Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Beginning

Read the Bible from start to finish, from Genesis to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Matendo 14-15

Paulo na Barnaba Wakiwa Ikonia

14 Paulo na Barnaba walikwenda katika mji wa Ikonia. Kama walivyofanya Antiokia, waliingia katika sinagogi la Kiyahudi. Walizungumza na watu pale. Walizungumza kwa ushawishi sana kiasi kwamba Wayahudi na Wayunani wengi waliamini walichosema. Lakini Baadhi ya Wayahudi hawakuamini. Wayahudi hao walisema mambo yaliyowafanya wasio Wayahudi kukasirika na kuwa kinyume na waamini.

Hivyo Paulo na Barnaba walikaa Ikonia kwa muda mrefu, na walihubiri kwa ujasiri kwa ajili ya Bwana. Waliwahubiri watu kuhusu neema ya Mungu. Bwana alithibitisha kwamba kile walichosema ni kweli kwa ishara na maajabu yaliyofanyika kufanyika kupitia wao. Lakini baadhi ya watu katika mji wakakubaliana na Wayahudi ambao hawakuwaamini Paulo na Barnaba. Baadhi walikubaliana na mafundisho ya mitume. Hivyo mji uligawanyika.

Baadhi ya Wayahudi, viongozi wao na baadhi ya watu wasio wayahudi, walidhamiria kuwaumiza Paulo na Barnaba. Walitaka kuwaua kwa kuwapiga kwa mawe. Paulo na Barnaba walipotambua kuhusu hili, wakaondoka katika mji huo. Walikwenda Listra na Derbe, miji katika Likonia na maeneo yanayozunguka Likonia. Wakahubiri Habari Njema huko pia.

Paulo na Barnaba Wakiwa Listra na Derbe

Katika mji wa Listra kulikuwa mtu aliyekuwa na tatizo katika mguu wake. Alizaliwa akiwa mlemavu wa miguu na hakuwahi kutembea. Alikuwa amekaa akimsikiliza Paulo akizungumza. Paulo alipomwangalia kwa kumkazia macho alitambua kuwa mtu huyo alikuwa na imani kuwa Mungu angemponya. 10 Hivyo Paulo akapaza sauti na kumwambia, “Simama kwa miguu yako!” Mtu yule akaruka na kuanza kutembea.

11 Watu walipoona alichofanya Paulo, walipaza sauti kwa lugha yao wenyewe ya Kilikaonia. Walisema, “Miungu wamekuja kwetu katika maumbo ya kibinadamu!” 12 Watu wakaanza kumwita Barnaba “Zeusi”, na Paulo “Hermesi”, kwa sababu ndiye alikuwa mzungumzaji mkuu. 13 Hekalu la Zeusi lilikuwa karibu na mji. Kuhani wa hekalu hili alileta mafahari ya ng'ombe kadhaa na mashada ya maua[a] kwenye lango la mji. Kuhani na watu walitaka kuwatolea sadaka Paulo na Barnaba.

14 Lakini mitume, Barnaba na Paulo walipoelewa jambo ambalo watu walikuwa wanafanya, walirarua mavazi yao.[b] Kisha wakakimbia kuingia katikati ya watu na kuwaambia kwa kupaza sauti zao wakisema: 15 “Ndugu, kwa nini mnafanya hivi? Sisi si miungu. Ni wanadamu kama ninyi. Tulikuja kuwaambia Habari Njema. Tunawaambia mviache vitu hivi visivyo na thamani. Mgeukieni Mungu wa kweli aishiye, aliyeumba mbingu, nchi, bahari na vyote vilivyomo ndani yake.

16 Huko nyuma Mungu aliyaacha mataifa yote yatende yale waliyotaka. 17 Lakini daima Mungu alikuwepo na alitenda mambo mema yanayothibitisha kuwa yeye ni wa hakika na wa kweli. Huwapa mvua kutoka mbinguni na mavuno bora kwa wakati sahihi. Huwapa chakula tele na kuijaza mioyo yenu kwa furaha.”

18 Hata baada Paulo na Barnaba kusema hayo, hawakuweza kuwazuia watu kuwatolea sadaka za kuteketezwa.

19 Ndipo baadhi ya Wayahudi wakaja kutoka Antiokia na Ikonia na kuwashawishi watu ili wampinge Paulo. Hivyo wakamtupia mawe na kumburuza kumtoa nje ya mji. Wakidhani kuwa wamemwua. 20 Lakini wafuasi wa Yesu walipokusanyika kumzunguka, aliamka na kuingia mjini. Siku iliyofuata yeye na Barnaba waliondoka na kwenda katika mji wa Derbe.

Kurudi Antiokia ya Shamu

21 Walihubiri pia Habari Njema katika mji wa Derbe, na watu wengi wakawa wafuasi wa Yesu. Kisha Paulo na Barnaba walirudi katika miji ya Listra, Ikonia na Antiokia. 22 Katika miji hiyo waliwasaidia wafuasi kukua na kuwa na nguvu katika imani yao na waliwatia moyo kuendelea kumwamini Mungu. Waliwaambia, “Ni lazima tuteseke kwa mambo mengi katika safari yetu ya kwenda katika ufalme wa Mungu.” 23 Waliwachagua pia wazee katika kila kanisa na kuacha kula kwa muda ili kuwaombea. Wazee hawa walikuwa wanaume wanaomtumaini Bwana Yesu, hivyo Paulo na Barnaba wakamwomba Bwana awalinde.

24 Paulo na Barnaba walipita katikati ya eneo la Pisidia. Kisha walifika katika jimbo la Pamfilia. 25 Waliwahubiri watu ujumbe wa Mungu katika mji wa Perge, kisha wakateremka kwenda katika mji wa Attalia. 26 Na kutoka huko wakatweka tanga kwenda katika mji wa Antiokia ya Shamu. Huu ni mji ambako waamini waliwaweka katika uangalizi wa Mungu na kuwatuma kufanya kazi hii. Na sasa walikuwa wameimaliza.

27 Paulo na Barnaba walipofika, walilikusanya kanisa pamoja. Waliwaambia waamini yote ambayo Mungu aliwatumia kutenda. Walisema, “Mungu amefungua mlango kwa watu wasio Wayahudi kuamini!” 28 Na walikaa pale pamoja na wafuasi wa Bwana kwa muda mrefu.

Mkutano Yerusalemu

15 Kisha baadhi ya watu kutoka Uyahudi wakaja Antiokia na kuanza kuwafundisha jamii ya waamini wasio Wayahudi, wakisema, “Hamwezi kuokolewa ikiwa hamkutahiriwa kama Musa alivyotufundisha.” Paulo na Barnaba wakayapinga mafundisho haya na wakahojiana na kubishana na watu hawa juu ya hili. Hivyo kundi la waamini likaamua kuwatuma Paulo, Barnaba, na baadhi ya watu wengine Yerusalemu ili kujadiliana na mitume na wazee kuhusu suala hili.

Kanisa liliwapa wale waliotumwa kila kitu walichohitaji kwa ajili ya safari yao. Walisafiri kupitia maeneo ya Foeniki na Samaria, ambako walieleza kwa undani mambo yote namna ambavyo wasio Wayahudi wamemgeukia Mungu wa kweli. Habari hii iliwafurahisha waamini wote. Walipofika Yerusalemu, mitume, wazee na kanisa lote waliwakaribisha. Paulo, Barnaba, na wengine wakaeleza yote ambayo Mungu alitenda kupitia wao. Baadhi ya waamini mjini Yerusalemu waliokuwa Mafarisayo,[c] walisimama na kusema, “Waamini wasio Wayahudi lazima watahiriwe. Ni lazima tuwaambie waitii Sheria ya Musa!”

Ndipo mitume na wazee wakakusanyika kulichunguza jambo hili. Baada ya majadiliano ya muda mrefu, Petro akasimama na kuwaambia, “Ndugu zangu, nina uhakika mnakumbuka kilichotokea siku za nyuma. Mungu alinichagua kutoka miongoni mwenu kuzihubiri Habari Njema kwa watu wasio Wayahudi. Kupitia mimi walisikia Habari Njema na kuamini. Mungu anamfahamu kila mtu, hata mawazo yao, na amewakubali watu hawa wasio Wayahudi. Amelionyesha hili kwetu kwa kuwapa Roho Mtakatifu kama alivyotupa sisi. Mbele za Mungu, wasio Wayahudi hawako tofauti na sisi. Mungu aliisafisha mioyo yao walipoamini. 10 Kwa nini sasa mnawatwisha mzigo mzito kwenye shingo zao? Je, mnajaribu kumkasirisha Mungu? Sisi na baba zetu hatukuweza kuubeba mzigo huo. 11 Hapana, tunaamini kuwa sisi na watu hawa tutaokolewa kwa namna moja iliyo sawa, ni kwa neema ya Bwana Yesu.”

12 Ndipo kundi lote likawa kimya. Waliwasikiliza Paulo na Barnaba walipokuwa wanaeleza kuhusu ishara na maajabu ambayo kupitia wao Mungu aliwatendea watu wasio Wayahudi. 13 Walipomaliza kusema, Yakobo akasema, “Ndugu zangu, nisikilizeni. 14 Simoni Petro ametueleza namna ambavyo siku za mwanzoni Mungu alilionyesha pendo lake kwa watu wasio Wayahudi, kwa kuwakubali na kuwafanya kuwa watu wake. 15 Maneno ya manabii yanakubaliana na hili:

16 ‘Nitarudi baada ya hili.
    Nitaijenga nyumba ya Daudi tena.
    Imeanguka chini.
Nitazijenga tena sehemu za nyumba yake zilizoangushwa chini.
    Nitaifanya nyumba yake kuwa mpya.
17 Kisha wanadamu wengine wote,
    watu niliowachagua kutoka mataifa mengine,
    watataka kunifuata mimi, Bwana.
Hivi ndivyo Bwana anasema,
    naye ndiye afanyaye mambo haya yote.’(A)
18     ‘Haya yote yalijulikana tangu zamani.’[d]

19 Hivyo nadhani tusiyafanye mambo kuwa magumu kwa wasio Wayahudi waliomgeukia Mungu. 20 Badala yake, tuwatumie barua kuwaambia mambo ambayo hawapaswi kutenda:

Wasile chakula kilichotolewa kwa sanamu maana chakula hiki huwa najisi.[e]

Wasijihusishe na dhambi ya zinaa.

Wasile nyama inayotokana na wanyama walionyongwa au nyama ambayo bado ina damu ndani yake.

21 Wasitende mojawapo ya mambo haya, kwa sababu bado kuna watu katika kila mji wanaofundisha Sheria ya Musa. Maneno ya Musa yamekuwa yakisomwa katika masinagogi kila siku ya Sabato kwa miaka mingi.”

Barua kwa Waamini Wasio Wayahudi

22 Mitume, wazee na kanisa lote wakataka kuwatuma baadhi ya watu wafuatane na Paulo na Barnaba kwenda Antiokia. Wakawachagua baadhi ya watu kutoka miongoni mwao wenyewe. Waliwachagua Yuda (ambaye pia aliitwa Barsaba) na Sila, watu walioheshimiwa na waamini. 23 Kundi la waamini likaandika barua na kuwatuma watu hawa. Barua ilisema:

Kutoka kwa mitume na wazee, ndugu zenu.

Kwa ndugu wote wasio Wayahudi katika mji wa Antiokia na katika majimbo ya Shamu na Kilikia.

Ndugu Wapendwa:

24 Tumesikia kuwa baadhi ya watu kutoka kwetu walikuja kwenu. Walichosema kiliwasumbua na kuwaudhi. Lakini hatukuwaambia kufanya hili. 25 Sisi sote tumekubaliana kuwachagua baadhi ya watu na kuwatuma kwenu. Watakuwa na rafiki zetu wapendwa, Barnaba na Paulo. 26 Barnaba na Paulo wameyatoa maisha yao kumtumikia Bwana wetu Yesu Kristo. 27 Hivyo tumewatuma Yuda na Sila pamoja nao. Watawaambia mambo yanayofanana. 28 Imempendeza Roho Mtakatifu na sisi kwamba tusiwatwishe mizigo ya ziada, isipokuwa kwa mambo haya ya muhimu:

29 Msile chakula kilichotolewa kwa sanamu.

Msile nyama inayotokana na wanyama walionyongwa au nyama ambayo bado ina damu ndani yake.

Msijihusishe na uzinzi.

Mkijitenga na mambo haya, mtakuwa mnaenenda vyema.

Wasalamu.

30 Hivyo Paulo, Barnaba, Yuda, na Sila waliondoka Yerusalemu na kwenda Antiokia. Walipofika huko walilikusanya kundi la waamini pamoja na wakawapa barua. 31 Waamini walipoisoma, wakafurahi na kufarijika. 32 Yuda na Sila ambao pia walikuwa manabii, waliwatia moyo waamini kwa maneno mengi na kuwafanya waimarike katika imani yao. 33 Baada ya Yuda na Sila kukaa pale kwa muda, waliondoka. Waamini waliwaruhusu waende kwa amani kisha wakarudi Yerusalemu kwa wale waliowatuma. 34 [f]

35 Lakini Paulo na Barnaba walikaa Antiokia. Wao na wengine wengi waliwafundisha waamini na kuwahubiri watu wengine Habari Njema kuhusu Bwana.

Paulo na Barnaba Watengana

36 Wakati fulani baadaye, Paulo akamwambia Barnaba, “Turudi katika miji yote tulikowahubiri watu ujumbe wa Bwana. Tuwatembelee waamini tuone wanaendeleaje.”

37 Barnaba alitaka Yohana Marko afuatane nao pia. 38 Lakini Yohana Marko hakukaa nao mpaka mwisho katika safari ya kwanza. Aliwaacha Pamfilia. Hivyo Paulo alisisitiza kuwa wasiende pamoja naye wakati huu. 39 Paulo na Barnaba walikuwa na mjadala mkali kuhusu hili. Ulikuwa mbaya sana ikabidi watengane na kwenda njia tofauti. Barnaba akatweka tanga kwenda Kipro, akamchukua Marko pamoja naye.

40 Paulo alimchagua Sila kwenda naye. Waamini Antiokia walimweka Paulo katika uangalizi wa Bwana na kumtuma. 41 Paulo na Sila walikwenda kwa kupitia katika majimbo ya Shamu na Kilikia, wakiyasaidia makanisa kuimarika.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International