Beginning
Baadhi ya Wayahudi Wamshitaki Paulo
24 Siku tano baadaye Anania, kuhani mkuu, alikwenda mjini Kaisaria. Aliwachukua pamoja naye baadhi ya viongozi wa wazee wa Kiyahudi na mwanasheria aitwaye Tertulo. Walikwenda Kaisaria kutoa ushahidi dhidi ya Paulo mbele ya gavana. 2-3 Paulo aliitwa kwenye mkutano, na Tertulo akaanza kueleza mashitaka.
Tertulo alisema, “Mheshimiwa Feliki, kwa muda mrefu watu wetu wamefurahia amani kwa sababu yako, na mambo mengi mabaya katika nchi yetu yanarekebishwa kutokana na msaada wako wa hekima. Kwa hili sisi sote tunaendelea kushukuru. 4 Lakini sitaki kuchukua muda wako mwingi. Hivyo nitasema maneno machache. Tafadhali uwe mvumilivu. 5 Mtu huyu ni mkorofi. Anasababisha vurugu kwa Wayahudi kila mahali ulimwenguni. Ni kiongozi wa kundi la Wanazorayo. 6-8 Pia, alikuwa anajaribu kulinajisi Hekalu, lakini tulimsimamisha.[a] Unaweza kuamua ikiwa haya yote ni kweli. Mwulize maswali wewe mwenyewe.” 9 Wayahudi wengine wakakubali na kusema ndivyo ilivyo.
Paulo Ajitetea Mbele ya Feliki
10 Gavana alifanya ishara ili Paulo aanze kuzungumza. Hivyo Paulo alijibu, “Gavana Feliki, ninafahamu kuwa umekuwa jaji wa nchi hii kwa muda mrefu. Hivyo ninafurahi kujitetea mimi mwenyewe mbele yako. 11 Nilikwenda kuabudu Yerusalemu siku kumi na mbili tu zilizopita. Unaweza kutambua wewe mwenyewe kuwa hii ni kweli. 12 Wayahudi hawa wanaonishitaki, hawakuniona nikibishana na mtu yeyote wala kukusanya kundi la watu Hekaluni. Na sikuwa nabishana au kufanya vurugu kwenye masinagogi au mahali popote katika mji. 13 Watu hawa hawawezi kuthibitisha mambo wanayoyasema dhidi yangu sasa.
14 Lakini nitakuambia hili: Ninamuabudu Mungu, Mungu yule yule aliyeabudiwa na baba zetu, na kama mfuasi wa Njia, ambayo wayahudi hawa wanasema si njia sahihi. Na ninaamini kila kitu kinachofundishwa katika Sheria ya Musa na yote yaliyoandikwa katika vitabu vya manabii. 15 Nina tumaini katika Mungu kama walilonalo Wayahudi hawa, kwamba watu wote, wema na wabaya, watafufuliwa kutoka kwa wafu. 16 Hii ndiyo sababu daima nimejaribu kufanya kile ninachoamini kuwa sahihi mbele za Mungu na kila mtu.
17-18 Nimekuwa mbali na Yerusalemu kwa miaka mingi. Nilikwenda kule nikiwa na fedha za kuwasaidia watu wangu. Pia nilikuwa na sadaka za kutoa Hekaluni. Nilipokuwa nafanya hivyo, baadhi ya Wayahudi waliponiona pale. Nilikuwa nimemaliza ibada ya utakaso.[b] Sikufanya vurugu yoyote, na hakuna watu waliokuwa wamekusanyika kunizunguka. 19 Lakini baadhi ya Wayahudi kutoka Asia walikuwa pale. Walipaswa kuwa hapa mbele yako wakinishtaki ikiwa wana ushahidi kuwa nilifanya kitu chochote kibaya. 20 Waulize watu hawa ikiwa waliona kosa lolote kwangu niliposimama mbele ya mkutano wa baraza kuu mjini Yerusalemu. 21 Jibu pekee watakaloweza kukujibu ni hili: Kwamba nilipokuwa mbele zao nilipaza sauti na kusema, ‘Mnanishitaki leo kwa sababu ninaamini watu watafufuka kutoka kwa wafu!’”
22 Feliki tayari alikuwa anaelewa mengi kuhusu Njia. Akasimamisha kesi na kusema, “Kamanda Lisiasi atakapokuja hapa, nitaamua nini cha kufanya.” 23 Feliki alimwambia ofisa wa jeshi kumlinda Paulo lakini wampe uhuru kiasi na wawaruhusu rafiki zake wamletee chochote atakachohitaji.
Paulo Azungumza na Feliki na Mkewe
24 Baada ya siku chache, Feliki alikuja na mke wake Drusila, aliyekuwa Myahudi. Feliki akaagiza Paulo apelekwe kwake. Alimsikiliza Paulo akiongea kuhusu kumwamini Yesu Kristo. 25 Lakini Feliki aliogopa Paulo alipoongelea kuhusu vitu kama kutenda haki, kuwa na kiasi, na hukumu itakayokuja baadaye. Akasema, “Unaweza kwenda sasa. Nitakapokuwa na muda mwingi, nitakuita.” 26 Lakini Feliki alikuwa na sababu nyingine ya kuzungumza na Paulo. Alitegemea Paulo angempa rushwa, hivyo alimwita Paulo mara nyingi na kuzungumza naye.
27 Lakini baada ya miaka miwili, Porkio Festo akawa gavana. Hivyo Feliki hakuwa gavana tena. Lakini alimwacha Paulo gerezani ili kuwaridhisha Wayahudi.
Paulo Aomba Kumwona Kaisari
25 Festo akawa gavana na siku tatu baadaye akasafiri kwenda Yerusalemu kutoka Kaisaria. 2 Viongozi wa makuhani na viongozi maarufu wa Kiyahudi wakatoa mashitaka dhidi ya Paulo mbele ya Festo. 3 Walimwomba Festo awasaidie. Walitaka amrudishe Paulo Yerusalemu kwa sababu walipanga kumwua akiwa njiani. 4 Lakini Festo alijibu, “Hapana, Paulo ataendelea kuwekwa Kaisaria. Nitaenda huko mimi mwenyewe hivi karibuni, 5 na viongozi wenu wanaweza kufuatana nami. Kama mtu huyu hakika amefanya chochote kibaya, wanaweza kumshitaki huko.”
6 Festo alikaa Yerusalemu kwa siku nane au kumi zaidi kisha alirudi Kaisaria. Siku iliyofuata Festo akawaambia askari wamlete Paulo mbele yake. Festo alikuwa amekaa kwenye kiti cha hukumu. 7 Paulo aliingia kwenye chumba na Wayahudi waliokuja kutoka Yerusalemu walisimama kumzunguka. Walileta mashitaka mengi mazito dhidi yake, lakini hawakuweza kuthibitisha chochote. 8 Paulo alijitetea mwenyewe, akasema, “Sijatenda kitu chochote kibaya kinyume na sheria ya Kiyahudi, kinyume na Hekalu au kinyume na Kaisari.”
9 Lakini Festo alitaka kuwaridhisha Wayahudi. Hivyo alimwuliza Paulo, “Unataka kwenda Yerusalemu ili nikakuhukumu huko kutokana na mashitaka haya?”
10 Paulo akasema, “Kwa sasa nimesimama kwenye kiti cha hukumu cha Kaisari. Hapa ndipo ninatakiwa kuhukumiwa. Sijatenda lolote baya kwa Wayahudi na unafahamu hilo. 11 Ikiwa nilitenda chochote kibaya na sheria inasema ni lazima nife, basi ninakubali kuwa ninapaswa kufa. Siombi kuokolewa kutokana na kifo. Lakini kama mashitaka haya siyo ya kweli, basi hakuna anayeweza kunikabidhi kwa watu hawa. Hapana, Nataka Kaisari aisikilize kesi yangu!”
12 Festo alijadiliana na washauri wake kuhusu hili. Kisha akasema, “Umeomba kumwona Kaisari, basi utakwenda kwa Kaisari!”
Festo Amwuliza Mfalme Agripa Kuhusu Paulo
13 Siku chache baadaye Mfalme Agripa pamoja na dada yake aliyeitwa Bernike[c] walikuja Kaisaria kumtembelea Festo. 14 Walikaa huko kwa siku nyingi, na Festo akamwambia mfalme kuhusu kesi ya Paulo. Festo alisema, “Kuna mtu ambaye Feliki alimwacha gerezani. 15 Nilipokwenda Yerusalemu, viongozi wa makuhani na viongozi wa wazee wa Kiyahudi walitengeneza mashitaka dhidi yake. Walinitaka nimhukumu kifo. 16 Lakini niliwaambia, ‘Mtu anaposhitakiwa kuwa ametenda jambo baya, Warumi hawampeleki kwa watu wengine ili ahukumiwe. Kwanza, ni lazima aonane na watu wanaomshtaki. Na kisha ni lazima aruhusiwe kujitetea yeye mwenyewe dhidi ya mashitaka yao.’
17 Hivyo Wayahudi walipokuja hapa kwa ajili ya kesi, sikupoteza muda. Siku iliyofuata nilikaa kwenye kiti cha hukumu na kuamuru Paulo aletwe ndani. 18 Wayahudi walisimama na kumshitaki. Lakini hawakumshitaki kwa makosa niliyodhani wangemshitaki. 19 Mashitaka yao yote yalihusu dini yao wenyewe na kuhusu mtu anayeitwa Yesu. Yesu alikufa lakini Paulo anasema bado yuko hai. 20 Baada ya kuona kuwa sijui jinsi ya kuyachunguza mambo haya. Hivyo nilimwuliza Paulo, ‘Unataka kwenda Yerusalemu ili ukahukumiwe huko?’ 21 Lakini Paulo aliomba abaki mahabusu hapa Kaisaria. Anataka uamuzi kutoka kwa mfalme mkuu. Hivyo niliamua aendelee kushikiliwa hapa mpaka nitakapompeleka kwa Kaisari huko Rumi.”
22 Agripa akamwambia Festo, “Ningependa kumsikiliza mtu huyu pia.”
Festo akasema, “Utaweza kumsikiliza kesho.”
23 Siku iliyofuata Agripa na Bernike walikuja kwenye mkutano kwa fahari kubwa, wakijifanya watu wa muhimu sana. Waliingia kwenye chumba pamoja na viongozi wa kijeshi na watu maarufu wa mji. Festo akawaamuru askari wamwingize Paulo ndani.
24 Festo akasema, “Mfalme Agripa nanyi nyote mliokusanyika hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu. Wayahudi wote, hapa na Yerusalemu wamelalamika kwangu juu yake. Wanapolalamika, wanapaza sauti zao wakisema kwamba anapaswa kuuawa. 25 Nilipochunguza, sikuona ikiwa alitenda kosa lolote linalostahili hukumu ya kifo. Lakini ameomba kuhukumiwa na Kaisari, hivyo niliamua apelekwe Rumi. 26 Hata hivyo, sifahamu kwa hakika ni nini cha kumwandikia bwana wangu Kaisari kama sababu ya kumpeleka mtu huyu kwake. Hivo nimemleta mbele yenu ninyi nyote, hasa wewe, Mfalme Agripa. Ninatumaini kwamba utamwuliza maswali na kunipa kitu cha kumwandikia Kaisari. 27 Nafikiri ni upumbavu kupeleka mfungwa kwa Kaisari bila kuainisha mashitaka dhidi yake.”
Paulo Asimama Mbele ya Mfalme Agripa
26 Agripa[d] akamwambia Paulo, “Unaweza sasa kujitetea wewe mwenyewe.” Paulo akanyoosha mkono wake ili wamsikilize kwa makini na akaanza kusema. 2 “Mfalme Agripa, najisikia heshima kusimama hapa mbele yako leo ili nijibu mashitaka yote yaliyotengenezwa na Wayahudi dhidi yangu. 3 Ninafurahi kuzungumza nawe, kwa sababu unafahamu sana kuhusu desturi za Kiyahudi na mambo ambayo Wayahudi hubishana. Tafadhali uwe mvumilifu kunisikiliza.
4 Wayahudi wote wanafahamu maisha yangu yote. Wanafahamu namna nilivyoishi tangu mwanzo miongoni mwa watu mwangu na baadaye Yerusalemu. 5 Wayahudi hawa wamenifahamu kwa muda mrefu. Wakitaka wanaweza kukwambia kwamba nilikuwa Farisayo mzuri. Na Mafarisayo wanazitii sheria za dini ya Kiyahudi kwa uangalifu kuliko kundi lolote. 6 Na sasa nimeshitakiwa kwa sababu ninatumaini ahadi ambayo Mungu aliiweka kwa baba zetu. 7 Hii ni ahadi ambayo makabila yote kumi na mbili ya watu wetu yanatumaini kuipokea. Kwa sababu ya tumaini hili Wayahudi wanamtumikia Mungu usiku na mchana. Ee Mfalme wangu, Wayahudi wamenishitaki kwa sababu ninatumaini ahadi hii hii. 8 Kwa nini ninyi watu mnadhani Mungu hawezi kuwafufua watu kutoka kwa wafu?
9 Huko nyuma nilidhani kuwa ninapaswa kufanya kinyume na Yesu kutoka Nazareti kwa kadri ninavyoweza. 10 Na ndivyo nilivyofanya, kuanzia Yerusalemu. Viongozi wa makuhani walinipa mamlaka ya kuwaweka gerezani watu wa Mungu wengi. Na walipokuwa wanauawa nilikubali kuwa lilikuwa jambo zuri. 11 Nilikwenda katika masinagogi yote na kuwaadhibu, nikijaribu kuwafanya wamlaani[e] Yesu. Hasira yangu dhidi ya watu hawa ilikuwa kali sana kiasi kwamba nilikwenda katika miji mingine kuwatafuta na kuwaadhibu.
Paulo Aeleza Alivyomwona Yesu
12 Wakati fulani viongozi wa makuhani walinipa ruhusa na mamlaka kwenda katika mji wa Dameski. 13 Nikiwa njiani, mchana, niliona mwanga kutoka mbinguni, unaong'aa kuliko jua. Uling'aa kunizunguka mimi pamoja na wale waliokuwa wanasafiri pamoja nami. 14 Sote tulianguka chini. Kisha nilisikia sauti iliyozungumza nami kwa Kiaramu. Sauti ilisema, ‘Sauli, Sauli, kwa nini unanitesa? Unajiumiza wewe mwenyewe kwa kunipinga mimi.’
15 Nilisema, ‘Wewe ni nani, Bwana?’
Bwana alisema, ‘Mimi ni Yesu. Unayemtesa. 16 Simama! Nimekuchagua wewe kuwa mtumishi wangu. Utawaambia watu habari zangu, ulichoona leo na yale nitakayokuonesha. Hii ndiyo sababu nimekuja kwako. 17 Nitakulinda dhidi ya watu wako na dhidi ya watu wasio Wayahudi, ninaokutuma kwao. 18 Utawafanya waielewe kweli. Watatoka gizani na kuja kwenye mwanga. Watageuka kutoka kwenye mamlaka ya Shetani na kumgeukia Mungu. Ndipo dhambi zao zitasamehewa, na wataweza kupewa nafasi miongoni mwa watu wa Mungu, walifanywa watakatifu kwa kuniamini.’”
Paulo Aeleza Kuhusu Kazi Yake
19 Paulo aliendelea kusema: “Mfalme Agripa, baada ya kuona maono haya kutoka mbinguni, nilitii. 20 Nilianza kuwaambia watu kubadili mioyo na maisha yao na kumgeukia Mungu. Niliwaambia kufanya yale yatakayoonyesha kwamba hakika wamebadilika. Kwanza nilikwenda kwa watu waliokuwa Dameski. Kisha nikaenda Yerusalemu na kila sehemu ya Uyahudi na nikawaambia watu huko. Nilikwenda pia kwa watu wasio Wayahudi.
21 Hii ndiyo sababu Wayahudi walinikamata na kujaribu kuniua Hekaluni. 22 Lakini Mungu alinisaidia, na bado ananisaidia leo. Kwa msaada wa Mungu nimesimama hapa leo na kuwaambia watu kile nilichokiona. Lakini sisemi chochote kipya. Ninasema kile ambacho Musa na manabii walisema kingetokea. 23 Walisema kwamba Masihi atakufa na kuwa wa kwanza kufufuka kutoka kwa wafu. Walisema kwamba ataleta mwanga wa kweli[f] ya Mungu inayowaokoa wote, Wayahudi na wasio Wayahudi.”
Paulo Ajaribu Kumshawishi Agripa
24 Paulo alipokuwa bado anajitetea, Festo alipaza sauti akasema, “Paulo, umerukwa na akili! Kusoma kwingi kumekufanya kichaa.” 25 Paulo akasema, “Mheshimiwa Festo, mimi si kichaa. Ninachokisema ni kweli na kinaingia akilini. 26 Mfalme Agripa analifahamu hili, na ninaweza kuzungumza naye kwa uhuru. Ninafahamu kwamba amekwisha kusikia kuhusu mambo haya, yalitokea mahali ambako kila mtu aliyaona. 27 Mfalme Agripa, unaamini yale ambayo manabii waliandika? Ninajua unaamini!”
28 Mfalme Agripa akamwambia Paulo, “Unadhani unaweza kunishawishi kirahisi kiasi hicho ili niwe Mkristo?”
29 Paulo akasema, “Haijalishi kwangu, ikiwa ni vigumu au rahisi. Ninaomba tu kwa Mungu kwamba si wewe peke yako lakini kila mtu anayenisikiliza leo angeokolewa ili awe kama mimi, isipokuwa kwa minyororo hii!”
30 Mfalme Agripa, Gavana Festo, Bernike, na watu wote waliokaa pamoja nao wakasimama 31 na kuondoka chumbani. Walikuwa wanaongea wenyewe. Walisema, “Mtu huyu hajafanya chochote kinachostahili kuuawa au kuwekwa gerezani.” 32 Kisha Agripa akamwambia Festo, “Tungemwachia huru, lakini ameomba kumwona Kaisari.”
© 2017 Bible League International