambia usiibe, lakini wewe mwenyewe unaiba. 22 Unasema wasizini, lakini wewe mwenyewe una hatia ya dhambi hiyo. Unachukia sanamu, lakini unaziiba sanamu katika mahekalu yao. 23 Unajivuna sana kwamba una sheria ya Mungu, lakini unamletea Mungu aibu kwa kuivunja sheria yake. 24 Kama Maandiko yanavyosema, “Watu wa mataifa mengine wanamtukana Mungu kwa sababu yako.”[j]

25 Ikiwa mnaifuata sheria, basi kutahiriwa kwenu kuna maana. Lakini mkiivunja sheria, mnakuwa kama watu ambao hawakutahiriwa. 26 Wale wasiokuwa Wayahudi hawatahiriwi. Lakini wakiifuata sheria inavyosema, wanakuwa kama watu waliotahiriwa. 27 Mnayo sheria na tohara, lakini mnaivunja sheria. Hivyo wale wasiotahiriwa katika miili yao, lakini bado wanaitii sheria, wataonesha kuwa mna hatia.

28 Wewe si Myahudi halisi ikiwa utakuwa Myahudi tu kwa nje. Tohara halisi si ile ya nje ya mwili tu. 29 Myahudi halisi ni yule aliye Myahudi kwa ndani. Tohara halisi inafanywa moyoni. Ni kitu kinachofanywa na Roho, na hakifanyiki ili kufuata sheria iliyoandikwa. Na yeyote aliyetahiriwa moyoni kwa Roho hupata sifa kutoka kwa Mungu, siyo kutoka kwa watu.

Je, Wayahudi wana upendeleo wowote kuliko wengine? Je, tohara yao inawasaidia lolote jema? Ndiyo, Wayahudi wana upendeleo mwingi. Lililo muhimu zaidi ni kuwa: Mungu aliwaamini akawapa kazi ya kuzitangaza ahadi zake kwa watu wote. Ni kweli kuwa baadhi ya Wayahudi hawakuwa waaminifu kufanya yale Mungu aliyotaka. Lakini je, hilo laweza kumzuia Mungu kutenda kwa uaminifu yale aliyoahidi? Hapana! Hata ikiwa wengine wote watashindwa kutimiza ahadi zao, daima, Mungu atatekeleza aliyosema. Kama Maandiko yanavyosema kuhusu Mungu,

“Utathibitika kuwa mwenye haki kwa maneno yako,
    na utashinda utakaposhitakiwa na watu.”(B)

Lakini hivi ndivyo wengine hufikiri: Tunapotenda mabaya, inaonesha wazi kuwa Mungu ni wa haki. Je, tunaweza kusema kwamba Mungu hatutendei haki anapotuadhibu? Hapana. Ikiwa Mungu si wa haki atawezaje kuuhukumu ulimwengu?

Ninaposema uongo, inamletea Mungu utukufu, kwa sababu uongo wangu hurahisisha ionekane kuwa yeye ni wa kweli. Hivyo kwa nini nihukumiwe kama mtenda dhambi? Na kwa nini tusiseme, “Tufanye maovu ili jambo jema litokee humo.” Baadhi ya watu wanadai kuwa hivyo ndivyo tunavyofundisha! Wahukumiwe kwa kusema hivyo.

Je, sisi Wayahudi ni bora kuliko wengine? Hapana, nimekwishaonyesha kuwa watu wote, wawe Wayahudi au wasio Wayahudi, wako chini ya nguvu ya dhambi.

Watu Wote Wana Hatia

10 Kama Maandiko yanavyosema,

“Hakuna atendaye haki,
    hakuna hata mmoja.
11 Hakuna hata mmoja anayeelewa,
    hakuna anayetaka kumfuata Mungu.
12 Wote wamegeuka na kumwacha,
    na hawana manufaa kwa yeyote.
Hakuna atendaye mema,
    hakuna hata mmoja.”(C)
13 “Maneno yao ni ya hatari kama kaburi lililo wazi.
    Wanatumia ndimi zao kwa kusema uongo.”(D)
“Maneno yao ni kama sumu ya nyoka.”(E)
14     “Midomo yao imejaa maneno ya laana na hasira.”(F)
15 “Nyakati zote wako tayari kuua mtu.
16     Kila wanakokwenda wanasababisha matatizo na uharibifu.
17 Hawajui jinsi ya kuishi kwa amani.”(G)
18     “Hawamheshimu wala kumcha Mungu.”(H)

19 Tunajua ya kwamba, kile ambacho sheria inasema ni kwa ajili ya wale waliopewa sheria. Hii inamaanisha kuwa watu wote, Wayahudi na wasio Wayahudi, hawana udhuru kwa matendo yao. Hivyo ulimwengu wote unasimama mbele za Mungu na lazima ujibu kwake. 20 Kwa sababu kufuata sheria hakumfanyi mtu akahesabiwa haki mbele za Mungu.[k] Sheria inatuonyesha dhambi zetu tu.

Mungu Anavyowafanya Watu Kuwa Wenye Haki

21 Lakini sasa Mungu ametuonesha jinsi alivyo mwema na mwaminifu. Alivyofanya haihusiani na sheria ingawa sheria na manabii walisema kuwa haya yangetokea. 22 Uaminifu wa wema wa Mungu umedhihirishwa kwetu kupitia imani katika[l] Yesu Kristo. Hufanya hivi kwa wote wanaomwamini Kristo. Kwa sababu kwa Mungu watu wote ni sawa. 23 Ndiyo, watu wote wametenda dhambi na wameshindwa kufikia kiwango cha utukufu wa Mungu kilichokusudiwa kwao. 24 Mungu ameamuru sisi sote tufunguliwe kutoka dhambini. Zawadi hii ya neema yake imekuja kwetu kupitia kile ambacho Kristo Yesu alikifanya ili tuwe huru. 25-26 Mungu alimtoa Yesu kama njia ya kusamehe dhambi za watu kupitia imani katika yeye. Mungu anasamehe watu kwa sababu sadaka ya damu ya Yesu iliwaweka huru na dhambi zao. Mungu alimtoa Yesu kuonesha kuwa hutenda haki na bila upendeleo. Alikuwa sahihi huko nyuma alipovumilia na hakuwaadhibu watu kwa sababu ya dhambi zao. Na katika wakati wetu bado anatenda haki. Mungu alifanya hili ili awahukumu watu pasipo kuwa na upendeleo na kumwesabia haki mtu yeyote aliye na imani katika Yesu.

27 Hivyo, sisi Wayahudi tuna nini cha kujivunia? Hatuna kitu. Mungu amefunga mlango kuzuia nje kiburi cha Kiyahudi. Sheria gani husema hivyo? Sheria inayohimiza matendo? Hapana, ni sheria inayosisitiza imani. 28 Ninamaanisha kuwa watu hufanyika wenye haki na kukubaliwa na Mungu kwa njia ya imani,[m] siyo kwa sababu ya yale wanayotenda ili kuifuata sheria. Hili ndilo tunaloamini. 29 Je, mnadhani kuwa Mungu ni Mungu wa Wayahudi tu? Je, yeye si Mungu wa watu wengine pia? Ndiyo, yeye ni Mungu wa wasio Wayahudi pia. 30 Kuna Mungu mmoja tu. Atawahesabia haki Wayahudi[n] kwa imani yao, na atawahesabia haki wasio Wayahudi[o] kwa imani yao. 31 Je, mnadhani kuwa tunaondoa sheria na kuweka imani hii? Hapana! Kwa kuifuata njia ya imani tunafanya kilichokusudiwa na sheria.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International