Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Beginning

Read the Bible from start to finish, from Genesis to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Matendo 18-20

Paulo Akiwa Korintho

18 Baadaye, Paulo aliondoka Athene na kwenda katika mji wa Korintho. Akiwa huko alikutana na Myahudi aliyeitwa Akila, aliyezaliwa katika jimbo la Ponto. Lakini yeye na mke wake aliyeitwa Prisila, walikuwa tu ndiyo wamehamia Korintho kutoka Italia. Waliondoka Italia kwa sababu Kaisari Klaudio alikuwa ametoa amri Wayahudi wote waondoke Rumi. Paulo alikwenda kuwatembelea Akila na Prisila. Walikuwa watengenezaji wa mahema,[a] kama alivyokuwa Paulo, hivyo alikaa na kufanya kazi pamoja nao.

Kila siku ya Sabato Paulo alikwenda kwenye sinagogi na kuzungumza na Wayahudi na Wayunani, akijaribu kuwashawishi wamwamini Yesu. Lakini baada ya Sila na Timotheo kufika kutoka Makedonia, Paulo alitumia muda wake wote kuuhubiri ujumbe wa Mungu kwa Wayahudi, akiwaeleza kuwa Yesu ndiye Masihi. Lakini walimpinga Paulo na wakaanza kumtukana. Hivyo Paulo akakung'uta mavumbi kutoka kwenye nguo zake.[b] Akawaambia, “Msipookolewa, itakuwa makosa yenu ninyi wenyewe! Nimefanya yote ninayoweza kufanya. Baada ya hili nitawaendea watu wasio Wayahudi tu.”

Paulo aliondoka katika sinagogi na kuhamia nyumbani kwa Tito Yusto, mtu aliyekuwa anamwabudu Mungu wa Kweli, nyumba yake ilikuwa jirani na sinagogi. Krispo aliyekuwa kiongozi wa sinagogi lile, pamoja na watu wote waliokuwa wanaishi nyumbani mwake walimwamini Bwana Yesu. Watu wengi katika mji wa Korintho walimsikiliza Paulo, wakaamini na wakabatizwa.

Wakati wa usiku, Paulo aliona maono. Bwana alimwambia, “Usiogope, na usiache kuzungumza na watu. 10 Niko pamoja nawe, na hakuna atakayeweza kukudhuru. Kuna watu wangu wengi katika mji huu.” 11 Paulo alikaa pale kwa mwaka mmoja na nusu akiwafundisha watu ujumbe wa Mungu.

Paulo Afikishwa Mbele ya Galio

12 Galio alipokuwa gavana wa Akaya, baadhi ya Wayahudi walikusanyika wakawa kinyume cha Paulo. Wakampeleka mahakamani. 13 Wakamwambia Galio, “Mtu huyu anawafundisha watu kumwabudu Mungu kwa namna ambavyo ni kunyume na sheria yetu!”

14 Paulo alikuwa tayari kuzungumza, lakini Galio aliwaambia Wayahudi, “Ningewasikiliza ikiwa malalamiko yenu yangehusu dhuluma au kosa jingine. 15 Lakini yanahusu maneno na majina tu, mabishano yanayohusu sheria zenu wenyewe. Ni lazima mtatue tatizo hili ninyi wenyewe. Sitaki kuwa mwamuzi wa jambo hili.” 16 Hivyo Galio akawafanya waondoke mahakamani.

17 Kisha wote kwa pamoja wakamkamata Sosthenesi, kiongozi wa sinagogi. Wakampiga mbele ya mahakama. Lakini Galio hakulijali hili pia.

Paulo Arudi Antiokia

18 Paulo alikaa na waamini kwa siku nyingi. Kisha aliondoka na kusafiri majini kwenda Shamu. Prisila na Akila walikuwa pamoja naye pia. Walipofika Kenkrea Paulo akanyoa nywele zake kwa sababu aliweka nadhiri[c] kwa Mungu. 19 Kisha walikwenda Efeso, ambako Paulo aliwaacha Prisila na Akila. Paulo alipokuwa Efeso alikwenda katika sinagogi na kuzungumza na Wayahudi. 20 Walimwomba akae kwa muda mrefu lakini alikataa. 21 Aliwaacha na kusema, “Nitarudi tena kwenu ikiwa Mungu atataka nirudi.” Na hivyo akaabili kwenda Efeso.

22 Alipofika Kaisaria, alikwenda Yerusalemu na kulitembelea kanisa pale. Baada ya hapo alikwenda Antiokia. 23 Alikaa Antiokia kwa muda kisha akaondoka akipita katika nchi za Galatia na Frigia. Alisafiri kutoka mji mmoja hadi mji mwingine katika mikoa hii, akiwasaidia wafuasi wa Yesu kuimarika katika imani yao.

Apolo Akiwa Efeso na Korintho

24 Myahudi aliyeitwa Apolo alikuja Efeso. Alizaliwa katika mji wa Iskanderia, alikuwa msomi aliyeyajua Maandiko vizuri. 25 Alikuwa amefundishwa kuhusu Bwana na daima alifurahia[d] kuwaeleza watu kuhusu Yesu. Alichofundisha kilikuwa sahihi, lakini ubatizo alioufahamu ni ubatizo aliofundisha Yohana. 26 Apolo alianza kuzungumza kwa ujasiri katika sinagogi. Prisila na Akila walipomsikia akizungumza, walimchukua wakaenda naye nyumbani mwao kisha wakamsaidia kuielewa njia ya Mungu vizuri zaidi.

27 Apolo alitaka kwenda Akaya. Hivyo waamini wa Efeso wakamsaidia. Waliwaandikia barua wafuasi wa Bwana waliokuwa Akaya wakiwaomba wampokee Apolo. Alipofika pale, alikuwa msaada mkubwa kwa wale waliomwamini Yesu kwa sababu ya neema ya Mungu. 28 Alibishana kwa ujasiri na Wayahudi mbele ya watu wote. Alithibitisha kwa uwazi kuwa wayahudi walikuwa wanakosea. Alitumia Maandiko kuonesha kuwa Yesu ndiye Masihi.

Paulo Akiwa Efeso

19 Apolo alipokuwa katika mji wa Korintho, Paulo alikuwa anatembelea baadhi ya sehemu akiwa njiani kwenda Efeso. Alipofika Efeso waliwakuta baadhi ya wafuasi wa Bwana. Akawauliza, “Mlimpokea Roho Mtakatifu mlipoamini?”

Wafuasi hao wakamwambia, “Hatujawahi hata kusikia kuhusu Roho Mtakatifu!”

Paulo akawauliza, “Kwa hiyo ni mlibatizwa kwa ubatizo gani?”

Wakasema, “Kwa ubatizo aliofundisha Yohana.”

Paulo akasema, “Yohana aliwaambia watu wabatizwe kuonesha kuwa walidhamiria kubadili maisha yao. Aliwaambia watu kuamini katika yule atakaye kuja baada yake, naye huyo ni Yesu.”

Wafuasi hawa waliposikia hili, wakabatizwa katika jina la Bwana Yesu. Kisha Paulo akawawekea mikono, na Roho Mtakatifu akaja juu yao. Wakaanza kuzungumza na kutabiri katika lugha tofauti. Walikuwepo wanaume kama kumi na mbili katika kundi hili.

Paulo akaingia katika sinagogi na akazungumza kwa ujasiri. Aliendelea kufanya hivi kwa miezi mitatu. Alizungumza na Wayahudi, akijaribu kuwashawishi kukubali alichokuwa anawaambia kuhusu ufalme wa Mungu. Lakini baadhi yao wakawa wakaidi, wakakataa kuamini. Waliikashifu Njia[e] ya Bwana mbele ya kila mtu. Hivyo Paulo aliwaacha Wayahudi hawa na kuwachukua wafuasi wa Bwana pamoja naye. Alikwenda mahali ambapo mtu aitwaye Tirano alikuwa na shule. Hapo Paulo alizungumza na watu kila siku. 10 Alifanya hivi kwa miaka miwili na kila mtu aliyeishi Asia, Wayahudi na Wayunani alilisikia neno la Bwana.

Wana wa Skewa

11 Mungu alimtumia Paulo kufanya miujiza ya kipekee. 12 Baadhi ya watu walichukua vitambaa vya mkononi na nguo zilizovaliwa na Paulo na kuziweka juu ya wagonjwa. Wagonjwa waliponywa na pepo wabaya waliwatoka watu.

13-14 Pia baadhi ya Wayahudi walikuwa wanasafiri huku na huko wakiwatoa pepo wabaya kwa watu. Wana saba wa Skewa, mmoja wa viongozi wa makuhani, walikuwa wakifanya hili. Wayahudi hawa walijaribu kutumia jina la Bwana kuyatoa mapepo kwa watu. Wote walikuwa wanasema, “Katika jina la Bwana Yesu anayezungumzwa na Paulo ninakuamuru utoke!”

15 Lakini wakati fulani pepo akawaambia Wayahudi hawa, “Ninamfahamu Yesu, na ninafahamu kuhusu Paulo, na ninyi ni nani?”

16 Kisha mtu aliyekuwa na pepo ndani yake akawarukia. Alikuwa na nguvu kuliko wote. Akawapiga, akawachania nguo za na kuwavua, nao wakakimbia kutoka katika nyumba ile wakiwa uchi.

17 Watu wote katika Efeso, Wayahudi na Wayunani wakafahamu kuhusu hili. Wakaogopa na kumtukuza Bwana Yesu. 18 Waamini wengi walianza kukiri, wakisema mambo yote maovu waliyotenda. 19 Baadhi yao walikuwa wametumia uchawi huko nyuma. Waamini hawa walileta vitabu vyao vya uchawi na kuvichoma mbele ya kila mtu. Vitabu hivi vilikuwa na thamani ya sarafu hamsini elfu za fedha.[f] 20 Hivi ndivyo ambavyo neno la Bwana lilikuwa linasambaa kwa nguvu, likisababisha watu wengi kuamini.

Paulo Apanga Safari

21 Baada ya hili, Paulo alipanga kwenda Yerusalemu. Alipanga kupitia katika majimbo ya Makedonia na Akaya kisha kwenda Yerusalemu. Alisema, “Baada ya kwenda Yerusalemu, ni lazima niende Rumi pia.” 22 Timotheo na Erasto walikuwa wasaidizi wake wawili. Paulo aliwatuma watangulie Makedonia. Lakini yeye alikaa Asia kwa muda.

Tatizo Katika Mji wa Efeso

23 Lakini katika wakati huo huo kulikuwepo tatizo kuhusiana na Njia. Hivi ndivyo ilivyotokea: 24 Alikuwepo mtu aliyeitwa Demetrio aliyekuwa mfua fedha. Alikuwa akitengeneza sanamu ndogo za fedha zilizofanana na hekalu la Artemi, mungu mke. Wanaume waliokuwa wakifanya kazi hii walijipatia pesa nyingi sana.

25 Demetrio alifanya mkutano na watu hawa pamoja na wengine waliokuwa wanafanya kazi ya aina hiyo. Akawaambia, “Ndugu, mnafahamu kuwa tunapata pesa nyingi kutokana na kazi yetu. 26 Lakini angalieni kitu ambacho mtu huyu Paulo anafanya. Sikilizeni anachosema. Amewashawishi watu wengi katika Efeso na karibu Asia yote kubadili dini zao. Anasema miungu ambayo watu wanatengeneza kwa mikono si miungu wa kweli. 27 Ninaogopa hili litawafanya watu kuwa kinyume na biashara yetu. Lakini kuna tatizo jingine pia. Watu wataanza kufikiri kuwa hekalu la Artemi, mungu wetu mkuu halina maana. Ukuu wake utaharibiwa. Na Artemi ni mungu mke anayeabudiwa na kila mtu katika Asia na ulimwengu wote.”

28 Waliposikia hili, walikasirika sana. Wakapaza sauti zao wakisema, “Artemi, mungu mke wa Efeso ni mkuu!” 29 Mji wote ukalipuka kwa vurugu. Watu wakawakamata Gayo na Aristarko, waliotoka Makedonia waliokuwa wanasafiri na Paulo, wakawapeleka kwenye uwanja wa mji. 30 Paulo alitaka kwenda ili azungumze na watu, lakini wafuasi wa Bwana walimzuia. 31 Pia, baadhi ya viongozi katika jimbo la Asia waliokuwa rafiki zake walimtumia ujumbe wakimwambia asiende uwanjani.

32 Watu wengi walikuwa akipiga kelele kusema hili na wengine walisema jambo jingine. Mkutano ukawa na vurugu kubwa. Watu wengi hawakujua ni kwa nini walikwenda pale. 33 Baadhi ya Wayahudi wakamshawishi mtu mmoja aliyeitwa Iskanda asimame mbele ya umati, wakamwelekeza cha kusema. Iskanda alipunga mkono wake, akijaribu kuwaeleza watu jambo. 34 Lakini watu walipoona kuwa Iskanda ni Myahudi, wote wakaanza kupiga kelele ya aina moja. Kwa masaa mawili waliendelea kusema, “Artemi, mungu mke wa Efeso ni mkuu!”

35 Ndipo karani wa mji akawashawishi watu kunyamaza. Akawaambia, “Watu wa Efeso, kila mtu anafahamu kwamba Efeso ndiyo mji unaotunza hekalu la mungu mkuu mke Artemi. Kila mtu anafahamu pia kwamba tunatunza mwamba wake mtakatifu.[g] 36 Hakuna anayeweza kupinga hili, hivyo mnyamaze. Ni lazima mtulie na kufikiri kabla hamjafanya kitu chochote.

37 Mmewaleta watu[h] hawa hapa, lakini hawajasema kitu chochote kibaya kinyume na mungu wetu mke. Hawajaiba kitu chochote kutoka kwenye hekalu lake. 38 Tuna mahakama za sheria na wapo waamuzi. Je, Demetrio na watu hawa wanaofanya kazi pamoja naye wana mashitaka dhidi ya yeyote? Wanapaswa kwenda mahakamani wakawashtaki huko.

39 Kuna kitu kingine mnataka kuzungumzia? Basi njooni kwenye mikutano ya kawaida ya mji mbele ya watu. Litaweza kuamuriwa huko. 40 Ninasema hivi kwa sababu mtu mwingine anaweza kuona tukio hili la leo na akatushtaki kwa kuanzisha ghasia. Hatutaweza kufafanua vurugu hii, kwa sababu hakuna sababu za msingi za kuwepo mkutano huu.” 41 Baada ya karani wa mji kusema hili, aliwaambia watu kwenda majumbani mwao.

Paulo Aenda Makedonia na Uyunani

20 Ghasia zilipokwisha, Paulo aliwaalika wafuasi wa Bwana kuja kumtembelea. Baada ya kuwatia moyo, aliwaaga na kuondoka kwenda Makedonia. Katika safari yake kupitia Makedonia alikuwa na maneno mengi ya kuwatia moyo wafuasi sehemu mbalimbali. Kisha alikwenda Uyunani na alikaa huko kwa miezi mitatu.

Alipokuwa tayari kutweka tanga kwenda Shamu, baadhi ya Wayahudi walikuwa wanapanga kitu kinyume naye. Hivyo aliamua kurudi nyuma kwenda Shamu kupitia Makedonia. Watu hawa walikuwa wanasafiri pamoja naye: Sopata, mwana wa Piro, kutoka mji wa Berea; Aristarko na Sekundo, kutoka mji wa Thesalonike; Gayo, kutoka mji wa Derbe; Timotheo; na watu wawili kutoka Asia, Tikiko na Trofimo. Watu hawa walimtangulia Paulo. Walitusubiri katika mji wa Troa. Baada ya Siku kuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu tulitweka tanga kutoka katika mji wa Filipi. Tuliwakuta watu hawa katika mji wa Troa siku tano baadaye na tulikaa pale kwa siku saba.

Paulo Atembelea Troa Mara ya Mwisho

Siku ya Jumapili[i] sote tulikusanyika pamoja kula Meza ya Bwana.[j] Paulo alizungumza na kundi. Kwa sababu alipanga kuondoka siku iliyofuata, aliendelea kuzungumza mpaka usiku wa manane. Tulikuwa wote kwenye chumba ghorofani na kulikuwa taa nyingi chumbani. Alikuwepo kijana mmoja aliyekuwa amekaa dirishani aliyeitwa Eutiko. Paulo aliendelea kuzungumza, na Eutiko alianza kuchoka na kusikia ungungizi. Mwishowe alisinzia na kuanguka. Alianguka chini, nje kutoka ghorofa ya tatu. Watu walipokwenda kumnyenyua alikuwa amekwisha kufa.

10 Paulo alishuka, akaenda mahali alipokuwa Eutiko, akapiga magoti, na akamkumbatia. Akawaambia waamini wengine, “Msiwe na hofu. Ni mzima yuko hai sasa.” 11 Kisha Paulo akapanda ghorofani, akamega baadhi ya mikate na kula. Alizungumza nao kwa muda mrefu. Alimaliza kuzungumza mapema asubuhi na akaondoka. 12 Wafuasi wa Bwana walimpeleka Eutiko nyumbani akiwa hai, walifarijika sana wote.

Safari Kutoka Troa kwenda Mileto

13 Tulimtangulia Paulo, tukatweka tanga kwenda Asso, tulipanga kumkuta huko. Alitwambia tufanye hivi kwa sababu alitaka kusafiri kwa nchi kavu. 14 Alipotukuta Asso, aliungana nasi na tulipanda meli pamoja naye, na sote tulitweka tanga kwenda Mitelene. 15 Siku iliyofuata, tulitweka tanga kutoka pale na kufika karibu na kisiwa cha Kio. Kisha siku iliyofuata tulitweka tanga kwenda kwenye kisiwa Samosi. Baada ya siku moja tukafika kwenye mji wa Mileto. 16 Paulo alikwisha amua kutosimama Efeso. Hakutaka kukaa Asia kwa muda mrefu. Alikuwa anaharakisha kwa sababu alitaka ikiwezekana awe Yerusalemu siku ya Pentekoste.

Paulo Azungumza na Wazee kutoka Efeso

17 Tukiwa Mileto Paulo alitume ujumbe kwenda Efeso, akiwaambia wazee wa kanisa la Efeso waje kwake.

18 Walipofika, Paulo akawaambia, “Mnafahamu kuhusu maisha yangu tangu siku ya kwanza nilipofika Asia. Mnafahamu namna nilivyoishi wakati wote nilipokuwa pamoja nanyi. 19 Wayahudi walipanga hila kinyume nami, na hila zao zilinisababishia matatizo mengi. Lakini mnafahamu kwamba daima nilimtumikia Bwana, nyakati zingine kwa machozi. Sikujipendelea mimi mwenyewe kwanza. 20 Daima niliwatendea mema. Niliwahubiri Habari Njema kuhusu Yesu sehemu za wazi mbele ya watu na pia nilifundisha katika nyumba zenu. 21 Nilimwambia kila mtu, Myahudi na Myunani, kubadilika na wakamgeukia Mungu. Niliwaambia wote wamwamini Bwana wetu Yesu.

22 Lakini sasa ni lazima nimtii Roho na kwenda Yerusalemu. Sifahamu nini kitanipata huko. 23 Ninafahamu kitu kimoja kwamba katika kila mji Roho Mtakatifu huniambia kwamba matatizo na hata kufungwa gerezani kunanisubiri. 24 Siujali uhai wangu mwenyewe. Jambo la muhimu zaidi ni mimi kuimaliza kazi yangu. Ninataka niimalize huduma ambayo Bwana Yesu alinipa niifanye, nayo ni kuwahubiri watu Habari Njema kuhusu neema ya Mungu.

25 Na sasa nisikilizeni. Ninafahamu kwamba hakuna mmoja wenu atakayeniona tena. Wakati wote nilipokuwa pamoja nanyi, niliwahubiri Habari Njema kuhusu ufalme wa Mungu. 26 Hivyo leo ninaweza kuwaambia kitu kimoja ambacho nina uhakika nacho: Mungu hatanilaumu ikiwa baadhi yenu hamtaokoka. 27 Ninaweza kusema hivi kwa sababu ninajua niliwaambia yote ambayo Mungu anataka mfahamu. 28 Jilindeni ninyi wenyewe pamoja na watu wote mliopewa na Mungu. Naye Roho Mtakatifu amewapa ninyi kazi ya kuwachunga[k] kondoo hawa.[l] Ni lazima muwe wachungaji wa kanisa la Mungu,[m] watu ambao Mungu aliwanunua kwa damu ya Mwanaye wa pekee.[n] 29 Ninafahamu ya kwamba nikishaondoka, baadhi ya watu watakuja kwenye kundi letu. Watakuwa kama mbwa mwitu na watajaribu kuwaangamiza kondoo. 30 Pia, watu kutoka kwenye kundi lenu wenyewe wataanza kufundisha mambo yasiyo sahihi. Watawaongoza baadhi ya wafuasi wa Bwana mbali na kweli ili wawafuate katika upotovu wao. 31 Hivyo iweni waangalifu! Na daima kumbukeni mambo niliyofanya kwa miaka mitatu nilipokuwa pamoja nanyi. Sikuacha kumkumbusha kila mmoja wenu jinsi anavyopaswa kuishi, nikiwashauri usiku na mchana na kulia kwa ajili yenu.

32 Sasa ninawaweka katika uangalizi wa Mungu. Ninategemea ujumbe wa neema yake kuwaimarisha ninyi. Ujumbe huo unaweza kuwapa ninyi baraka ambazo Mungu huwapa watakatifu wake wote. 33 Nilipokuwa pamoja nanyi, sikutamani pesa ya mtu yeyote au nguo nzuri. 34 Mnafahamu kwamba daima nilifanya kazi kwa mikono yangu mwenyewe ili nimudu mahitaji yangu mwenyewe na mahitaji ya watu waliokuwa pamoja nami. 35 Daima niliwaonesha kwamba mnapaswa kufanya kazi nilivyofanya na kuwasaidia wadhaifu. Niliwafundisha kukumbuka maneno ya Bwana Yesu aliyosema, ‘Ni baraka kuu kutoa kuliko kupokea.’”

36 Paulo alipomaliza kuzungumza, alipiga magoti chini, na wote waliomba pamoja. 37-38 Walilia sana. Kilichowahuzunisha sana ilikuwa kauli ya Paulo alipowaambia kuwa hawatamwona tena. Walimkumbatia na kumbusu. Kisha walikwenda pamoja naye mpaka kwenye meli na wakaagana naye.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International